NA HAJI NASSOR, PEMBA
‘KABLA ya kuongezeka kwa wavuvi na wachuuzi hapa
soko la samaki Mkoani, nilikuwa mauzo yangu ya uji na maandazi ni
shilingi 35,000 kwa siku, lakini sasa yamezidi mara mbili,’’anasema Aisha Hemed
Khalifa.
Anasema, kwanza hakujua nini sababu ya kuongezeka kwa
wavuvi na wachuuzi kwenye soko hilo, na alijikuta akiishiwa na biashara yake
kabla ya saa 5:00 asubuhi muda aliouzoea tokea zamani.
Kwa kwaida, alishazoea anapoanza biashara yake hiyo, humaliza
kati ya saa 5:00 hadi 5:30, ingawa kuanzia mwezi Januari mwaka huu hali
imebadilika.
Biashara yake hiyo aliyoianza miaka mitano sasa, anasema
ilikuwa ya kusua sua, kutokana na kuwa na idadi ndogo ya wavuvi na wachuuzi
(wateja) kwenye soko hilo.
Awali aliacha biashara ya duka la vyakula, na kujiingiza
kwenye uuzaji wa uji na maandazi, sokoni hapo Mkoani, ili kuongeza pato lake.
Akiwa kwenye soko hilo anasema biashara ilikuwa ya
kudoro dora kiasi, ingawa pato lake lilikuwa tofauti, ikilinganishwa na
biashara ya duka aliyokuwa nayo.
“Biashara hii ya uji na maandazi makavu kwangu, inalipa
zaidi kuliko ile ya duka, maana kwanza hapa huwa naifanya kulingana na hali ya
wavuvi na wachuuzi wanapokuja na sio kila wakati,’’anasema.
Mjasiriamali huyo aliyeachika miaka mitatu sasa akiwa
anawahudumia watoto sita, kwa kwaida ikifika saa 5:30 mchana huwa ameshamaliza
biashara na kurudi nyumbani kuendelea na shughuli za kilimo.
SERA YA UCHUMI WA BULUU ULIVYOKUZA BIASHARA
Anasema, kuanzia mwezi Januari mwaka huu 2022, sasa
biashara yake imekuwa ikipanda siku hadi siku, akisema sera ya Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, imeongeza idadi ya
wavuvi na wachuuzi.
Anasema, sio wavuvi lakini hata vijana wameamua kufunga
susu nyuma ya baiskeli, kuamua kuchuuza samaki, wakiamini kuwa sekta hiyo, sasa
imepata mkombozi.
“Sina takwimu halisi lakini sasa wavuvi wapya ninaowajua
mimi tu wanafika 20, sambamba na wawachuuzi 30 wapya waliongezeka, wakifurahia
uchumi wa buluu,’’anasema.
Mjasiriamali huyo anasema ahadi ya Dk. Mwinyi ya kuitumia
bahari kwa ajili ya kukuza pato la wananchi, kwake limeanza hata kabla ya kuvua
rasilimali yoyote baharini.
Sera ya uchumi wa buluu anaifahamu kuwa, ni kuinua pato
la serikali na hata la mtu mmoja mmoja, likisababishwa na uwepo wa bahari.
“Hata mimi sasa kuongeza pato langu la biashara kutoka
kilo nne za zamani za unga wa mtama hadi sasa kufikia kilo sita sio jambo
dogo,’’anaeleza.
Anasema hata kwenye maandazi, alikuwa kabla ya ujio wa
sera ya uchumi wa buluu, akitumia unga wa nganu kilo mbili kwa ajili ya
maandazi, lakini sas analazimika kutumia kilo nne.
“Mimi amaandazi yangu sio kwa ajili ya wateja wa uji tu,
lakini hata wengine wanaokuja sokoni, lakini ukweli kuanzia mwezi Januari hadi
Machi mwaka huu mauzo yangu yamepaa,’’anasema.
Huyu ni mmoja tu, lakini wapo wapishi wa uji na maandazi
na wengine chai wanaouza kwenye madiko (masoko ya samaki) 22 walielezea kupata
manufaa.
Halima Omar Haji, aliyepo soko la samaki Wete, anasema
sera ya uchumi wa buluu, kwake umeshapanda chati, baada ya kujikuta akiongeza
mauzo ya biashara zake.
“Mimi nauza maandazi ya mafuta, ya kupambia na chai
lakini sasa nimeshahama mauzo ya shilingi 35,000 kwa siku na sasa nahesabu
kwenye shilingi 50,000 kwa siku,’’anasema.
Nilipotaka kujua sababu za kuongeza mauzo, akajikuwa kuwa
anachokishuhudia ni kuongeza kwa wavuvi hata wale ambao walishatangaaza
kustaafu.
Sababu nyingine ni kuongeza kwa wachuuzi vijana, jambo
ambalo wapo waliopata mshangao na walipoulizwa wamesema wamejenga matumaini kwa
ahadi ya rais Dk. Mwinyi.
Hata mjasiriamali wa juisi, vileja, uji na chai aliyepo
bandari ya Tumbe wilaya ya Micheweni Tumu Haidari, anasema ameanza biashara
hiyo kwa miaka sita sasa.
Kwa miaka yote hiyo, anasema hakuwahi kushuhudia mauzo
ya shilingi 65, 000 kwa siku, ambapo hayo ameyashuhudia ndani ya mwaka huu.
“Mimi ilikuwa biadhaa zangu zote nikishauza najikuta nna
shilingi 40,000 tu, lakini sasa dhana ya chumi wa buluu na kuongeza kwa wavuvi
na wachuuzi, kwangu ni neema,’’anasema.
Hivyo hivyo, nae muuza mihogo ya kukaanga, chai na
samaki soko la samaki Micheweni, Mwache Haji Hija anasema kwa sikukuu hii
ijayo, anahakika ya watoto wake kuwanunua nguo kwa uhakika.
Anasema awali alikuwa akiifanya biashara hiyo kama eneo
lake la mapunziko tu, lakini anataka kutanua mafya kwa sasa na kujenga kibanda
cha kudumu.
“Lazima nimpongeze rais wangu wa Zanzibar Dk. Hussein
Ali Mwinyi, kwa kuamua kuinua kipato chetu kwa mtazamo wa bahari, hii kwangu
ndio yajayo ni neema tupu,’’anasema.
Mjasiriamali huyo anasema, kwa vile amekuwa akiingia kwa
zamu na mwenzake sokoni hapo, ndio hasa pato lake huwa la uhakika zaidi.
Anasema, kwa miaka iliyopita kwa vile hakukua na idadi
kubwa ya wachuuzi wala wavuvi na walaji, inaweza ikapita siku tatu bila ya
kushuka sokoni.
MALENGO YA WAJASIRIAMALI HAO NI YEPI?
Wanasema, sasa wanajipanga kwenda Idara ya Uwezeshaji,
ili kuomba mikopo, kwa ajili ya kuendeleza biashara zao na ikiwezekana waajiri
wenzao.
Halima Juma Khamis wa aliyepo sokoni Wesha Chake chake,
anasema aliwahi kuchukua mkopo wa shilingi 200,000 mwaka 2013, ingawa
ulimshinda kurejesha.
“Kwa hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuimarisha uvuvi na wengine wanaotegemea
rasilimali za bahari, sasa najiamini kuchukua mkopo hadi shilingi
500,000,’’anasema.
Nae Halima Omar Haji, anaiomba Idara ya Uwezeshaji
kupunguza masharti, ili sasa na wao waingie kwenye sekta ya mikopo, kama
walivyo wenzao,’’anasema
WAVUVI NA WACHUUZI WANASEMAJE
Msaidizi mkuu wa diko la Wesha Chake chake Mohamed Haji,
anakiri kuongezeka kwa wavuvi kwenye diko hilo, ambao baadhi yao walishataka
kustaafu.
Anaema, sio wavuvi tu lakini hata kuna ongezeko kubwa la
wachuuzi, na wengi wao kutoka nje ya mji wa Chakechake.
“Hivi sasa wapo wachuzui wanaotumia gari ndogo aina ya ‘carry’
kutoka miji ya Mkoani na Wete wakifuata samaki hapa, hivyo hawa wengi wao baada
ya kufika hupata vinywaji,’’anafafanua.
Kwake anasema, dhana ya uchumi wa buluu ambao hata ndani
ya soko hilo matunda yake yameshaonekana, ndio miongoni mwa sababu za
kuongezeka kwao.
Mkuu wa wilaya ya Mkoani Khatib Juma Mjaja, anasema azma
ya serikali, sasa kuwa ndio mkombozi wa kuinua kipato cha taifa na hata mtu
mmoja mmoja.
Mvuvi Haji Kheir Haji wa Mwambe mwenye ngalawa jina la
‘joka pevu’ anakiri kuwa, ongezeko la wavuvi ni manufaa kwa wafanyabiashara
hasa walioko kwenye madiko.
Pandu Mjanaheri Ussi ambae ni mchuuzi mpya, anasema
kilichomvuta kufanya shughuli hiyo, ni kutokana na kauli ya rais wa sasa wa
Zanzibar, wa kuiimarisha sekta ya uvuvi.
“Ni kweli, nimeona kundi la vijana wenzagu wakiwa
wamefunga masusu na kuchuuza, lakini tukifika kwenye diko, kwanza hupata
kifungua mdogo kwa wale mama zetu,’’anasema.
AHADI YA DK.
MWINYI KUINUA PATO KWA UCHUMI W A BULUU
Wakati akinadi sera za chama chake cha Mapinduzi CCM
kwenye kampeni, kuelekea chaguzi mkuu, aliwaahidi wananchi kuinua pato kupitia
bahari.
Akisema kuwa, bado bahari ya Zanzibar haijaguswa kiuvuvi,
na pindi akipata ridhaa, atakahakikisha anaongeza pato la taifa na la mtu mmoja
mmoja kupitia shughuli zilizoko baharini.
Uchumi unaotokana na rasilimali za bahari kama vile
samaki, chaza, majongoo na mwani (uchumi wa buluu) utaweza kuongeza pato la taifa.
Dk. Mwinyi aliwaambia wananchi wa Zanzibar kuwa, hali
hiyo inaweza kuongeza makusanyo la mapato ya ndani kutoka shilingi bilioni 428.
511 kwa mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 748.9
Lakini dhana ya uchumi wa buluu, ikitumika vilivyo
inaweza kupunguza utegemezi wa bajeti na kufikia asilimia 5.7 na kuvuuka lengo
lililoanishwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, na kufikia asilimia 7
hapo mwakani.
Dk. Mwinyi anaamini kuwa, kwa vile uchumi wa buluu
hauwalengi, wavuvi, wachuuzi, wakulima wa mwani, majongoo, wavuvi wa mishipi,
nyavu na madema pekee, anaona hata wanaofanya shughuli za juu watanufaika.
Hapa, alilenga sekta binafasi ambapo serikali inaazimia
kushuka kwa riba ya mikopo, kutoka wastani wa asilimia 18 ya mwaka 2015 hadi
asilimia 14 ya mwaka 2020.
Jambo moja ambapo wavuvi na wengine wanaotegemea bahari
wanatarajia kulipata kama alivyoahidi Dk. Mwinyi wakati wa kampeni, ni
kukamilisha utayarishaji wa sera mpya ya uvuvi na kufanya mapitio ya sheria ya
uvuvi nambari 7 ya mwaka 2010.
Kwenye Ilani hiyo ya CCM, ambayo imeahidi pia kuongeza
uzalishaji wa samaki, aina ya Jodari katika bahari kuu na ufugaji maalum wa
kutumia vizimba ‘cage farming’ kutoka tani 36,728 hadi
tani 44, 450.
Kubwa zaidi, ambalo nalo litafanywa ni kujenga
miundombinu kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa kampuni ya uvuvi ya Zanzibar
‘ZAFICO’ ikiwemo vyumba baridi vya kuhifadhia samaki.
Hapa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Uvuvi Zanzibar
‘ZAFICO’ Zahoro Kassim, anasema alichokiahidi Dk. Mwinyi sio ndoto bali
yanaukweli, na hasa kwa vile hata ununuzi wa boti za uvuvi kwa ajili ya bahari
kuu zinakuja.
Matumaini pia kwa wananchi na hasa wavuvi na wachuuzi wa
samaki ni pale, Dk. Mwinyi alipowaahidi wizara husika ya Uchumi wa Buluu,
kuzalisha na kusambaaza vifaranga milioni 10 vya samaki, kaa na majongoo kila
mwaka.
Haya sasa yakifanyika kwa pamoja, wale mama mtilie ambao
wanaendesha biashara zao kando kando ya madiko na masoko ya samaki, wanaweza
kuongeza pato lao mara dufu.
Mwisho
Comments
Post a Comment