NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
Alidai kuwa, mahakama inamakali mithili ya kiwembe na ina nguvu
hata kusukuma jabali, sasa ni vyema wakazitumia, ili shataka hilo, kuliondosha
na lisimuumize mteja wake.
Aidha wakili Massoud, alida kuwa mteja wake Haroub Bakar Hamad
miaka 22, bado ni kijana mdogo anahitaji kuweko uraiani, ili aendelee na
shughuli zake, na sio kuendelea kuumia akiwa rumande.
Wakili huyo, aliyadai hayo mbele ya hakimu wa mahakama hiyo
Muumini Ali Juma, mara baada ya upande wa mashataka kudai kuwa, shauri hilo
lipo kwa ajili ya kusikilizwa, ingawa hawakupokea mashahidi.
Ndipo Hakimu alipompa nafasi wakili huyo wa utetezi, na kudai
kuwa, sasa imekuwa wimbo wa kila siku kutoka upande wa mashtaka, juu ya suala
la kutopokea mashahidi wa shauri hilo.
‘’Mheshimwa upande wa mashataka wanaichezea sharubu mahakama
yako, na wamekuwa wakifanya wimbo sasa, suala la kutoleta mashahidi, hivyo ni
vyema sheria itumike, ili kuliondoa shauri hili,’’alidai.
Aidha katika hatua nyingine wakili huyo wa utetezi, aliiomba
mahakama hiyo, kuwapa nafasi ya mwisho upande wa mashataka, ili kama hawakuleta
mashahidi na iwe ndio mwisho wa kesi hiyo.
Awali wakili wa serikali Mussa Khamis Ali, alidai kuwa wito wa
mahakama uliwahi kutolewa wiki mbili zilizopita, na kwa upande wa baba mazazi,
aliupokea.
‘’Baba mazazi wa mtoto aliyedai kuingiliwa kinyume na maumbile
wito wa mahakama ameupokea, na kuandika nyuma kuwa, hawezi kufika mahakamani
kutoa ushahidi, kwa vile mtoto wake, hamjui alipo,’’alidai.
Hivyo wakili huyo wa serikali, alimuomba hakimu huyo
kuliahirisha shauri hilo, na kulipangia siku nyingine, na kuomba wito mwengine
wa mahakama utolewe.
Hakimu wa mahakama hiyo Muumini Ali Juma, alisema baada ya
kusikiliza pande zote mbili, ameamua kuliahirisha shauri hilo.
‘’Mtuhumiwa utarudi tena rumande na kufika tena mahakamani hapa Disemba 6 mwaka huu, nanyi upande wa
mashataka mhakikishe siku hiyo mnaleta mashahidi,’’alifafanua.
Hata hivyo, ameuonya upande wa mashataka, ikiwa siku hiyo
hawakuleta mashahidi, uamuzi wa kesi hiyo uko mikononi mwake.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, mtuhumiwa Haroub Bakar
Hamada (22) wa Michenzani wilaya ya Mkoani Pemba, alimuigilia kinyume na
maumbile mtoto wa kike mwenye miaka 12.
Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 133 (a) cha sheria
ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
MWISHO.
Comments
Post a Comment