Skip to main content

PPC YAFANYA MKUTANO MKUU MAALUM, MAAZIMIO 10 YA UTPC YARIDHIWA

 



NA HAJI NASSOR, PEMBA:::

MWENYEKITI mstaafu wa Klabu ya waandishi wa habari Pemba ‘PPC’ Said Mohamed Ali, amewakumbusha wanachama kulipa ada zao kwa wakati, kwani ndio uimara na uhakika wa kuwepo kwa PPC.

 

Mwenyekiti huyo aliyasema hayo Disemba 24, 2022 kwenye mkuatano mkuu maalum wa PPC, uliofanyika ukumbi wa Maktaba Chake chake Pemba.

 

Alisema uhai wa ‘PPC’ unategemea mno uhai wa wanachama wanaolipa ada, kwani sio vyema klabu hiyo kuendeshwa kwa michango na miradi ya wafadhili pekee.

 

‘’Wafadhili kama Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania ‘UTPC’, Interenews na hata Baraza la Habari Tanzania ‘MCT’ wanaweza kuja na kuondoka, lakini sisi wanachama ndio wenyewe,’’alishauri.

 


Katika eneo jingine, Mwenyekiti huyo mstafu aliwakumbusha waandishi hao kufanyakazi kwa kufuata maadili na sheria zao, ili wasiwe chanzo cha uvunjifu wa amani.

 



Mapema Mwenyekiti wa sasa wa ‘PPC’ Bakar Mussa Juma, akielezea mwelekeo wa ‘UTPC’ pamoja na yatokanayo na mkutano uliofanyika hivi karibuni, alisema ni kuvitaka vilabu kuwa na miradi endelevu.

 

Alieleza kuwa, jingine ni waandishi wa habari wenywe kujikita katika kufanyakazi, kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari mtandao.

 

‘’Mafunzo baadhi yenu mmeshapata ya usalama wa mitandao, na mengine ‘UTPC’ wameahidi kuwa yanakuja, sasa tushindwe sisi tu kuhamia huko,’’alieleza.

 

Katibu Mkuu wa ‘PPC’ Ali Mbarouk Omar, amewahimiza waandishi hao kulipa ada zao, kama wanavyofanya viongozi wao wa juu.

 

Alieleza kuwa, kwa mpango ujao wa ‘UTPC’ ni kuviwezesha vilabu kwa mujibu wa idadi ya wanachama walio hai, vyenginevyo, wanaweza kukosa ufadhili.

 

Wakichangia masuala mbali mbali wanachama wa ‘PPC’ walisema mafunzo zaidi yanahitajika kwao, ili kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia.

 

Mwanachama Kauthar Is-haka alisema, wakati umefika sasa kwa ‘PPC’ kurejesha tuzo za umahiri wa waandishi wa habari, ili kuongeza juhudi za kufanyakazi.

 

Asha Mussa Omar alipendekeza kuwa, wanachama waliopo wawezeshwe namna ya kuandika miradi, ili iwe rahisi kuwatumia kila wakati.

 

Kuhusu ada mwanachama Jaffar Abdalla alipendekeza kuwa, kuwe na utaratibu wa kukatwa fedha kwa lazima, pale mwanachama atakapopata fursa ya mafunzo.

 

Katika mkutano huo, Msaidizi Katibu wa PPC Mchanga Haroub Shehe akiwasilisha ripoti ya utendaji kazi ya mwaka 2022 ya PPC, alisema ilifanya mambo makubwa, ikiwa ni pomoja na kuendesha miradi.

 

Alisema, walikuwa na mradi wa kutoa elimu ya kifua kikuu, mradi wa amani pamoja na kuwapatia wanachama mafunzo kadhaa ikiwa ni pamoja yale yanayoandaliwa na UTPC.

 

Wakati huo huo Msaidizi huyo Katibu wa ‘PPC’ Mchanga Haroub Shehe aliyasoma maazimio 10 ya mkutano wa ‘UTPC’ uliofanyika Disemba 2022 jijini Dar-es Salaam ikiwa ni pomoja na kuwepo kwa miongozo ya utatuzi wa migogoro.

 

Azimio jengijne ni kila klabu kufuata kwa vitendo, misingi ya usimamizi wa fedha, klabu kuomba kibali cha matumizi ya fedha, zinazozidi asilimia 10, pale wanapotaka kubadilisha matumizi ya fedha.

 


Azimio jengine, ni la klabu kupewa fedha kulingana na mahitaji yake, klabu kupewa fedha kwa mujibu wa idadi ya wanachama wake kwa ajili ya mkutano mkuu maalum.

Wakati huo huo mkutano huo mkuu maalum, uliwapatisha wanachama takriban 10 kuwa wanachama wapya, baada ya kufanya maombi kwa muda wa mwaka mmoja. 

                               Mwisho

 

 

 

Comments