NA BAKAR MUSSA, PEMBA:::
HEDHI ni hali ya mabadiliko katika mwili wa mwanawake ambayo hutayarisha nyumba
ya uke kupata ujauzito.
Kila mwezi mji wa uzazi hupata kokwa ambapo mwanamke akipata
ujauzito, mtoto ataweza kukuwa.
Ingawaje mwanamke asipo pata ujauzito, kokwa haihitajiki damu
itatokea ukeni na hiyo huitwa damu ya hedhi.
Wanawake wengi walio komaa, hupata hedhi, na wasichana hupata hedhi zao kati ya
miaka tisa (9) na miaka 16, lakini huacha kupata hedhi wanapotimia miaka 50.
Mwanamke, akiwa na hedhi anapaswa kutumia visodo au pedi kuzuia damu, ambazo
zimeundwa na vifaa vya laini zinazo nyonya damu hiyo.
Kutokana na umuhimu wa jambo hilo Umoja wa Mataifa imetenga kila tarehe
28 mwezi Mei, dunia huadhimisha siku ya hedhi safi na salama.
Usafi ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu, awe mke au mume lakini
mwanamke inasisitizwa sana, kwa vile akifikia balegh huingia katika mazingira
fulani ambayo humlazimu kila wakati kuhakikisha yuko msafi.
Wizara ya Elimu ndio mlezi mkubwa watoto, kwani hupata fursa ya kuwa nao kwa
muda mrefu, hata kuliko kwenye familia zao ingawaje baadhi ya wakati wanafunzi
hao wenye jinsia ya kike hukumbana na changamoto inayotokana na maumbile yao(Hedhi).
Itoshe kuzungunzia hilo ila tuone Wizara ya Elimu na mafunzo ya amali Pemba,
inavyochukuwa juhudi ya kukabiliana na suala hilo kwa wanafunziwakiwa skulini.
Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim,
akizungumza na makala hii anasema, wizara imekuwa ikichukuwa juhudi ya
kupambana na hedhi salama kwa wanafunzi, kwakuwapa stadi za maisha ‘ABC’ .
Anaeleza kuwa stadi za maisha hizo ni pamoja na kujitambuwa na udhalilishaji,
kuwa salama na hedhi na kuimarisha miundo mbinu hususan yyoo.
Jengine anasema wapo waalimu wa kutosha wa ushauri nasaha wa
msingi na sekondari, akimaanisha kila skuli lazima wawepo waalimu kati mmoja
hadi wawili.
Kutokana na umuhimu wa kuwahifadhi wanafunzi wa kike waliofikia katika kuingia
kwenye hedhi, wameamuwa kuwa na Ped za muda mrefu, kwa kuwafundisha kushona
wenyewe na baadae kuzisafisha.
wakati mwengine hupata misaada mbali mbali ya PED na hivi sasa wanazo 3000
ambazo watazigawa kwa wanafunzi walioko katika dakhalia (mabweni) kwa wanafunzi
wastani wa 314 kisiwani Pemba pekee.
Anafahamisha kuwa wanafunzi wa kike ambao wanatumia vifaa hivyo ni wengi, kwani
hadi Septemba mwaka 2022 kutoka kidato cha kwanza hadi cha sita kwa Pemba wako
wanafunzi 19,649 na Chuo cha Kiislamu pekee wako wasichana 488.
“ Hizi tulizonazo ni kidogo kulingana na idadi ya wanafunzi wa watu wa kike
tulionao, ingawa tutaendelea kutafuta wafadhili wengine ili waweze kutusaidia
na kuwapatia wanafunzi wetu”, anaeleza.
Ofisa mdhamini huyo anasema kuwepo kwa vifaa hivyo (Ped) litaondosha kabisa
suala la wanafunzi ambao wamekuwa wakikata masomo kutokana na kupata siku zao
za kawaida Hedhi.
“Suala hili la wanafunzi kukata masomo kutokana na kuingia katika kawaida yao (wanapopata
hedhi) lipo, lakini limekuwa likiondoka kidogo kidogo na wizara inaendelea
kupambana nalo.
Sasa akawaelekea wazazi na walezi watoe ushirikiano na hasa wasiwakatishe
masomo wanafunzi kutokana na tatizo hilo waendelee kuwaamini kwani, wamewaandaliwa
mazingira salama.
Ofisa huyo anaeleza wamekuwa wakipata wahisani mbali mbali wanaotowa elimu ya
kujihifadhi kwa wanafunzi wa kike kama vile TAMWA, UNICEF na Serikali wenyewe.
Ofisa ushauri nasaha wa kujitegemea kisiwani Pemba Sabahi Mussa Said
anasema, wamekuwa mstari wa mbele kutowa ushauri nasaha pale wanapokutana
na wanafunzi ili kukabiliana na hali hiyo.
Anaeleza kuwa mbali na wizara ya elimu kuchukuwa juhudi katika kukabiliana na
tatizo hilo, lakini zimekuwepo na taasisi mbali mbali, ambazo hutoa mafunzo kwa
walimu iliwaweze kukabiliana na suala la hedhi salama kwa wanafunzi.
“Ushauri nasaha umekuwa juu ya tatizo hili, umekuwa ukitolewa na taasisi mbali
mbali, kwani sio jambo la mtu mmoja unapomuelimisha mwanamke mmoja ni sawa
kuielimisha jamii mzima”, alisema.
Mfano wa taasisi hiyo ni KFHI ( yaani mradi wa wajengea uwezo walimu
katika mazingira rafiki ya moto wa kike) unaofadhiliwa na Korea ambao kwa
Zanzibar umeshatowa mafunzo kwa skuli 5.
Ikiwa ni pamoja na kwa Pemba skuli ya sekondari Shumba Vyamboni
na Chwaka Tumbe sekondari.
Ambapo mkurugenzi wa mradi huo Esther Mwakarobo anaeleza kuwa lengo la
mradi huo, ni kutaka kutengeneza mazingira rafiki kwa wanafunzi hasa wa kike.
Hasa wakati anapokuwa skuli, ambapo itasaidia kuondoa changamoto
ambazo zinaweza kujitokeza, wakati wakiwa katika kipindi cha Hedhi.
Esther anasema, kuwa wameamua kuendesha mradi huo kwa upande wa Zanzibar,
kutokana na kuona kuna uhitaji na kuangalia miundombinu iliyopo, katika skuli
hizo ina mapungufu.
“ Mradi wetu huu tutauwendesha katika Skuli tano za Zanzibar, ikiwa Pemba ni
Skuli ya Sekondari Chwaka Tumbe na Skuli ya Sekondari Shumba Vyamboni huku
Unguja ni Paje Mtule, Fukuchani na Jendele," alisema Park.
Anafahamisha usafi usipozingatia katika kipindi cha Hedhi kunaweza kusababisha
maambukizi katika mfumo wa uzazi na kwenye njia ya mkojo hivyo huathiri afya ya
mwanafunzi.
“Tunavyozidi kukuwa mabadiliko mbali mbali ya matokeo ya miili yetu hutokea
ikiwemo hedhi kwa Wasichana , mabadiliko haya ni kawaida na husababishwa na
vichecheo ndani ya miili yetu”, anaeleza.
Anasema ni muhimu kuweka miili ya wasichana katika hali ya usafi kwa kipindi
chote cha Hedhi kwa kutumia taulosafi za wasichana ambazo wanaweza
kuzitengeneza majumbani au kununuwa madukani.
Nae Taiwa Park kutoka mradi huo wa KFHI unaofadhiliwa na KOICA na kwa ushirikiano
na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar anaeleza kuwa mradi huoutakuwa ni wa
miaka (3) na utatoa elimu kwa wanafunzi wapatao 1,300 na walimu 100 kwa Skuli
tano (5).
“ Tumeamuwa kutowa mafunzo haya kwa walimu na wanafunzi ili
kuwawezesha wanafunzi kuweza kujitambuwa zaidi na kutumia vifaa ambavyo vitawasaidia kujistiri wakati wa hedhi na watapata kuhudhuria masomo kama kawaida na sio kukata kata kila mwezi”, anasema.
Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Shumba Vyamboni Khatib Rashid Mwinyi alieleza kuwa katika Skuli yake, yako matatizo mbali mbali ambayo huwa yanawakabili watoto wa kike hasa pale wanapokuwa katika hedhi.
"Mara nyingi watoto wa kike wanapopata hedhi wakiwa Skuli kiukweli hatujui nini cha kufanya, lakini kupitia elimu tuliyoipata ni dhahiri tutaweza kuitumia vyema katika mazingira yetu ya Skuli kwa watoto wetu," alisema.
Nae Mwalimu mkuu wa skuli ya sekondari Chwaka Tumbe Hamad Dadi Khamis, anasema kuwa mafunzo hayo wataweza kuyatumia vizuri, kwa kuwahamasisha wanafunzi pamoja na jamii kwa ujumla, ili kudumisha usafi wa mazingira yao.
Dadi anafahamisha kuwa elimu ya afya ni jambo zuri sana, hivyo ni wajibu wa jamii kushirikiana pamoja katika kuendeleza jambo hilo.
"Kabla ya kupata elimu hii changamoto nyingi zilikuwepo lakini
tulikuwa tunasaidiana na wizara katika kuzitatua," anasema Dadi.
Nae Mwalimu Salma Tahir Omar kutoka Skuli ya Sekondari Shumba Vyamboni anasema changamoto
kubwa ni ukosefu wa taula za kike (pedi) hivyo wanafunzi kushindwa kuwasaidia wanapopatwa
na hedhi.
Hata hivyo kwa sasa Skuli imeamua kununua taulo hizo (pedi) na kuweka akiba
ili mwanafunzi anapopatwa na tatizo hilo waweze kumsaidia na kuondokana na
usumbufu wa kurudi nyumbani na kukosa masomo.
Mwanafunzi ambae hakutaka jina lake litajwe nasema wamekuwa wakipatiwa ushauri
nasaha kutoka Skuli na hivyo umewasaidia sana na wamekuwa wakihudhuria
madarasani kama kawaida ingawaje kuna changamoto wanazokumbana nazo baadhi ya
wanafunzi ikiwemo kuumwa na tumbo.
Anafahamisha kwa sasa wanafunzi waliowengi wamekuwa wakihudhuria Skuli kama
kawaida, na wala hawajuilikani wako katika kipindi hicho, kwani kunataaluma
mbali mbali wanazopewa na walimu wao.
“ Tumekuwa tukihudhuria masomo yetu bila ya wasi wasi wowote hata tukiwa katika
siku zetu za Hedhi, na wala huwezi kumuelewa mtu kirahisi kuwa yuko na hedhi,”alieleza.
Hapo awali baadhi ya wanafunzi wa kike hususan wale ambao
wameshafikia umri wa baleghe, walikuwa wakikata masomo kila mwezi kutokana na
kuingia katika siku zao(hedhi) iliosababishwa na kukosa elimu juu ya
kujitambuwa na kujihifadhi.
MWISHO
Comments
Post a Comment