Skip to main content

TUME YA MIPANGO YAWANOA MAAFISA UFUATILIAJI NA TATHMINI

 

 


NA MOZA SHAABAN, PEMBA@@@@

Maafisa ufuatiliaji na tathmini wa wizara mbali mbali  Pemba wameshiriki katika mafunzo ya  kujengewa uwezo juu ya ufuatiliaji na tathmini za miradi, ili kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo   katika ukumbi wa makonyo Wawi chake chake Pemba  mgeni rasmi kwa niaba ya  Kaimu  Katibu mtendaji  Tume ya mipango Zanzibar, Kamishna idara ya Uchumi Ameir Haji Sheha alisema, mafunzo hayo ni muhimu kwa maafisa hao katika utekelezaji wa majukumu yao ya kikazi.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia kujenga utamaduni wa kufuatilia na kutathmini ili kupata takwimu sahihi za utekelezaji miradi na shughuli za maendeleo , ambazo mara nyingi hutumika katika utaarishaji wa mpango wa maendeleo ya Zanzibar.

Alisema ufuatiliaji na tathmini husaidia watekelezaji wa miradi kujua mwelekeo wa utekelezaji  wa kazi zao, ili kuhakikisha utimilifu wa malengo ya mda mrefu waliojiwekea kulingana na muda sahihi.

" Ufuatiliaji wa miradi na tathmini husaidia kujua mwelekeo wa utekelezaji wa kazi kwa  kuhakikisha malengo ya mda mrefu yaliowekwa yanafikiwa kulingana na muda husika, ndio maana tumeandaa mafunzo haya, " alieleza.



Aidha aliwapongeza watendaji wa tume ya mipango kwa kuandaa mafunzo hayo kutokana na umuhimu wake katika kuwaongezea uwezo maafisa hao ili watimize majukumu yao kwa ufaninisi zaidi.

Nae  Afisa mdhamini tume ya mipango Pemba Khamis Issa Mohamed  aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutumia taaluma watakayo ipata katika utekelezaji kazi zao ili  kuendana na kasi ya utendaji kazi wa rais katika kuleta maendeleo kwa jamii.

Alisema maafisa ufuatiliaji na tathmini wanakazi ya kupanga na kufuatilia miradi mbali mbali ya kimaendeleo, hivyo mafunzo hayo ni hatua muhimu katika utekelezaji majukumu yao.

"Nyinyi ndio wenye kazi ya kupanga na kufuatilia miradi ya maendeleo, hivyo mafunzo haya ni hatia muhimu katika utekelezaji majukumu yenu ya kikazi", alieleza.

 Kwa upande wake kamishna wa tume ya  mipango Zuhura Mohamed Abdallah alisema, mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea ujuzi na uwelewa maafisa hao, ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utendaji wao wa kazi,

Aliongeza kua  kwa mara ya kwanza maafisa hao watapatiwa mafunzo  ufuatiliaji katika  miradi ya kiuhandisi ambayo ni mara ya kwanza  kufanyika kwa Zanzibar.




Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Nachia Hamad Suleiman kutoka wizara ya fedha na mipango Pemba alisema, mafunzo hayo yatawasaidia kujua ufuatiliaji wa miradi kwa usahihi ili kupata matokeo chanya kama inavyokusudiwa.

Mafunzo hayo yalioandaliwa na Tume ya mipango  yameanza leo tarehe 1Disemba  yamehusisha maafisa ufuatiliaji na tathmini  kutoka wizara 18 za serikali na yanatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku nne.

                                                             MWISHO


Comments