NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
SIKU ya kimataifa ya watu wenye ulemavu duniani, ilianza
kuadhimishwa mwaka 1992 na Umoja wa Mataifa.
Tangu kuanzishwa kwa siku hii, kumekuwa na mafanikio mbalimbali
duniani, ambapo kwa Zanzibar pekee, ni kuwepo wa sheria nambari 8 ya mwaka 2022.
Malengo ya siku hii, ni kuongeza uelewa juu ya mambo yanayohusu watu
wenye ulemavu, pamoja na kutoa elimu juu ya haki na fursa zao.
Taarifa za mitandao zinafafanua kuwa, siku hii hutazamiwa kuongeza
uelewa kwa watu wenye ulemavu, katika masuala kadhaa, likiwemo la uchumi wao.
Malengo endelevu ya dunia Sustainable
Development Goals ‘SDGs’ ni mkusanyiko wa malengo 17 yalopangiliwa kwa
faida ya watu wote ulimwenguni, wakiwemo wao.
Maana, malengo haya yalianzishwa mwaka
2015 na Baraza kuu la umoja wa mataifa, yalikiwa na malengo ya
kufikiwa mwaka 2030, kama sehemu za ajenda za mwaka huo.
Kwani inafahamika kuwa, miongoni mwa
malengo hayo endelevu ni pamoja na kutokomeza umaskini, kukomesha njaa, afya njema
na ustawi, elimu bora, usawa wa kijinsia na maji salama.
Wakati leo dunia ikiadhimisha siku ya
kimataifa ya watu wenye ulemavu, watu wenye ulemavu Pemba, wanasema ipo hatua
iliyochukuliwa dhidi yao.
MATAMU DHIDI YAO
Mashavu Juma Mabrouk ambae ni Mratibu
wa Baraza la taifa la watu wenye ulemavu Zanzibar ofisi ya Pemba, anasema
kuwepo kwa sheria mpya ni jambo jema kwao.
‘’Leo tukiadhimisha siku ya kimataifa
ya watu wenye ulemavu, lazima tujivunie walau kuwa na sheria hiyo mpya na sera
yake,’’anasema.
Suleiman Manour kutoka Jumuiya ya wasioona
ZANAB, anasema awakiadhimisha siku ya watu wenye ulemavu, yapo mazuri kwao.
‘’Hata kuwa na wizara inayoshughulikia
watu wenye ulemavu ni jambo jema, maana zamani ilikuwa sisi tukihangaika huku na
kule tu,’’anakumbuka.
Hidaya Mjaka Ali kutoka Umoja wa watu
wenye ulenmavu ‘UWZ’, anasema zipo asasi zaidi 10 za watu wenye ulemavu na hukutana
na kujadiliana.
‘’Kwa mfano tulianza na ‘UWZ’ sasa
zipo kama ZANAB, ZAPDD, CHAVIZA, JUWALAZA zote hizi na nyingine ni ishara kwamba
tunatambulika kisheria,’’anaeleza.
Katija Mbarouk mjumbe wa baraza la
watu wenye ulemavu wilaya ya Wete Pemba, anasema sasa wanashirikishwa, kwenye
mambo kadhaa ya kiinchi kama uongozi.
‘’Kwa mfano hivi karibuni tulikuwa na
Tume za uchaguzi ile ya Zanzibar ‘ZEC’ na ile ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ‘INEC’, katika ushauri wa kuelekea uchaguzi mkuu,’’anakumbuka.
Omar Haji Nassib wa Mchanga mdogo,
anakiri kuwa wakati wakiadhimisha siku ya watu wenye ulemavu, kwa kiasi kikubwa,
heshima yao ipo kwa jamii.
‘’Kwa mfano hata ukitaka kupanda meli,
ndege au gari watu wanakupata nafasi na wakati mwingine unapewa heshima kubwa,’’alieleza.
HAYA YALIKUJAJE?
Aliyekuwa Waziri katika ofisi ya
Makamu wa Kwanza Harusi Said Suleiman, anasema serikali inaendelea kuthmani kwa
vitendo, haki za watu wenye ulemavu.
‘’Kwa mfano hata ujio wa sheria mpya
ya watu wenye ulemavu nambari 8 ya mwaka 2022, ni ishara kwa serikali kuwathamini,’’anasema.
Afisa Mdhamini wa Afisi hiyo Pemba
Ahmed Abubakar, anasema eneo jingine ambalo serikali, inathamini watu wenye
ulemavu kwa vitendo, ni kuanzishwa kwa baraza la taifa la watu wenye ulemavu.
Anakumbuka kuwa, kwenye hiyo sheria
yao mpya, vifungu vinalazimishwa kuanzishwa kwa baraza hilo kwa ajali yao, na
sasa lipo na ni msaada mkubwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, akilihutubia baraza la wawakilishi, aliahidi
kuendelea kuzitekeleza haki za watu wenye ulemavu.
MITANDAO INARIPOTI NINI?
Kwa mujibu taarifa kutoka kwa Tume ya Haki za
Binaadamu na Utawala Bora ‘THBUB’ wakati wa maadhimisho ya siku kama hii, mwaka
2021, ilisisitiza haja ya kuzitunza haki za kundi hilo.
Kwenye taarifa
yake, ikisisitiza kuwa, siku hii ni matokeo ya Azimio nambari 47/3, la mwaka 1992
la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lililopitisha Disemba 3 ya kila mwaka, kuwa
ni siku ya kimtifa.
Juni 13, mwaka 2021, BBC Swahili iliripoti, kuwa
watu wenye ulemavu na hasa wale wa ngozi, hupitia changamoto kadhaa, katika maisha
yao, na kukosa furaha.
Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, kinaendesha mradi maalum, ambao unawajengea uwezo waandishi wa habari, ili kuyaibua wanayofanywa na wawtu wenye ulemavu.
Mkurugenzi wao Dk. Mzuri Issa Ali, anasema vyombo vya habari, havikuwa na weledi wa kuandika taarifa za watu wenye ulemavu, jambo lililowaficha na kuzidi kupata msongo wa mawazo.
''Loe tukiwa ndani ya siku ya kimataifa kwa ajili yao, walau unaona mazuri yanayofanywa na watu wenye ulemavu katika vyombo vya habari,''anasema.
Mwisho




Comments
Post a Comment