NA HAJI
NASSOR, PEMBA
KITUO cha
Huduma za Sheria Zanzibar, ZLSC kimewashauri wananchi wa shehia ya Wingwi Njuguni
wilaya ya Micheweni Pemba, kikitumia kituo hicho wanapokuwa na migogoro mbali
mbali, ili kupata sulhu kwa njia ya amani na haki.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Kituo hicho Pemba, Safia
Saleh Sultan, wakati akizungumza na wananchi hao, kwenye mkutano wa wazi wa
kutoa elimu ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala za amani na haki,
uliotanguliwa na igizo.
Alisema, ZLSC imekuwa ikibuni njia kila siku, kuhakikisha
wananchi wanajengewe uwezo wa kujua sheria na kanuni, na kisha weweze kutatua migogoro kwa njia ya
amani, hasa kwa kesi za madai.
Alieleza kuwa, migogoro ya kesi za madai kama vile ya ardhi,
ndoa, matunzo ya watoto, madeni baina yao ni vyema wakavitumia vikao vya
familia, kuyamaliza.
‘’Kesi kama hizi mnapokimbilia mahakamani, kuna athari kadhaa
moja wapo ni kupoteza muda, fedha na kuchelewa kupatikana sulhu, ambayo itakuwa
endelevu,’’alifafanua.
Akizungumzia mradi utatuzi wa migogoro kwa njia ya mbadala za
amani na haki, wanaouendesha kwa mwezi mmoja, chini ya the foundation for civil
society, alisema wanatajia kuona wananchi, wanatumia vikao kutatua migogoro ya.
Kwa upande wake Wakili wa watoto wanaokinzana na sheria kutoka
kituo hicho kisiwani Pemba, Siti Habib Mohamed, alisema njia ya utatuzi wa migogoro
kwa njia ya vikao vya familia, inafaa zaidi.
Alieleza kuwa, huwajenga wanajamii kuendelea kuelewana, kutowekeana
visasi pamoja kutokurejea tena kwa mgogoro uliotatuliwa kwa njia mbadala za
amani.
Katika hatua nyingine Wakili huyo, amewakumbusha wananchi hao
wa Wingwi Njuguni, kuwatumia wasaidizi wa sheria, wanapokumbana na changamoto
za kisheria.
‘’Kila jimbo na sasa karibu kila shehia wapo wasaidizi wa
sheria, ambapo moja ya majukumu yao ni kutoa elimu, ushauri na msaada wa
kisheria bila ya malipo, sasa hao watumieni,’’alishauri.
Mapema Afisa Ufuatiliaji na tathmini kutoka ‘ZLSC’ Zanzibar Khamis
Harouon Hamad, aliwataka wanananchi na hasa wanawake, kufuatilia haki zao kwa
upana.
‘’Wanawake mnapokumbwa na changamoto za kisheria msikate tamaa
mapema, fuatilieni hatua kwa hatua, na bahati nzuri sisi ZLSC, ni moja ya jukumu
letu kuwasaidia tena bure,’’alieleza.
Akifungua mkutano huo sheha wa shehia ya Wingwi Njuguni Ali
Hamad Said, alikipongeza Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ kwa uamuzi
wake, wa kuwapa elimu hiyo.
Alieleza kuwa, zipo shehia kadhaa wilaya ya Micheweni, ingawa
Njuguni, imekuwa na bahati, na kuwaomba kufika mara kwa mara kutoa elimu kama hiyo.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, walisema suala
la kutunza amani ni jambo moja kubwa, kwani inapochafuka, kuirejesha kwake,
huwa vigumu.
Hamad Ali Suleyum, alisema amani ni tunda muhimu na ndio
msingi na chachu ya kufikia maendeleo ya kweli, kwenye taifa lolote ulimwenguni.
Nae Mwaliche Haji aliwataka wanawake wenzake, kuwa na subra
wakati wanapokumbana na changamoto kama za migogoro ya ndoa.
‘’Suala la kufanya sulhu kwa njia ya amani na haki ndio chachu
ya kuendeleza ndoa na familia kwa ujumla, na kwa hakika igizo tuliloliona kama
tukilifuata hakuna sababu ya kuzuka migogoro,’’alisema.
Nae kiongozi wa dini sheikh Mohamed Ali Rubea, alisema kwa
sasa, njia wanazotumia kijijini hapo kutatua migogoro, ni vikao vya kamati ya
mskiti na vile vya familia.
‘’Wakati mwengine, ili kuzinusuru ndoa, huwataka mmoja kati ya
wanandoa, kupuuza ama kujisahaulisha unapotokezea mgogoro, na njia hii hufanikiwa
mno tena kwa amani,’’alieleza.
Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ kwa sasa
kinaendesha mradi wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala za amani na haki, unaofadhiliwa
na the foundation for civil society.
Mwisho
Comments
Post a Comment