NA
HAJI NASSOR, UNGUJA:::
MWENYEKITI
wa Bodi ya Wadhamini wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Jaji wa Mahakama kuu
Zanzibar, Mshibe Ali Bakari, amesema lazima jamii na walinzi waamke, kutokana
na wahalifu kutumia mbinu mbadala za kihalifu.
Alisema, hata wale wanaowadhalilisha
wanawake na watoto wamekuwa wakitumia mbinu za ziada, kabla na baada ya kufanya
matendo hayo, ambapo sio rahisi hata wataalamu wa kiulizi kubaini.
Mwenyekiti huyo wa Bodi,
ameyasema hayo ukumbi wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzbar ‘ZLSC’ Kijangwani
mjini Unguja, wakati akifungua kongamano la siku mbili, la kuelekea siku 16 za
kupinga ukatili.
Alisema, lazima jamii na
jeshi la Polisi liongeza nguvu za
zaiada katika utendaji wake wa kazi, ili kukabiliana vyema na uhalifu na udhalilishaji
uliopo.
Alieleza kuwa, urahisi wa
usafiri, wa vyombo vya maringi mawili, boti, ndege na meli zinazoingia Zanzibar,
lazima walinzi na jamii washirkiane, ili kukabiliana na uhalifu.
‘’Kwa mfano uwepo wa boda
boda baadhi yao sio waaminifu, na sasa ukipanda kwa mtu usiyemjua unakuwa na
hofu kama safari yako hujafika,’’alieleza.
Katika hatua nyingine,
Jaji huyo mstaafu alisema, sio fahari
watu wengi kufungwa, kuweko rumande, kesi kuongezeka na matendo, bali fahari ni
kutokuwepo kwake.
‘’Jamii na wahalifu
hawaogopi suala la kufungwa miaka mingi, bali lazima kutafutwe njia mbadala ya
kupunguza matendo hayo, ili kila mmoja aishi kwa amani,’’alieleza.
Aidha Jaji huyo ambae pia
ni Mwenyekiti wa Bodi wa ‘ZLSC’ aliwataka washiriki wa kongamano hilo, kutoa
michango ambayo itasaidia katika mapambano hayo.
Mapema Afisa Mipango wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ Jamila Massoud, alisema kituo kimekuwa karibu mno na jamii, katika kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria bila ya malipo.
‘’Tukiwa ndani ya siku 16
za kupinga ukatili, tumekuwa tukishirikiana katika kuona, jamii inapata uwelewe
wa haki zao kupitia wasaidizi wa sheria,’’alieleza.
Akiwasilisha mada ya
ukatili na udhalilishaji, Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’
tawi la Pemba, Safia Saleh Sultan, alisema hali hiaridhishi katika jamii, hasa
kutokana na udhalilishaji wa watoto, sasa kufanywa na watu wa karibu.
Alisema, kwa mfano katika
utafiti wa kihabari uliofanywa na TAMWA kati ya mwezi Oktoba 2021 hadi Juni
2022, wapo baba wazazi 13, kwa Pemba wanne na tisa Unguja, wamegundulika
kuwabaka watoto wao.
Aidha alisema, utafiti huo
pia umegundua kuwa, wapo waganga wa kienyeji 10 wakiwa wanne Pemba, na Unguja
sita nao waliwabaka wateja wao, huku waalimu wa madrassa 20 nao wamegundulika
kuwadhalilisha wanafunzi wao.
‘’Lakini hata kwa upande
wa Pemba, sasa imegundulika kuwa wastani wa malalamiko 23 ya kuomba talaka,
yamekuwa yakipokelewa mahakama ya kadhi,’’alifafanua.
Aidha mtoa mada huyo,
alisema zipo athari kadhaa za ukatili na udhalilishaji kwa watoto, ikiwa ni
pamoja na kukosa elimu, kupata athari ya kiakili na afya.
Naibu Mrajisi wa mahakama
kuu Zanzibar Salum Hassan Bakar, alisema serikali imeanzisha mahakama maalum ya
kupambana na udhalilishaji, na sasa hali inaridhisha.
‘’Kwa mfano mahakama
maalum ya mkoa wa kusini Pemba, kwa mwaka huum imebakisha kesi tatu na mkoa wa
kaskazini Pemba kesi 10, ambapo haya ni mafanikio makubwa,’’alisema.
Afisa dawati la wanawake
na watoto kutoka jeshi la Polisi makao makuu Zanzibar Rahma Ali Salim, alisema
bado jamii, inahamu ya kuzimaliza kesi hizo nje ya mahakama.
Hakimu wa mahakama maalum
ya kupambana na makosa ya udhalilishaji mkoa wa kusini Pemba, Muumini Ali Juma,
alisema adhabu kubwa haisaidii kupunguza makosa hayo.
Aidha alisema, bado kesi
zinazaowahusu watoto wenye umri wa miaka 14 hadi 17 ndio zenye mashaka
mahakamani, kwa kule kutoa ushahidi wa uongo.
Mwakilishi kutoka Jumuiya
ya wanawake wenye ulemavu Zanzibar JUWAUZA, Salma Saadati, alishauri kuwa ofisi
ya Mtakwimu mkuu iweke takwimu maalum za watu wenye ulemavu waliodhalilishwa.
Alisema, takwimu lazima
ziwe jumuishi, zisiwe jumla jumla kama ilivyo sasa, ambapo hukosa mchanganuo halisi
na kukosekana kuchukuliwa hatua stahiki.
Wakichangia mada kwenye kongamano hilo, washiriki
hao walisema elimu zaidi inahitajika kwa jamii, ili kuona waliowengi wanafika
mahakamani kutoa ushahidi.
Mmoja kati ya washiriki
hao, Kamisha wa msaidizi wa Polisi kutoka ofisi ya Naibu Mkurugenzi wa makosa
ya jinai Zanzbar Haji Abdalla Haji, sasa kasi ielekee kwenye kuzuia matendo
haya, na sio kutumia nguvu katika sheria kali.
‘’Nakishauri Kituo cha
Huduma za Sheria Zanzibar sasa tuanzishe utamaduni wa elimu ya kuzuia matendo
haya na zaidi ilengwe vijijini,’’alishauri.
Kongamano hilo la siku mbili
ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili, ambapo Disemba 10 Kituo
hicho kitaadhimisha siku ya kimataifa ya haki za binadamu.
mwisho
Comments
Post a Comment