DISEMBA 3 ya kila mwaka dunia
huadhimisha siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu.
Siku hii ilianza
kuadhimishwa mwaka 1992 na umoja wa mataifa, lengo likiwa ni kuongeza uwelewa
juu ya mambo yanayo husu watu wenye ulemavu.
Pia inalenga kutoa elimu kwao na kwa jamii juu ya haki zao na kuongeza ufahamu juu ya
uungwaji mkono kwa ajili ya utu, heshima na ustawi wao.
Historia inaonyesha watu
wenye ulemavu walikua na wakati mgumu zaidi kwa miaka iliopita.
Kwakile kinachooeleza kua
walikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kutelekezwa na kunyimwa haki zao za msingi ikiwemo ya kuishi.
Hivyo uwepo wa siku hii
ni kuthamini na kuenzi utu na heshima ya watu wenye ulemavu ambavyo vilitiwa
kapuni kwa miaka mengi.
Hivyo Disemba 3 ni wito
wa kukumbatia utofauti wa kimaumbile tulio nao, kuvunja vizuizi na kuhakikisha
mustakbali uliojumuishi zaidi kwa watu wote.
Ikizingatiwa kwamba
takribani watu bilioni 1.3 duniani kote wana ulemavu mkubwa, sawa na asilimia
16 ya watu duniani.
Wakati dunia ikiwa na
takwimu hizo, Tanzania katika sensa yake ya watu na makazi ya mwaka 2022, inafafanua asilimia 11.4 ya watu wote Zanzibar
wana ulemavu.
Huku ikieleza idadi hiyo imeongezeka kutoka
asilimia 5.4 ilivyokuwa katika sensa ya mwaka 2012.
Takwimu hii na ile ya
dunia zinasisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto zinazowakabili watu
wenye ulemavu na kuhakikisha ulemavu wao hauwi sababu ya kuvunjwa utu na
heshima zao.
Izingatiwe kwamba watu
wenye ulemavu wana haki sawa na watu wengine, kama zilivyo kaziwa na sera kanuni na sheria za watu wenye ulemavu.
Hivyo siku ya watu wenye
ulemavu ulimwenguni kipekee zaidi imekuja kuwapa fursa ya kupaza sauti pale
wanapoona kutokuwepo kwa usawa katika jamii au uvunjwaji wa sheria zinazo wasimamia
katika upiganiaji haki zao.
Kauli mbiu ya mwaka huu
inasema “Kua na jamii jumuishi inayo wathamini na kuwapa fursa sawa watu wenye
ulemavu katika nyanja zote za maendeleo’.
Yenye maana kuwa kila
kitu katika jamii kiwazingatie watu
wenye ulemavu, ili kuwapa thamani na fursa kushiriki katika nyanja za kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na elimu, afya, siasa na mengineyo.
Kaulimbiu hii inaungana
na Sera, Sheria na kanuni mbali mbali zinazo simamia haki za watu wenye ulemavu,
ikiwemo ya ujumuishi wao katika nyanja za kimaendeleo.
Mfano mkataba wa umoja wa kimataifa wa haki za watu
wenye ulemavu (2006) ibara ya 19 (b) na (c) inaeleza kuhusu ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu.
Ibara hiyo inataka watu wenye ulemavu wawe wanapata huduma za
aina mbalimbali nyumbani na katika jamii na misaada binafsi ambayo ni ya lazima katika
kuwawezesha kujumuika kwenye jamii.
“Huduma za kijamii na
miundombinu kwa ajili ya umma, inapatikane kwa watu wenye ulemavu kwa misingi
ya usawa na inayoendana na mahitaji yao”, pia imeeleza sehemu ya mkataba huo.
Aidha sheria ya watu
wenye ulemavu ya Zanzibar ya mwaka 2022 katika kifungu chake cha 32 (d)
kinaeleza taratibu za utoaji na uaptikanaji huduma ziwe zinazingatia mahitaji maalumu ya watu wenye
ulemavu.
Hii yote ni kuhakikisha
jamii jumuishi, jamoja na kuwathamini watu wenye ulemavu kwa kuwapa fursa sawa
katika nyanja zote za maendeleo.
WATU
WENYE ULEMAVU
Rehema Juma Makame wa
Kukuu Pemba ni mwenye ulemavu wa uoni anasema, jamii jumuishi ni daraja la
kupita katika kuhakikisha upatikanaji fursa sawa kwa kila mmoja.
Anasema kama kaulimbiu
inavyooeleza, kua na jamii jumuishi inayowathamini watu wenye ulemavu,
utekelezaji wake utarahisisha usawa na upatikanaji haki zao za msingi ambayo
ndio kiu yao kubwa.
Hidaya Mjaka Ali ni
mwenye ulemavu wa viungo anasema,
kaulimbiu hii itasaidia kujenga uwelewa kwa jamii na nchi kwa ujumla
kwamba, watu wenye ulemavu wanapaswa kujumuishwa katika safari zote za
maendeleo.
Anaeleza jamii jumuishi itatoa
fursa na haki sawa kwa watu wenye ulemavu, ambayo ni hatua muhimu katika
kufikia maendeleo.
“Jamii jumuishi ni fursa
ya upatikanaji wa haki sawa na ni hatua muhimu ya kufikia maendeleo, kwani bila
kuwepo kwa ujumuishi ni ngumu kulifikia fursa zilizopo”, alieleza.
Anasema jamii jumuishi inamaanisha
kuwa watu wenye ulemavu wana fursa sawa za kupata elimu, ajira, huduma za afya
na mengineyo.
Amina Khamis Khalfan wa
Mtambile Pemba ni mwenye ulemavu wa ualbino anasema, kuwa na jamii jumuishi ni
fursa kwao kujiimarisha kiuchumi, kwani kutawawezesha kufanya shughuli zao za
kiuchumi bila vizuizi.
Anasema ikiwa miundombinu
ya masoko, usafiri, elimu afya na mengineyo yatakua jumuishi kwa watu wote,
kutawapa fursa ya kuendesha shughuli zao za kimaendeleo bila vizuizi na
maendeleo yatapatikana.
JAMII
Adam Mbarouk Juma wa
Mbuguani Mkoani Pemba anasema, kunaumuhimu wa kua na jamii jumuishi na
inayowathamini watu wenye ulemavu, kwani itawapa fursa ya kushiriki kikamilifu
katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo.
Sada Mohamed Amour wa
Mjimbini Pemba anasema, jamii inapaswa kuondoa vikwazo kwa watu wenye ulemavu vya kuzifikia fursa mbali mbali kama wanavyo
zifikia wengine.
“Watu nwenye ulemavu huchangia
pakubwa katika kila nyanja ya maisha iwe ni sanaa, sayansi, michezo au
teknolojia, ni vizuri waondolewe vikwazo na wathaminiwe ili washiriki kwa
uhuru”, alieleza Sada.
JUMUIYA
ZA WATU WENYE ULAVU
Maryam Mohamed Salum
Afisa watu wenye ulemavu Pemba kutoka “UWZ” anasema, kila kitu kinachohusu jamii
lazima kihusishe ujumuishi wa watu wenye ulemavu hapo ndipo jamii jumuishi
ipatikane.
Anasema hii ni
kuhakikisha elimu, Afya, miundombinu, kazi na kila sehemu inayohusu haki ya msingi ya
binaadamu inakidhi mahitaji ya kila mtu,
hapo ndipo fursa sawa katika maendeleo itapatikana.
Mashavu Juma Mabrouk
Mratibu baraza la watu wenye ulemavu Pemba anasema, siku ya watu wenye ulemavu
ulimwenguni ni fursa ya kuitambulisha jamii
haki za watu wenye ulemavu,
ambazo ndio msingi imara wa kupatikana jamii jumuishi.
Anasema kila mmoja katika
jamii kuanzia familia hadi serikali kuu, inajukumu la kuhakikisha tunakua na
jamii jumuishi, ili kujenga thamani na kutoa fursa sawa kwa watu wenye ulemavu
katika maendeleo.
HITIMISHO
Siku ya watu wenye
ulemavu duniani 2025 ni ukumbusho kwamba ujumuishaji sio tu tukio la siku moja
lakini ni ahadi ya maisha ya kila siku.
Hivyo ni vyema kwa watu
binafsi, mashirika, na serikali kuvunja vizuizi na kujenga jamii ambapo kila
mtu bila kujali uwezo wa maisha anaweza kustawi.
Katika kufikia hilo ni
vizuri kuboresha ufikiaji katika maeneo ya umma, kuajiri watu wenye ulemavu
katika majukumu ya maana, na kuelimisha jamii kuhusu thamani ya ushirikishwaji
wa watu hao katika maendeleo.
Kwa vile siku ya
Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu huangazia changamoto na fursa katika kuunda
ulimwengu unaojumuisha zaidi, ni vizuri kuzifanyia kazi changamoto hizo ili
kuhakikisha usawa katika jamii.
MWISHO
Comments
Post a Comment