NA BAKAR MUSSA, PEMBA::
MARCH 2020
Tanzania, iligundua kesi ya mwanzo ya ugonjwa Corona baada ya dunia kugubikwa na janga kubwa la uwepo wa gonjwa huo, 'UVICO19' ambalo ulianza mwezi disemba 2019 nchini China.
Licha ya Zanzibar kupoteza roho za watu wake kadhaa, lakini pia kwa kiasi fulani, iliathirika kiuchumi, ijapo kwa asilimia ndogo kutokana na watalii kutoingia kwa kasi kama ilivyozoeleka.
Ikumbuke kuwa, ugonjwa huo unaelezwa unasambaa kwa kasi kutokana na kuwepo kwa makaazi ya watu karibu (msongomano) na hivyo kuwepo na hadhari ya kutokukaa karibu na kuvaa Mask (Barkoa).
Kwa vile ugonjwa huo ulitawala dunia nzima, ni wazi kulitokea mtikisiko wa uchumi, ingawa waswahili husema ‘Mwenyeezi Mungu akikupa kilema hukupa na mwendo’.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilipata mkopo wa fedha kutoka Umoja wa Mataifa, baada ya kuonekana nchi nyingi kukumbwa na ukosefu mkubwa rasilimali fedha za kujiletea maendeleo kutokana na kuwepo ugonjwa huo.
Zanzibar ikiwa ni nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nayo ilifaidika kutokana na fedha hizo na kuziekeza katika maeneo mbali mbali.
Sina nia kubwa ya kuelezea
kuhusiana na gonjwa la Covid 19 lilivyoingia, bali ni kuelezea fedha hizo za
Covid 19 zilivyoifaidisha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na watu wake
walivyofaidika kupitia miradi ilioanzishwa na mfuko huo.
Zanzibar, imekuwa na miradi hiyo nilioeleza lakini leo nitagusia ujenzi wa madarasa katika skuli za msingi na Sekondari kisiwani Pemba, ulivyoweza kuondoa msongamano wa wanafunzi madarasani.
Akizungumza na makala hii, Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu na mafunzo ya amali Pemba, Mohamed Nassor Salim, anasema ujenzi wa madarasa ya skuli yaliojengwa, kupitia fedha za ahuweni wa mfuko wa Covid19, utapunguza kwa kiasi kikubwa, japo hautaondosha kabisa tatizo liliopo.
Madarasa hayo licha ya kupunguza wimbi la uwepo wanafunzi wengi madarasani, lakini pia utapunguza masafa kwa wanafunzi kufuata elimu, wimbi la utoro, udhalilishaji.
Wastani kila
darasa la mita 7 hadi 8, watakaa wanafunzi 45 hadi 50, ingawa lakini kwa Pemba
wanakaa 120 wa msingi na Sekondari na maandalizi ni 25 lakini wanakaa 90 hadi 120.
Anasema uwepo wa
wanafunzi wengi madarasani, waalimu hufundisha kwa kutumia mbinu
shirikishi kwa kuuliza masuali na
humfanya atumie mbinu ya muhadhara ya kufundishia ambayo sio njia nzuri.
Anaeleza kuwa ujenzi wa madarasa hayo, mkoa wa kusini Pemba yalijengwa 143 na kaskazini 208 , madarasa ya chini mkoa wa kusini ni 63 na ghorofa 3 na vyumba 8 vya wanafunzi wa mahitaji maalumu .
Na mkoa wa kaskazini 203 ya chini na ghorofa vyumba 21 ambapo katika kisiwa cha Pemba kina wanafunzi zaidi 174,000.
Madarasa ya chini kwa mkoa wa kusini yametumia shilingi bilioni 2.6, wakati yale ya ghorofa tatu kwa mkoa wa kusini, yametumia wastani wa shilingi 4.3, ambapo mkoa wa kaskazini zilitumika shilingi bilioni 3.6 ya chini na ya ghorofa ni shilingi bilioni 1.2 .
Ofisa Mdhamini wa wizara ya elimu na mafunzo ya amali anasema skuli zinazoingia katika mikondo miwili nyingi, zikiwa ni za msingi na mikondo 3 ni Skuli za Mwambe pekee kwa Pemba.
Ingawaje kwa asilimia kubwa tatizo la uwepo
wa wanafunzi wengi madarasani, litaondoka kwa skuli za sekondari.
Anasema kuna tafauti ya saa 1.15
ya masomo wanayoingia wanafunzi wa mkondo mmoja na wanaoingia mikondo 2 na 3,
kwani wanaoingia mkondo mmoja husoma
masaa 7.15 mpaka 30 na mikondo miwili husoma kwa masaa 6, hivyo kunaupotevu wa
masaa ya masomo.
“ Kwa vyovyote kutakuwa na
tofauti ya muda wa masomo baina ya wanafunzi, wanaoingia skuli mkondo mmoja na
mikondo miwili na mitatu lakini uwepo wa madarasa haya ya Uviko 19 utapunguza
tafauti hiyo”, anaeleza.
Nae Msimamizi mkuu wa wa miradi ya maenedeleo ambayo inatekelezwa kupitia fedha za ahuweni ya uviko 19, mkoa wa kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, anasema hatua iliyofikiwa katika ujenzi ni kubwa.
Anaeleza ni faraja iliopo, kwa wananchi wa mkoa wa kaskazini na pemba kwa ujumla kupata madarasa mengi, ambayo yako ya ghorofa na ya chini yote ni juhudi za Dk. Mwinyi kuwawekea mazingira bora ya kusomea watoto wa Zanzibar.
Kwa upande wake Ofisa Elimu na mafunzo ya Amali mkoa wa Kaskazini Pemba maalim Khamis Said Hamad anasema, idai ya wanafunzi wakiwa wengine madarasani, changamoto kadhaa hujitokeza ikiwa ni pamoja na kupoteza ufahamu.
''Ujio wa madarasa haya ya UVICO ndani ya mkoa wangu, sasa utakwenda kuondoa msongamano wa wanafuzi madarasani na kuchechemua ufahamu wa wanafunzi,''anasema.
“ Kwa mfano skuli ya Makangale ambako wanafunzi wanaingia mikondo miwili, ingawa kwenye ujenzi huu wamejengewa vyumba 20 vya madarasa, hii ni wazi kuwa, kuna mwanafunzi wa sekondari atakae atakaeingia mikondo mwili”, anafahamisha.
Anaeleza kuwa ndani ya mkoa huo
kuna Skuli nyingi ambazo zilikuwa na wanafunzi wanaoingia mikondo miwili
litaondoka tatizo hilo kama vile skuli ya Micheweni, Maziwani,Tumbe.
Anasema ziko skuli 43 kati ya hizo ni asilimia 5 zilikuwa zinaingia mkondo mmoja , kwa uwepo madarasa
ya Uviko asilimi 40 ya skuli za sekondari zitakuwa zinaingia mkondo mmoja ,ingawaje kwa
msingi haitokuwa rahisi kuingia mkondo mmoja.
Kwa upande wa Ofisa Elimu wilaya ya Mkoani Mohamed Abdalla Omar anasema, kutokuwepo madarasa ya kutosha, kuna tatizo kwa wanafunzi kutokujifunza kwa ufanisi.
Idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa, imekuwa ikiongezeka kila mwaka na hupelekea kuwa kero kwa mwalimu katika ufundishaji kwani hamudu kufanya wajibu wake ipasavyo.
Kwa mwaka 2021 pekee, wilaya ya Mkoani wanafunzi 3,608 waliandikishwa katika madarasa ya maandalizi, Tutu waliandikishwa 3,846 na skuli za maandalizi za binafsi 439.
Omar Ali Omar ni mwalimu wa msingi katika skuli ya Shengejuu anasema serikali ya awamu ya nane, imejitahidi kujenga madarasa hayo kila skuli.
Alisema kuwepo kwa wingi wa wanafunzi darasani kunakuwa na changamoto kubwa hata wanafunzi, wanakosa kupata ufahamu kama inavyotakiwa.
“Mimi kwa hili niseme Serikali imefanya jambo jema sana, kwani kuwekeza katika elimu ni jambo la msingi sana, sasa ni juhudi za wanafunzi na waalimu kwani mazingira ya kusomea yako vizuri”,alisema.
Nao Wazazi wa wanafunzi Ali
Mohamad Issa wa Wingwi anasema uwepo wa ujenzi wa madarasa mapya kupitia Uviko
19, umeleta faraja kubwa sio kwa Wizara ya Elimu pekee bali hata kwa wazazi.
“ Sisi wazazi tutaondokewa na michango ya kila siku, ambayo tumekuwa tukichangia kwa ujenzi wa madarasa, igawaje ujenzi wa madarasa hayo ya Uviko 19 hayawezi kuondowa tatizo la wingi wa wanafunzi madarasani moja kwa moja”, alieleza.
Anaeleza kila wakati wanafunzi
walikuwa wakidai mchango kwa baadhi ya Skuli, kwa ajili ya kuongeza madarasa
wako waliofanikiwa na wako wasiofanikiwa kutokana na hali za wazazi zilivyo.
Anasema lakini kwa usimamizi wa
Dk. Hussein Mwinyi kupatikana kwa fedha hizo za Uviko 19 kwa sasa hakuna pahala
ambapo hakuna ujenzi wa madarasa mapya hii ni hatuwa kubwa sana kwao.
MWISHO.
Comments
Post a Comment