NA BAKAR MUSSA, PEMBA
Kama ilivyo kawaida kwa samaki, hawezi kuishi bila ya kupata maji, ili yaweze kumsaidia kuishia na ndio mwanamke anavyohitaji kupata mwanamme
ili kuanzisha na kuendeleza familia.
Kwa mujibu wa taarifa ya kidunia,watu bilioni 1.7 wanaishi vijijini duniani kote, huku zaidi ya asilimia 40 ya nguvu kazi katika kilimo ni
wanawake.
Ambao wanatajwa na kuiwakilisha na kuindeleza jamii lakini wanabakia kuwa ndio masikini wakubwa.
Hiyi ni kauli ya Bi Cornelia Richter,Rais wa mfuko wa Kimataifa wa maendeleo ya Kilimo ‘IFAD’ wakati akizungumza na ‘UN news’ miongoni
mwa mikutano ya hali ya wanawake duniani.
“Endapo umasikini ungekuwa na sura basi ingekuwa ya mwanamke wa kijijini, sisi hapa ‘IFAD’ tunajaribu kuwekeza katika uwezo wa
wanawake na sio kuwadhalilisha wanawake”, alisema Bi Cornelia.
Katika mkutano huo, alisisitiza kuwa kuboresha maisha yao ni muhimu ili kutokomeza umasikini, jambo ambalo litahitaji mtazamo tofauti na
hatua mbalimbali kulifanikisha.
Mwanamke kama mama wa familia, amekuwa na majukumu mengi na makubwa ya kila siku ambayo anawajibu wa kuyatekeleza kwa ajili ya familia yake,
iende vizuri na kuhakikisha kila mmoja ndani ya familia amepata haki yake ikiwemo chakula usafi wa nyumba, watoto , baba.
Mwanamke ni kiumbe kilichotukuzwa sana na Mwenyeenzi Mungu,kutokana na umuhimu wake na hili limebainika katika hadithi mbali mbali kama
ifuatavyo;-
Mtume Muhamad (S.A.W) – Rehema na Amani zimshukie – anazidi kuudhihirisha ulimwengu nafasi aliyonayo mwanamke katika mfumo huu
sahihi wa maisha (Uislamu), anatuonyesha uhusiano uliopo baina ya mwanamume na mwanamke katika kauli yake:
"Wanawake ni ndugu baba mmoja, mama mmoja na wanamume, wanayo haki kwa sheria (kufanyiwa na wanamume) kama ile haki iliyo juu yao kuwafanyia
wanamume" Abu Dawoud.
Istilahi ya ndugu baba mmoja, mama mmoja aliyoitumia Bwana Mtume inatoa sura kamili ya usawa baina ya mwanamke na mwanamume.
Mama Fatma bint Said miaka 45,sio jina lake halisi, ni mama wa kijijini mwenye watoto nane 8 na wajukuu wawili, ambae anaishi na mume
wake.
Ambaye mume huyo kwa bahati mzuri, ni mfanyakazi wa Serikali, hivyo huondoka nyumbani kwake mapema na kukimbilia kazini, huku akimuacha
mama huyo akishughulika na majukumu ya familia.
Mama huyo pamoja na majukumu ya usafi wa nyumba na kushughulikia watoto waliyopo nyumbani, lakini bado amekuwa akifanya haraka ya
kukimbilia shambani kwa ajili ya kilimo kwa kila siku ambacho huwasaidia kwa chakula.
Pamoja na kazi nyingi za kila siku anazokabiliana nazo mama huyo wa kijijini, lakini hubakia kuwa maskini kwani baadhi yao kile
wanachozalisha huwa kinamilikiwa na akinababa na kukosa maamuzi ya kukitumia kwa shughuli mbali mbali.
Mwanamke wa kijijini huwa na majumu makubwa kuliko mama wa mjini, kwani tokea asikie sauti ya adhana na jogoo likiwika, muda wa saa 11
alfajiri, ndio gamu, wasi wasi na wahaka huanzia hapo.
Upepo, mvua, kiza, hakiwi kikwazo kwake kuweza kujiamsha muda huo na kuanza kupapasa zana za kilimo kama vile jembe, panga kwa safari ya
kuelekea shambani.
Ingawaje hakuna utafuti mkubwa katika kujinasua na umaskini hasa kwa wanawake wa kijiji baina ya muolewa na mjane (asie na mume), kwani
hamkani za kimaisha wanazoziita za kujinausua na umaskini, miongoni mwao.
Kama hiyo haitoshi huwaamsha wale watoto wenye kuenda skuli na kuwaandalia maji ya kukoga na kipasha tumbo, kikibahatika kuachwa na
mume.
Baada ya hapo mama huyo wa kijijini huanza pirika za kujitayarisha kwenda shambani, hususan msimu wa kilimo huwa hana nafasi ya kupumzika
pengine ifike saa 2:00 kwa kuamuwa kulala.
Kazi hiyo hudumu kwa maisha makubwa hadi pale atakapo maliza nguvu za kufanyakazi kama hizo.
Mwanamke huyo wa kijijini, hajuwi muda wa kuoga wala wa kupumzika itokezee tu lakini hakuna muda anaoutenga maalumu, kwani huwa kwenye
pirika za maisha tu kila kukicha , itokee bahati tu aweze kuamuwa angalau kuoga na kupumzika kwa muda mchache kabla ya kuingia
kitandani.
Hata hivyo pamoja na kazi kubwa ya uzalishaji wa mazao ikiwemo kupanda vipando mbali mbali vya chakula na mazao, mama huyo huishiwa na nguvu
bado akiwa ni maskini.
Bibi Asha Omar miaka 50, ni mama ambae amejaaliwa kuolewa na waume wawili kwa nyakati tofauti, ambapo wa kwanza alifariki na kumuachia
watoto saba (7), mama huyu kabla ya kufariki mume wake alikuwa na shida kubwa na alipofariki ikazidi mara dufu.
Mbali na kusubiri jogoo liwike alfajiri, ili aweze kuelekea shambani kwa ajili ya kilimo chake mwenyewe cha kujipatia riziki ya halali,
lakini pia aliweza kulima hata makataa (mapande) kwa watu wengine ili aweze kupata pesa za kumuendeshea maisha na watoto wake.
“Nitafanya nini ndugu yangu kama sikumlimia mtu akaweza kunipatia pesa nikaendeleza maisha na watoto, wakati sina wa kumtegemea, utadhani
hata mafuta ya taa nitayapata humu ndani,”alisema kwa masikitiko.
Kwa vile mama huyo pengine hana mtu wa kumsaidia kweli na watoto wake ,aliiambia makala hii kuwa umasikini kwao ni jadi hata akitokea mume
akimuoa ,basi hatoweza kumtegemea.
“ Pamoja nakuwa watoto hao wanababa zao wakubwa na wadogo, lakini siwezi kuwategemea kwani na wao wanafamilia zao hivyo hivyo, ila langu
mimi ni jembe ingawaje limeshamitia maradhi”,alisema.
Alieleza pamoja na kuweko matrekta kwenye serikali yanayolimia watu, mama huyo hajawahi kumiliki uwezo wa kutia trekta ndani ya shamba
lake, kwa ajili ya kumlimia ni yeye na jembe lake tu ambalo linamuwezesha angalau kupata chakula cha siku moja.
Alifahamisha kuwa analima shamba karibuni tatu za mpunga kwa kutumia jembe la mkono,lakini mavuno anayopata mfano wake ni kula ya siku
moja, kwani yanayopatikana hayawezi kufikia hata wiki mbili.
Mama huyo pamoja na kupitia maisha magumu ya kuishi kwa umaskini, lakini kwa sasa ameamuwa kujiunga na vikundi vya saccos ( kuweka na
kukopa ), ambacho pengine kinaweza kumuinuwa na kadhia hiyo pale wanapogawana ama kukopa.
Hata hivyo ni wanawake wachache ambao wamekuwa wakijihusisha na hisa ambao wamefanikiwa na kupambana na umaskini kama vile Nasra Sulum
Mohamed wa Kiuyu Kigorofani .
Ingawaje wako wachache pamoja na kujihusisha na saccos za kuweka na kukopa, lakini kile wanachokipata huishia mifukoni mwa akinababa na
pengine kwa ajili ya kuongezea mke wa pili huku akimuacha mama anaeteseka na mvua, jua akiendelea kuishi na umaskini.
Pamoja na kwamba Nassra, kafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuendesha maisha yake kupitia mgongo wa Saccos na sasa kuwa mjasiria mali aliejipatia
jina kubwa Kisiwani Pemba, lakini ni wazi wako kama Nasra wanaohitaji kuonekana wakipiga hatuwa ya kujikwamuwa na umaskini.
Bwana Ali Salim Ali (50) amesema ni kweli mwanamke wa kijijini amekuwa na majukumu mazito katika familia tafauti na mwanamme hususan katika
kipindi cha kilimo kutokana na kuachiwa mzigo mkubwa wa kuihudumia familia kwa mambo mbali mbali.
Alieleza mwanamke amekuwa akifanya kazi kubwa ya kilimo na wala haoni jua wala mvua analo liweka mbele ni suala la kuona familia yake
haipati tabu kwa jambo lolote likiwemo la chakula.
“ Nikupe mfano sasa hivi ni msimu wa kilimo cha mpunga, unapotembea kwenye mashamba mbali mbali unaowakuta ni akinamama pekee ,anaeteseka
na mvua kubwa wakati akipalilia na humuoni mwanamme akiwa anafanya kazi hiyo ni nadra sana,”alisema.
Nae Mohammed Hamad Ali ( 43), alikiri Wanaume wamekuwa wakiachia kazi mzito ya kusimamia familia akinamama ikiwemo naya kilimo cha aina
mbali mbali na wanaume wakijifanya wako na kazi nyingi japo wengine wakiwa hawanakazi inayojuilikana ili kucheza bao.
“ Mwanamke hasa wa kijijini amekuwa hana muda wa kupumzika tokea asubuhi mpaka jioni anakuwa katika harakati za kimaisha hujuwi alie na
mume au asie na mume wala alie na mume mfanyakazi au asie na kazi asilimia kubwa wanakuwa na wakati mgumu,”alieleza.
Alisema akinababa wamekuwa wepesi wa kusahau kuwa akinamama hawakuletwa duniani kuwa ni majembe ya kuwalimia wanaume au
washuhulikiaji wa familia peke yao na akinababa anawajibu wa kumsaidia Mwanamke katika kazi za kila siku , lakini ni kinyume chake baadhi ya
akinababa wanasahau wajibu wao.
“ Sisi akinababa wa kijijini tunaona aibu hata kumsaidia mwanamke kupeleka mtoto Klinik hata kama mama yake anaumwa na inawezekana hata
kuosha watoto wetu hatuwezi kuwaosha jee hiyo hata dini sijuwi kama inaturuhusu tufanye hivyo, lazima tuwasaidie hawa tusiwafanye ni
watumwa wetu,”alieleza.
Kwa upande wa Idara ya Vyama vya Ushirika Zanzibar, imekuwa ikimuandaa mwanamke kushiriki katika kujinasua na umaskini kwa kuwahimiza
kujiunga na vikundi vya ushirika na kwa muda huu ndio wanaongoza katika vikundi vya kuweka na kukopa .
Idara ya Vyama vya ushirika imekuwa ikiwapatia mafunzo mbali mbali ya kujinasua na umaskini akinamama kwa kuwapatia nyenzo mbali mbali za
kujiendesha kupitia Idara ya vyama vya ushirika ikiwemo VICOBA nk.
Aidha vikundi mbali mbali vya akinamama vimekuwa vikipatia mikopo kupitia mifuko ya uwezeshaji wa Wananchi kiuchumi pamoja na mafunzo ya
ujasiriamali.
Kwa upande wa Serikali imekuwa ikitafuta njia mbali mbali za kumnasua mwanamke na umaskini ,ikiwemo kuendeleza juhudi za kuwahamasisha
wanawake kujiendeleza kielimu na kutoa kipaumbele cha elimu kwa watoto wa kike.
Serikali pia imekuwa ikiimarisha uwezo wa mifuko mbali mbali ya kuwawezesha kiuchumi Wanawake na kuwajengea mazingira
yatakayowawezesha kuanzisha Benk ya Wanawake.
Kuimarisha mifuko iliopo ya mikopo ili wanawake wengi zaidi waweze kufaidika kutokana na mifuko hiyo.
Mwanaharakati wa masuala ya akinamama Pemba, Tatu Abdalla Mselem, amesema umaskini kwa mwanamke wa kijijini hauwezi kuondoka kutokana na
mfumo dume uliojengeka kwa baadhi ya Wanaume mbali mbali walioko huko.
Alieleza mwanamke wa kijijini anaweza kubakia hivyo hivyo kkutokana na kujiweka katika mazingira hayo kwani akina baba anabakia kuwa bwana na
huku akimuachia majukumu mazito mwanamke kwa kumfanya ndio mwenye majukumu makubwa kuliko yeye.
Alifahamisha ili mwanamke wa kijijini aweze kujinasua na umaskini lazima mfumo wa kizamani uwe na mabadiliko kuanzia malezi ya watoto na
kujenga mfumo wa kushirikiana kwa kila jambo.
“ Elimu zaidi inahitajika ya kumtowa mwanamke wa kijijini katika dimbwi la umaskini na elimu hiyo isitolewe tu kupitia vyombo vya
habari bali itolewe kwa kuwafikia huko waliko na kuwashirikisha akinababa katika elimu hiyo,”alisema.
Hata hivyo alisema elimu zaidi juu ya kumtowa mwanamke wa kijijini katika umaskini kwa kumtaka ajitowe katika maficho ili ashiriki katika
shuhuli mbali mbali ukiwemo ujasiriamali, uwekaji wa hisa nk, lakini inaonekana bado haijawafikia waliowengi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment