NA ZUHURA
JUMA, PEMBA::::
NI majira
ya saa 6:00 za mchana nikiwa katika harakati zangu za kazi, nilijikuta naibukia
katika kijiji cha Tumbe Mashariki Wilaya ya Micheweni Pemba.
Muda huo kijua kilikuwa kinawaka mithili ya moto uliomwagiwa
maji kutokana na vuke lililokuwepo.
Wakati macho yangu yakiangaza huku na kule, punde nilimkuta
mama mmoja wa makamo, akiwa amekaa pembeni ya mlango wake wa mbele akishona
makawa.
Kumbe alikuwa ni mama wa miaka 46 aliejulikana kwa jina la
Khadija Sleyum Mtawa anaejishugulisha na ushonaji wa makawa ya nyiti tangu
akiwa mtoto.
Bila kujali alinielezea ushonaji wa makawa ya nyiti kwamba ni
kazi anayoipenda ambayo inampatia angalau pesa ya sabuni.
Uso wake ukionesha tabasamu anasimulia ni kazi aliyoianza
tangu akiwa na miaka 11, wakati huo akiwa darasa la tano mwaka 1985.
Makawa hayo anatengeneza kwa kutumia ukindu mzima
uliopasuliwa, rangi na kamba inayojulikana kwa jina la unu ambayo hupatikana
kwenye kuti la mnazi.
Kilichomsukuma Khadija kushona makawa ni kutokana na hali ya
maisha aliyokuwa nayo katika familia yake na kuona kwamba ipo haja ya
kuwasaidia wazazi baadhi ya majukumu.
“Wazazi wangu walikuwa wanajitahidi kutuhudumia na mdogo
wangu, lakini kuna baadhi ya vitu nikihitaji huwa hawana uwezo navyo”, anasema
Khadija.
Alishona makawa na kuuza, ambapo alipata fedha ya kumsaidia
kutatua shida zake na pia kuisaidia familia yake pale inapokuwa na tatizo.
Makawa anayoshona mama huyo ni tofauti na yale ya ukili, kwani
yana ubaora wa hali ya juu na yanawavutia watu wengi.
Watu wanayapenda sana makawa ya nyiti kutokana na kuwa yanadumu
kwa muda mrefu ukilinganisha na makawa ya ukili, ambapo pia yana muonekano mzuri
pindi unavyoyatazama.
“Nanunua ukindu halafu naupasua, nyengine nazipika kwa rangi, kisha
zile mbale ndio ninazoshonea makawa kwa kutumia kamba ya unu na hayana kazi
kubwa sana ukilinganisha na yale ya ukili”, anaeleza.
Anatengeneza makawa ya rangi mbali mbali pamoja na vipepeyo
kwa kutumia ukindu uliopikwa kwa rangi tofauti.
Anasema, ujuzi wa kutengeneza makawa aliupata kwa rafiki yake
ambae walikuwa jirani na anamshukuru sana kwa kumfundisha, kwani ujuzi haufi utaendelea
kumsaidia.
“Kwa kweli nimefarijika sana kupata ujuzi huu, kwani napata
pesa ya kujikwamua na hali ngumu ya maisha, nawanunulia wanangu nguo za sikukuu,
kila siku nawapa pesa ya kutumia skuli na nawalipia ada ya madrasa”,
anasimulia.
Ingawa pesa anayoipata haikidhi haja lakini hakuna kupata
kudogo, kwani maisha yake ni tofauti kabisa na wanawake wengine katika maeneo
anayoishi.
“Kujituma kunatusaidia kuwa na muonekano mzuri kila wakati,
hivyo nawanasihi wanawake wenzangu tusijipweteke tu, waume watatukimbia”,
anaeleza mama huyo.
Mjasiriamali huyo ananunua ukindu kutoka Mkoani Tanga na rangi
ananunua kisiwani hapa kwa wafanyabiashara ambao huchukua nchini Kenya.
Anaeleza kuwa, kwa sasa imekuwa ghali sana kutokana na nchi
hiyo kukumbwa na ugonjwa wa Corona, kwa sababu wafanyabiashara hawaendi sana.
Mtaji wa mama huyo ni mdogo sana, hali ambayo inasababisha kuzalisha
bidhaa kidogo, ambayo haikidhi mahitaji yake kwa sasa.
“Zamani ilikuwa sina watoto, lakini baada ya kuolewa na kuzaa
majukumu yameongezeka, hivyo pesa ninayoipata ni ndogo sana”, anaeleza.
Mjasiriamali huyo anaeleza, atakapokuwa na fedha za kutosha
atanunua ukindu mwingi kwa jumla na kushona makawa mengi ambayo yatampatia tija.
Anahitaji angalau apatiwe shilingi 500,000 ambazo zitamsaidia
kusafiri kwenda kununua ukindu kwa jumla na anaamini litamsukuma mbele katika kuendeleza
biashara yake.
Kwa upande wa soko anaeleza kuwa, lipo kiasi na zaidi anauza
soko la ndani.
Anaamini kwamba, ikiwa atatengeneza makawa mengi, atayapeleka
hata katika masoko ya utalii kwa sababu ni makawa adimu kupatikana kutoana na
utengenezaji wake.
“Naamini watalii yatawavutia sana makawa haya, kwani ni makawa
ya ubunifu na yanawavutia watu wengi wa ndani ya nchi, kila anaeyaona hushangaa
na kuhitaji atenenezewe”, anasifia.
Watu wengi hununua kwa ajili ya kufunikia chakula, kupamba
ndani ya nyumba, kwa sababu yanapendeza sana na ukiyaona utajiuliza jinsi yalivyoshonwa.
Anafafanua kuwa, kawa moja kubwa anauza shilingi 9,000 na dogo
shilingi 7,000 ambapo lililochorwa mauwa ni shilingi 12,000 kubwa kwa sababu
hupeleka kwa mchoraji shilingi 3,000 kwa kila kawa moja.
Anasikitika sana kwamba hajawahi kuwafundisha watu
utengenezaji wa makawa hayo kutokana na kuwa, wengi wao wanaona ni kazi isiyo
na manufaa kwao.
“Ni kweli hii ni kazi isiyo na kipato kikubwa, lakini unapata
kupunguza shida zako, kila nikiwambia wanawake wenzangu niwafundishe hawataki”,
anasikitika.
Mjasiriamali huyo aliolewa na mume wa kwanza ambae alimuacha
baada ya kukaa muda mrefu bila ya kupata kizazi (watoto).
Ingawa kwa sasa ana watoto saba (7), wakike wanne (4) na
wakiume watatu (3) tangu alipoolewa tena na mume mwengine mwaka 1994.
Ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wawili, akiwa yeye
na mdogo wake wa kiume ambao walizaliwa hapo hapo Tumbe.
Mume wake Khadija aliejukana kwa jina la Hamad Haji anasema,
tangu alipomuoa mke wake anafanya kazi hiyo ingawa kipato ni kidogo sana.
“Nampa mashirikiano sana, lakini tatizo ni mtaji, kwa sababu
malighafi anazotumia kutengeneza makawa hayo zinatoka nje ya kisiwa cha Pemba”,
anaeleza.
Anasema, ikiwa atapata mtaji wa kutosha basi bidhaa yake hiyo
inaweza kumpatia fedha zitakazomsaidia kujikwamua na hali ya maisha.
Tambuu Mwadini Juma mwenye miaka 60 ambae ni mtu wa karibu wa
mjasiriamali huyo anasema, anamkumbuka Khadija tangu akiwa mdogo anatengeneza
makawa hayo na kuuza.
“Ni mzaliwa wa hapa hapa Tumbe na ameolewa hapa, makawa ni
mazuri na watu wanayapenda sana, ni kazi ya ubunifu kwa kweli”, anasifia.
Haji Khamis Haji ambae ni Mratibu
wa Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Pemba anasema, wanaviwezesha vikundi
vya wajasiriamali na mtu mmoja mmoja aliyemo kwenye kikundi kwa kuwapatia
mikopo na mafunzo.
“Ikiwa mjasiriamali hayumo
kwenye kikundi hatumpi mkopo, labda kwa wakulima wa mboga, matunda na wale wanaosafirisha
bidhaa kutokana kwa vile sasa kuna mradi wa mboga mboga ambao unawasaidia”,
anafafanua.
Mratibu huyo anafahamisha kuwa,
kuanzia mwaka 2015 hadi mwaka jana wameshatoa mikopo kwa vikundi na mtu mmoja
mmoja alie kwenye kikundi ipatayo 968 ambapo Wilaya ya Micheweni ni mikopo 181
yenye thamani ya shilingi 152,000,000.
Fat-hiya Mussa Said ambae ni Mratibu wa Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Pemba anasema, kawaida
wanawawezesha wajasiriamali wa vikundi vya shehia ambazo zimefikiwa na mradi
wao wa kuwawezesha wanawake kiuchumi (WEZA).
“Mjasiriamali huyu anatakiwa ajiunge kwenye vikundi vya kuweka
na kukopa, ili apate fedha za mkopo zitakazomsaidia kujikwamua na changamoto
zinazomkabili”, anafahamisha.
Alimtaka mjasiriamali huyo ajifunze zaidi na awe tayari
kujifunza mambo mbali mbali sambamba na kuchangamkia fursa za masoko.
Wajasiriamali wadogo wadogo kisiwani Pemba wamekuwa wakikabiliwa
na changamoto mbali mbali zinazosababisha kuwakwamisha katika shughuli zao,
licha ya kuwa na lengo la kujikwamua.
MWISHO.
Comments
Post a Comment