KAMATI ya maadili na taaluma ya
kijiji cha Kidutani shehia ya Chumbageni Wilaya ya Mkoani Pemba, imepitisha
kanuni 19 zitakazowaongoza katika kusimamia malezi ya watoto na vijana.
Akizungumza kijijini hapo katika kikao cha kupitisha kanuni hizo
kilichoandaliwa na kamati hiyo Mwakilishi wa sheha ambae pia ni Mratibu wa kamati ya maadili ya shehia hiyo
Abrahman Mohamed Khamis alisema, Ofisi ya sheha ipo tayari kushirikiana na
wanakijiji katika kusimamia kanuni hizo.
Alisema ni vyema wananchi kutoa
ushirikiano wa kutosha kwa kamati hiyo, ili lengo liweze kufanikiwa, huku
akiwataka wanakamati hao iwapo patakua na kikwazo chochote katika utekelezaji
majukumu yao, kupeleka changamoto zao kwa sheha.
"Ofisi ya sheha ipo tayari
kushirikiana na nyinyi katika hili, naomba na wananchi mutoe ushirikiano wa
kutosha ili kufanikisha jambo hili, na iwapo patatokezea kikwazo katika utendaji kazi wenu musisite kuripoti
kwa sheha", alieleza.
Nae Mjumbe wa Sheha wa Shehia ya
Chumbageni Juma Shaaban Jabir alisema, hatua iliyochukuliwa na wanakikijiji hao, ni nzuri kwani itasaidia kutatua changamoto za kimaadili katika shehia yao,
huku akisisitiza kamati hiyo kua endelevu.
Aliongeza kua huenda kijiji hicho
kikawa mfano nzuri na wakuigwa ndani ya shehia hiyo na hata shehia nyingine,
huku akitoa wito kwa kamati hiyo kuweka pembeni itikadi zao za kisiasa na
badala yake wafanye kazi kwa maslahi ya kijiji hicho.
Akizungumza katika kikao hicho Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la polisi Abdallah
Mohamed Abdallah alisema, iwapo mtu yeyote atapingana na kanuni hizo kwa
makusudi, ni vyema kamati kumripoti kwa kwao, kwa lengo la kuchukuliwa
hatua zaidi, huku akiitaka jamii kutoa mashirikiano ya kutosha kwa jeshi hilo.
Nae Mwenyekiti wa kamati hiyo Machano
Ali Makame, alipongeza ushirikiano wanaoupata kutoka kwa jamii na uongozi wa
shehia, ambapo alifafanua kua tokea kuanza kamati hiyo wanafunzi 25 wameanza
kusoma, baada ya kupewa vitabu vya aina tofauti vikiwemo vya kumjua Muumba wao
kutoka katika kamati hiyo.
Akisoma kanuni 19 zilizopitishwa
katika kikao hicho Mshauri Eelekezi wa kamati hiyo Haji Nassor Mohamed
alisema, kanuni hizo ni pamoja na marufuku ya kutembea usiku zaidi ya saa nne
kwa asiekua na dharura, marufuku ya ukataji nywele usio zingatia maadili pamoja
na uvaaji nguo za mbano.
Huku kanuni nyengine zikiwa ni
marufuku ya uvutaji sigara, unywaji
pombe na madawa ya kulevya, upigaji ngoma ovyo pamoja na kanuni
inayotaka futarisho kwa wanakijiji kila mwaka mara moja kwa lengo la
kuwaunganisha.
Kamati ya maadili na taatuma ya
kijiji cha Kidutani shehia ya Chumbageni, ilioanzishwa mienzi
minne iliopita, ikiwa na wajumbe 12 wakiwemo wanaume na wanawake, na
imepitisha kanuni 19 itakazozisimamia katika utendaji kazi wake, ambazo
zitasainiwa na sheha wa shehia hiyo, Kamanda wa polisi wa Wilaya ya Mkoani
pamoja na Mkuu wa wilaya hiyo.
MWISHO




Comments
Post a Comment