NA HAJI NASSOR, PEMBA::
email: hajipembatoday@gmail.com
TAASISI ya Foundation for Civil Society ‘FCS’ ya
Tanzania bara, imesema itaendelea kufanyakazi kwa karibu na Kituo cha Huduma za
Sheria Zanzibar ‘ZLSC’, ili kuhakikisha jamii inajengewa uwezo, wa kutatua
migogoro kwa njia mbadala za amani na haki.
Hayo yalieleza na Afiss programu
kutoka tasisi hiyo Eveline Mchau, wakati akiwasalimia wananchi wa Kibubunzi
shehia ya Shumba Mihogoni, wilaya ya Micheweni, kwenye mkutano wa wazi wa kutoa
elimu ya utatuzi wa migogoro, kwanjia mbadala.
Alisema ‘ZLSC’ imekuwa ikifanya
vyema kwenye kutoa elimu, ushauri na msaada wa kisheria kwa wananchi bila ya malipo,
jambo ambalo wao limewavutia.
Alieleza kuwa, kinachofanywa na ‘ZLSC’
cha kuwaelekeza wananachi namna bora ya utatuzi wa migogoro, hasa kwa kesi za
madai, ni jambo jema, na tasisi yao inapendezewa mno.
‘’Wananchi, wakati umefika
kutozitumia sana mahakama hasa kwa migogoro ya madai, na badala yake tuitumie
elimu tunayopewa na wenzetu, kama hawa ‘ZLSC’ ambao tunafanya nao kazi,’’alishauri.
Mapema baadhi ya wananchi wa kijiji
hicho cha Kibubunzi shehia ya Shumba Mihogoni, walisema utaratibu wa ‘ZLSC’
kuwafuata wananchi, uwe endelevu ili kupata uwelewa zaidi.
Mwananchi Ali Abdalla Ameir, alisema
mpango huo wa kufika kijijini kwao, ni vyema na wananchi wengine kufikiwa na
kufaidika na elimu hiyo.
‘’Elimu ya utatuzi wa migogoro kwa
njia mbadala za amani na haki ni nzuri, lakini sasa ‘ZLSC’ isiishie kwetu na
vijiji vyengine mfike, ili ienee,’’alipendekeza.
Nao wananchi Khalfan Khamis na Hussein
Faki, walisema changamoto mbali mbali zitajitokeza, pindi migogoro ya kesi za
madai zitapelekewa mahakamani.
Akifungua mkutano huo, sheha wa shehia hiyo Salim Said Salim, alisema nafasi hiyo ni adhimu kwao, na aliwataka wananchi kuitumia, kwa kuuliza maswali.
‘’Kwa niaba ya wananchi wa kijiji
hichi cha Kibubunzi, niwapongeze watendaji wa Kituo cha Huduma za Sheria
Zanzibar ‘ZLSC’ na wafadhili wenu ‘FCS’ kwa hatua ya kutufika,’’alieleza.
Akieleza namna ya utatuzi wa
migogoro kwa njia mbadala za amani na haki, Mratibu wa ‘ZLSC’ tawi la Pemba
Safia Saleh Sultan, alisema njia moja ni kuwatumia viongozi, dini na wazee
kutatua migogoro hiyo.
Njia nyingine alisema, ni vikao vya
familia, wasaidizi wa sheria na hata kuwatumia watu maarufu wanapokuwa na
migogoro yenye mfumo wa madai.
Wakili wa watoto wanaokinzana na
sheria kutoka ‘ZLSC’ tawi la Pemba Siti Habib Mohamed, alisema ni kosa
kuzifanyia sulhu kesi za jinai, kama vile ubakaji, ulawiti, wizi na kuua.
‘’Kesi ambazo jamii inapaswa
kuzikalia kitako na kutafuta sulhu ni zile za madai kama madeni, migogoro ya
ardhi, ndoa na matunzo ya watoto na nyingine zinazofanana na hizo,’’alifafanua.
Aidha wakili huyo, alisema kwa kesi
za madai wananchi wanapozitumia mahakama, hukumbana na changamoto kadhaa kama vile
gharama, kupoteza muda na wakati mwengine kuwekeana visasi baada ya hukumu.
Kwa upande wake Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka ‘ZLSC’
Zanzibar Khamis Haroun Hamad, aliwataka wanananchi kushirikiana katika utatuzi
wa kesi za madai, zinapotokezea katika maeneo yao.
Kituo cha Huduma za Sheria
Zanzibar ‘ZLSC’ kwa sasa kinaendesha mradi wa utatuzi wa migogoro kwa njia
mbadala za amani na haki, unaofadhiliwa na the foundation for civil society kwa
muda wa mwezi mmoja.
Mwisho
Comments
Post a Comment