NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WADAU wa habari kisiwani Pemba wamesema, kuwepo kwa baadhi ya vifungu vya sheria visivyo rafiki kwa wanahabari vinasababisha kunyima uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Wakizungumza wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya wadau juu ya maboresho ya vifungu vinavyominya uhuru wa habari, uliofanyika TAMWA Pemba, wadau hao walisema, kuna haja ya kuwekwa sheria ambazo zitawasaidia waandishi wa habari kufanya kazi zao bila vikwazo.
Walisema kuwa, habari ni muhimu sana na ndio chanzo cha maendeleo katika nchi, hivyo ni vyema vifungu vya sheria vilivyo na mapungufu vifanyiwe maboresho na visivyofaa viondoshwe kwa maslahi ya wanahabari na jamii kwa ujumla.
"Kwa kweli baadhi ya vifungu vyetu vya sheria havipo huru kwa wanahabari kwa sababu upande mmoja wamepewa uhuru lakini upande wa pili unapokonywa, kwa hiyo sio rafiki vinahitaji kurekebishwa", walisema wadau hao.
Said Rashid Hassan kutoka kituo cha Huduma za Sheria Pemba alipendekeza kuwepo kifungu kitakachomlinda mwandishi wa habari, ili wafanye kazi zao kwa uhuru.
"Katika sheria hii sijaona sehemu ambayo inamlinda mwandishi wa habari bali nimeona kwamba atakapofanya makosa achukuliwe hatua na ndio maana hawapo huru katika kufanya kazi zao, wanashindwa hata kuibua madudu ndani ya jamii", alisema.
Kwa upande wake Ali Massoud Kombo kutoka radio Jamii Micheweni alisema sheria ya Mtandao ya mwaka 2015 kinampa Mamlaka Waziri kukifungia chombo cha habari, hivyo ikiwa ana utashi wake binafsi au ameamka vibaya anaweza kukifungia chombo bila sababu ya msingi.
"Vijana tumeambiwa tujiajiri wenyewe lakini kutokana na fedha ya usajili iliyowekwa tunashidwa, Sheria inapaswa kurekebishwa ili kupunguza kuwango cha fedha za malipo na usajili" alisema.
Nae mwandishi wa habari wa mtandaono wa UGA TV Esau Kalukubila alisema, kuna kipengele kinampa mamlaka Rais kuunda Bodi bila kuangalia Mjumbe wa bodi hiyo atakuwa na sifa gani, hali ambayo inaweza kusababisha vikwazo katika tasnia ya habari.
"Hivi vifungu vilivyowapa Mamlaka makubwa Waziri, Afisa Polisi na Rais vinahitaji viboreshwe, kwani vinaminya uhuru wa habari, wajumbe wa bodi wanatakiwa kuomba wenye sifa wafanye usaili na sio kuteuliwa", alisema.
Akiwasilisha vifungu hivyo Mjumbe wa Bodi kutoka TAMWA Zanzibar Shifaa Said Hassan alisema kuwa, kila mtu ni mdau wa habari hivyo ikiwa sheria hizo zitabaki kuwa kandamizi na wao zitawakwaza kwa namna moja ama nyengine.
"Nyinyi ndio mnaotaka habari, ndio ambao mnataka kupaza sauti zenu kutokana na changamoto zinazowakwaza, kwa hiyo ikiwa hamukutoa mapendekezo yenu na nyinyi sheria hizi zitawabana tu", alisema muwasilishaji huyo.
Alieleza kuwa, baadhi ya vifungu hivyo sio tu vinanyima uhuru wa vyombo vya habari lakini pia vinanyima uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, hivyo vinahitaji maboresho ili wananchi wapaze sauti zao.
Nae Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMWA Mohamed Khatib alifahamisha kuwa, kuna baadhi ya vifungu vya sheria ya habari sio rafiki kwa wanahabari, hivyo wadau wanapaswa kuchangia ili kupata mawazo yao yatakayosaidia katika maboresho.
"Tunataka tupate sheria bora ya habari, itakayompa uhuru mwandishi wa habari kufanya kazi zake vizuri, hivyo tutakiwa tufanye ushawishi na utetezi kuhakikisha tunafanikiwa katika hili", alisema Afisa huyo.
Mkutano huo wa kujadili na kukusanya maoni ya wadau juu ya marekebisho ya sheria ya habari ina lengo la kupata sheria bora na huru kwa vyombo vya habari nchini.
MWISHO.
Comments
Post a Comment