USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU TANZANIA
-Wazazi wakiri tamaa, umaskini vyawaelemea kuwatoa watoto wao
HAJI NASSOR, PEMBA::
cell phone: +255656265945
emali: hajipembatoday@gmail.com
‘’Mimi baada ya kuona mtoto wa jirani yangu mwaka 2000 alisafirishwa na mtu tunayemjua, na wangu mimi mwaka 2022 nimemtoa, ingawa
naarifiwa alishauawa akiwa Oman,’’maneno ya mzazi.
Mzazi huyo aliyekataa kuchapishwa
jina lake halisi, anasema atakubali kuhojiwa ikiwa mwandishi atatumia jina la Zawadi,
kwa ajili ya kufanikisha mazungumzo haya baina yake.
Anasema mtoto wake wa kike mwenye miaka
17, baada ya kumaliza masomo, huku akiwa na watoto sita wanaomtegemea, baada ya
baba yao kufariki kwenye meli ya Mv. Spice, hakuwa na wasi wasi, kumtoa kwenda
Oman.
Anasema alimjia mtu ambae hamfamu,
ingawa alimueleza kuwa, alikuwa karibu mno na marehemu mume wake, na hivyo
baada ya kuzoea mno kwake, kisha alimuamini.
Alimtaja kwa jina moja la Hashim,
na ndie aliyemtengenezea pasi ya kusafiria ‘pass port’ baada kumueleza
kuwa hana uwezo wa hata shilingi moja, kwa ajili ya maandalizi ya safri ya
Oman.
Alifikiria mno juu ya safari ya
mtoto wake, ingawa anasema Hashim, alimuonesha picha za vijana wengine ambao
ameshawapeleka nchini huko, wakiendelea na kazi.
‘’Mwandishi usinirikodi wala usinichapishe
jina langu,’’ alikuwa akinisisitiza kila wakati mama huyo, mkaazi wa Tumbe
wilaya ya Micheweni Pemba.
Anasema alivutika mno, na alielezwa
na kijana Hashim kuwa, asimueleza mtu yeyote wa familia yake, maana wanaweza
kuiharibu safari kwa ushirikina.
‘’Hapo mtaa mbele, kuna kijana
nilitaka kumsafirisha, ingawa mama yake baada ya kumueleza kila mtu mtoto huyo,
alipata uendawazimu,’’ni maneo ya ulaghai aliyoelezwa Zawadi na Hashim.
Anasema alitii agizo, hilo na
Januari 29, mwaka 2022 mtoto wake alikabidhiwa pasi ya kusafiria, na alipewa
shilingi 500,000 na Hashim za kufanyabiashara ndogo ndogo.
‘’Wakati anaondoka alielezwa mtoto
wangu, yule Hashim kuwa amuite baba na hata akiulizwa uwanja wa ndege aseme ni
baba yake mzazi,’’anasema mama huyo.
Zawadi anasema siku moja, wakati
mtoto wake anajiandaa kuondoka, aliulizwa ikiwa yule Hashim na baba yake kweli,
na kumjibu hapana.
‘’Ilibidi nimdanganye kuwa ni baba
yake, mdogo na nilisisitizwa hata akiulizwa uwanja wa ndege ajibu kama
hivyo,’’anakiri mama kumdanganya mtoto wake.
BAADA YA KUFIKA OMAN
Mama huyo anasema, mtoto wake ilikuwa
kila Ijumaa anawasiliana nae na mwezi Aprili, alitumiwa shilingi 300, 000 kwa
fedha za Tanzania, kutoka kwa kijana Hashim.
Siku moja, mtoto huyo alimueleza
mama yake, anatamani kurudi kutokana na ugumu wa kazi, ingawa alimtaka awe
mstahamalivu.
Na siku nyingine alimueleza kuwa,
anataka kurudi kwao Pemba Micheweni, akielezea kukosa muda hata wa kumpuzika,
akimtaka kama analipwa, aendelee.
Kuanzia mwezi Julai mwaka huu 2022,
anasema alikuwa akiwasiliana nae kila mwezi mara moja, tena chini ya ulinzi wa
bosi wake wa kazi, tena kwa dakika tatu.
‘’Wasiwasi uliniingia na sasa yule
Hashima hana tena mawasiliano na mimi, na mtoto wangu alikuwa tukiwasiliana
haoneshi furaha, kumbe alianza kupata mateso,’’anasema.
Mama Zawadi anasema, siku moja
mtoto wake, aliiba simu na kumeleza kuwa, sasa analazwa na kijana wa kiarabu,
ambapo usiku humfanya kama mke wake.
‘’Siku moja wakati anambaka
aliambia alimtafuna shavu, na kumueleza kuwa, yeye hakujia kazi hiyo, na asubuhi
yake alipigwa na baba mwenye nyumba,’’anasema.
Kwa mara ya mwisho mwezi Oktoba
2022, alipigiwa simu na tajiri wa mtoto wake, kuwa anaumwa sana na amelazwa
hospitali na baada ya wiki, alielezwa kuwa amefariki.
‘’Sina hakika mwandishi kuwa, mtoto
wangu wa kike ameshauliwa, ameolewa, anatumikishwa, anajiuza au amechinjwa,
mimi nipo nipo tu,’’anaeleza.
Anasema hawezi kwenda popote
kueleza hayo, maana hakumshirikisha mtu yeyote ndani ya familia yake, wala
Polisi kama agizo la dalali lilivyokuwa.
MAJIRANI
Jirani wa mama huyo, anasema wao
wanachofahamu ni kuwa mtoto huyo, anaendelea na masomo chuoni Tanzania bara,
kama alivyowaeleza mwenyewe (mama mtoto).
Kijana Omar Haji Mcha wa Tumbe, anasema mwaka 2019, nae alifuatwa na kijana mwengine, ambae ni dalali, juu ya safari ya Qatar, ingawa baada kuieleza familia alizuiwa.
NINI BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI BINADAMU?
Biashara haramu ya binadamu ni kusafirisha, kuhamisha, kuweka au kupokea, kuhifadhi mtu lengo la kuwanyonya, kuwakandamiza na kunyimwa huru wao.
WAHANGA
Radhia Issa Haji wa Mgogoni Wawi Chake
chake, anasema mateso makubwa aliyapata kuamua kutorudi tena, ni kukosa muda wa
mapunziko.
‘’Hata siku ambazo mmepanga kuwa ni
za mapunziko, unahamishiwa nyumba yako ya kawaida, inapelekwa kwa mama yake au
baba yake tajiri wako,ukifika ni kazi tu,’’anasimulia.
Lililomuumiza zaidi, ni kutakiwa
kuwa huru, kushikwa na kuchezewa chezewa na baba mwenye nyumba, au watoto wake
wa kike.
Haitham Aleyi Manssour wa Wete
Pemba, anasema vijana wasing’anganie sana safari za nje, na hasa eneo ambalo
ukiamua kutaka kurudi ni shida.
Mama mzazi wa mtoto mmoja wa kiume
anaeishi shehia ya Makoongwe wilaya ya Mkoani anasema, kama sio dawa na dua
aliyoitumia, hadi leo ingekuwa mtoto wake hajarudi.
‘’Tulisikia anatumikishwa na
kinyume na kazi yake ya awali, tulimuomba dalali amrejeshe lakini aligoma,
ingawa tulitumia dawa na sasa amerudi yuko Dar-es Salaam,’’anasimulia.
VIONGOZI WA DINI
Sheikh Said Ahmad wa ofisi ya Mufti
anasema, dini inakataza kwaza kufanya hadaa pili kumuuza mtu, maana huo ni
ukatili na udhalilishaji.
Mchungaji Benjamen Kisssanga,
anasema ukiristo unakerwa na kulalamikia mno, tendo la madali kuwafanyiwa
ghilba wazazi au vijana.
WANAHARAKATI
Safia Saleh Sultan wa Kituo cha
Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ anasema, utaratibu wa kazi za nje ya nchi uko
wazi, ni vyema jamii ikaufuata.
‘’Kisheria ni kosa kufanya hadaa au
kuupinda uaminifu, maana katiba zinaeleza binadamu wote ni sawa mbele ya
sheria, hivyo kama kuna mtu anaipinda ni kosa,’’anasema.
Mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya
Pemba Fat-hya Mussa Omar, anasema huo ni aina mwengine wa ukatili na
udhalilishaji wa watoto, ambao unapaswa kukemewa.
‘’Hivi sasa dunia iko katika siku
16 za kupinga ukatili na udhalilishaji, hivyo jamiii iache tamaa na kuingia
katika mitego kama hiyo,’’anasema.
Edwin Mugambila ambae ni Mkurugenzi
Mtendaji wa tasisi ya Tanzania Relief Initiatives ‘TRI’ kila watoto 100 ambao
ni wa biashara haramu ya binadamu 65 ni wasichana na wanawake.
Ambapo anaeleza kuwa, wahanga hao wameajiriwa
na kunyonywa kingono, taarifa za mfano wa jimbo la Marekani kupambana biashara
haramu ya binadamu, inasema kwamba, wale wanaojihusisha na biashara haramu ya
binadamu wanapata kiasi kikubwa cha fedha kama dola bilioni 150 kwa mwaka.
Ambapo hiyo, imeifanya kuwa biashara
haramu ya tatu yenye faida zaidi, ikitanguliwa na dawa za kulevya na uuzaji wa
silaha haramu.
Naibu Balozi wa umoja wa nchi za
Ulaya ‘EU’ Elimo Rossetti akizungumza kwenye mafunzo ya waandishi wa habari na
wanaharakati wa haki za binadamu mjini Zanzibar, alisema Tanzania imekuwa lango
la biashara hiyo.
‘’Sio
kama serikali ya Tanzania haichukii biashara hii haramu, hapana bali kimaumbile
na jinsi ilivyopakana na nchi kadhaa, ndio maana wahanga wanapitishwa na
wakienda kutumikishwa,’’anasema.
Ndio
maana anasema, mafunzo hayo kwa waandishi, yatawazindua wananchi na serikali
kuzidi kupanga mikakati ya kupunguza biashara haramu ya kusafirisha binadamu.
NJIA ZINAZOTUMIKA KUWASAFIRISHA
WAHANGA
Kwa sasa
njia za kielektroniki, kama face book, watsap, email, tovuti huwaunganisha
madalali na vijana na kisha huombwa picha kwa ajili ya kutengenezewa pasi ya
kusafiria.
Wapo
wanaosafirishwa kwa kutumia njia halili za uwanja wa ndege, boti, au gari
kutoka nchi moja kwenda nyingine, na wakati mwengine wakiwa wadogo hufanywa
baba na mtoto.
TAKWIMU ZA NDANI
Ripoti
ya Jeshi la Polisi Tanzania ya mwaka 2020, ilipokea matukio 25 ya watoto
kusafirishwa, kwa njia za kwenda kuuzwa nje za nchi.
Kati ya
watoto hao 25, wa kike walikuwa watano (5) huku wa kiume wakiwa 20, ambapo mkoa
wa kipolisi wa Temeke uliongozwa kwa kuripoti watoto wanane (8) ukifuatiwa na
mkoa wa Manyara watoto wanne (4).
Mikoa ya
Mbye na Simiyu, iliripoti idadi ya watoto watatu (3) kila mkoa, ingawa kwa
mwaka huo wa 2020 mikoa mitano ya Zanzibar, jeshi la Polisi halikuripoti tukio
lolote.
Ingawa masheha sita wa wilaya ya Micheweni waliripoti watoto 12, kwa mwaka huo, kuondoka kinyume na sheria.
''Hawa tumewabaini baada ya waalimu wa skuli kulalamikia kuwa wananafunzi ni wao ni watoro, na tulipowaabili wazazi walieleza kuwa, wako nchini Kenya,''anasema sheha mmoja.
TAKWIMU ZA NJE
Kulingana na Ripoti ya hali ya kimataifa ya
Idara ya Jimbo la Merika juu ya usafirishaji haramu wa binadamu, kuanzia mwezi Juni,
2021 hadi Juni 2022, kulikuwa na kesi 185 zilizoripotiwa za zikihusishwa kuwa
ni za Tanzania.
Ambapo kati
ya kesi hizo, 113 tu ndio ambazo zilichunguzwa na wahalifu 13 pekee ndio
waliotiwa hatiani, ambao wote walilipa faini badala ya kifungo.
JUHUDI ZA SERIKALI NI ZIPI
Mkurugenzi
wa Ustawi wa Jamii Zanzibar Adalla Saleh Omar, anasema moja ya mikakati ya
serikali ni kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama EU, UNFPA ili
kuwajengea uwezo wananchi.
Lakini hata serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tazania imeonyesha msukumo mkubwa wa
kuzuia biashara hiyo, kwani Oktoba 2021, bunge ilifanyia marekebisho sheria ya ‘TIP,
kuandikwa upya ya marekebisho ya na kuingizwa jaribio la kusafirisha kuwa ni
kosa tofauti na zamani.
Juhudi nyingine
ni serikali kuanzisha nyumba tatu salama, kwa ajili ya waathirika, moja ikiwa Zanzibar,
moja ya Dar es salaam na nyingine Dodoma.
Hata
hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba Juma Saadi, anasema lazima
wazazi waamke, na kuwatilia shaka watu wanaowaendea wakitaka watoto.
Kamishna
wa Uhamiaji Zanzibar Hassan Ali Hassan, amenukuliwa akisema, lazima jamii
iamke na kufuata sheria za usafiri na usafirishaji.
‘’Sisi uhamiaji tunampa mtu pasi ya kusafiria, kwa mujibu wa maelezo yake au kama ni mtoto msimamizi wake, sasa dalali akidanganya huo ni kosa ikibainika,’’anasema.
Moja ya athari ya biashara haramu ya usafirishaji binadamu kama ilivyotajwa na Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahaya, ni vifo visivyotarajiwa kwa wahanga
Mama ambae mtoto wake amesharudi Misri hivi karibuni, anasema athari kubwa ni vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
Muhanga wa biashara hiyo, mwene miaka 22, anasema maslahi duni na kazi nzito, ndio jambo ambalo linajitokeza.
NINI KIFANYIKE
Afisa Mfawidhi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Pemba Suleiman Salim Ahmad anasema, elimu ya tahadhari kwa wazazi na vijana, ndio suluhisho.
Kijana Omar Haji Omar ambe mdogo wake ni muhanga wa biashara hiyo, anapendekeza sheria kwa wahalifu wa biashara hiyo, iondoe ulipaji wa fani, bali iwe ni kifungo.
Mratibu wa Jumuiya ya wasioona Pemba 'ZANAB' Suleiman Mansour Suleiman, anasema ziwekwe sheria kali kwa wazazi watakabainika kuwasafirisha watoto wao kwa kushirikiana na madalali.
Mwisho
Comments
Post a Comment