NA HAJI
NASSOR, PEMBA
JESHI la
Polisi Mkoa wa kusini Pemba, linaendelea kumtafuta, Khamis Ali Khamis ‘Diri’ wa
kijiji cha Ukunda shehia ya Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba, aliedaiwa kumpa
ujauzito mwanafunzi wa skuli ya Kengeja wilayani humo.
Jeshi hilo limesema, mtuhumiwa huyo aende atakako na ajifiche
kwenye msitu mkubwa kiasia kigani, lakini mwisho wa siku, atatiwa mikononi na
kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria, kujibu tuhuma hizo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamada wa Polisi
mkoani humo Richard Tadei Mchomvu, alisema baada ya kutokea tukio hilo, mwaka juzi,
alituma askari wake kumtafuta kisiwani Unguja, alikokimbilia bila ya mafanikio.
Alisema kwa vile mtuhumiwa huyo alijua kuwa ameshafanya jinai,
kwa kumpa ujauzito mwanafunzi huyo miaka 16, aliamua kukimbia, ingawa kwa sasa
wanashirikiana kwa karibu mno na Jeshi la Polisi la mikoa yote ya Unguja, kwa
ajili ya kumtafua.
Alieleza kuwa, kwa sasa mitego imeshawekwa kila kona, na
taarifa za mtuhumiwa huyo zimeshasambaa, ili kuhakikisha anakamtwa.
“Taarifa za tukio la kijana ‘Diri’ kumpa ujauzito mtoto huyo tunazo,
na awali tulituma askari Unguja kwenda kumtafuta, ingawa hatukufanikiwa,”alieleza.
Akizungumza hatua nyengine iliokwisha chukuliwa na Jeshi hilo
la Polisi, alifahamisha kuwa, ni pamoja na kufungua jalada la kesi la ubakaji la
kumpa ujauzito mwanafunzi huyo.
Awali wazazi wa mwanafunzi huyo, walisema baada ya kutokea kwa
tukio hilo mwaka juzi, mtoto wao walidhani anaumwa na ndipo aliposafirishwa hadi
Unguja, kwa ajili ya matibabu zaidi.
Mama mzazi huyo alisema, baada ya kufikishwa Unguja na
kufanyiwa vipimo, iligundulika kuwa ana ujauzito wa miezi sita, ingawa yeye kwa
hatua za awali hakuelezwa kwa vile mume wake alikuwa mgonjwa.
“Mimi waliniambia tu kwamba anauma, na sasa ameshapata
ahuweni, ingawa baadae nilianza kusikia kwa ajirani na kisha ndio nikapewa
taarifa rasmi,”alieleza.
Mtoto huyo ambae mwaka jana alifanya mtihani wa taifa wa
darasa la sita, alisema mtuhumiwa alimuendea usiku ndani nyumba yao, na kabla
ya kufanya tendo hilo, alimtaka asitowe taarifa kwa mama yake.
“Baada ya kufika chumbani wakati taa nimeizima, alivua nguo
zake na kuniweka goti kifuani na kuniziba mdogo na alinitaka nisije mueleza
mama, na nikifanya hivyo atanijeruhi,”alieleza mtoto huyo.
Kwa sasa tayari mtoto huyo ambae mwaka huu alitarajiwa
kuendelea na masomo yake ya darasa la tisa, ameshajifungua, na anasema kama
akiruhusika baadae ataendelea na masomo yake ya sekondari.
Majirani wa mtoto huyo, walisema familia yao imekuwa ikikumbwa
na mitihani ya kubakwa, maana hata dada yake kabla ya kuolewa na mume huyo
aliembaka yeye, nae alibakwa.
Kwa upande wake Afisa wa ustawi wa Jamii wilaya ya Mkoani
Aisha, alisema taarifa hizo wanazo ingawa, bado hawajalifuatilia kujua nini
kinaendelea.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 11, kinaeleza
kuwa, binadamu wote huzaliwa wakiwa huru, na wote sawa, wanastahiki heshima ya
kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
Azimio la ulimwengu juu ya haki za binadamu toleo maalum la
miaka 60, kifungu cha 7, kinaweka wazi kuwa, mbele ya sheria watu wote ni sawa,
na wanastahiki haki sawa za kulindwa.
Sheria mpya ya Adhabu no 6, ya mwaka 2018 ya Zanzibar, kwenye
kifungu chake cha 109, kimetamka kuwa, mtu yeyote ataketiwa hatiani kwa kosa la
ubakaji, atatumikia kifungo cha maisha, ingawa katika mazingira mengine ya
ubakaji, adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30.
Sheria ya Mtoto ya Zanzibar nambari 6 ya mwaka 2011
imetamka wazi juu ya jukumu la wazazi, walezi au mwengine anayekaa na mtoto
kuhusu kumtunza na kumlinda na janga lolote lile likiwemo ubakaji na ulawiti.
Sheria
ya elimu ya Zanzibar ya mwaka 1982 kifungu cha 20 (1) kinaelezea jukumu la
wazazi au walezi kuhakikisha watoto wanasoma na kumaliza elimu ya lazima.
Lakini
sheria ya kuwalinda wari na watoto wa mzazi mmoja, ya mwaka 2005, baada ya
marekebisho, imeweka wazi iwapo, mwanafunzi atapata mimba, baada ya kujifungua
anaweza kurejea masomoni.
Utafiti wa kitaifa uliofanywa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka
2009, juu ya sababu za udhalilishaji, uligundua, watoto sita wa kike, na wa
kiume kila tisa (9) wameshafanyiwa udhalilishaji kwa kila watoto 20.
Aidha utafiti ukagundua kuwa, watoto wa kike 62 na wakiume 71 walikuwa
wamefanyiwa udhalilishaji wa kingono kabla ya kufikia miaka 18.
Mwisho
Comments
Post a Comment