IMEANDIKWA
NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
MWAKA
2025 ni mwaka ambao wanawake wengi wamejitupa jimboni kuwania nafasi mbali
mbali za uongozi.
Hii
inaoneshea dhahir kwamba, sasa jamii imepata uwelewa juu ya masuala ya uongozi
kwa wanawake na ndio maana wakachaguliwa kwenye kura za maoni, ili kusudi
waingie katika mchakato wa kugombea.
Imeonekana
kuwa, wanawake wapo imara na waaminifu katika kutekeleza yale wanayoyaahidi kwa
wananchi kwa lengo la kuipatia maendeleo jamii iliyowazunguka.
Tayari
wamefikia hatua ya kuingia jimboni kugombea, lililobaki ni kusubiri siku ya
uchaguzi ili wachaguliwe kuingia kwenye vyombo vya maamuzi, kwa ajili ya kuwasilisha
kero za wananchi na kupatiwa ufumbuzi unaofaa.
Mwanaidi
Hamad Rashid mwenye umri wa miaka 39 mkaazi wa Kitambuu Wilaya ya Wete, ni
mmoja kati ya wanawake waliojitupa majimboni kuwania nafasi za uongozi kwa
lengo la kuleta mafanikio kwenye maeneo yake.
Ni
mgombea uwakilishi Jimbo la Kojani kupitia chama cha Wakulima (AFP) ambae ni
mara ya kwanza kugombea na kufanikiwa kuingia katika mchakato wa uchaguzi.
Mgombea
huyo hakuwa na ndoto za kuwa kiongozi hapo awali, ingawa alipoona sasa jamii
inamkubali mwanamke kuwa kiongozi, ndipo alipoona kuna haja kugombea ili aweze
kutatua kero zilizomo kwenye Jimbo lao.
"Kuna
changamoto mbali mbali zinazotaka ufumbuzi, hasa zinazotukwanza wanawake na
watoto wetu, lakini sikuwa na njia ya kuzisemea, ndio nikaona ili nipate sehemu
ya kuziwasilisha ni vyema nigombee uwakilishi," anaeleza.
Mwanaidi
ana imani kwamba wananchi wa Jimbo lake watamchagua kwenye kuwawakilisha katika
chombo cha kutoa maamuzi, kwani wameona wameshapata mtetezi.
Anasema,
wananchi wa Jimbo lake wanampa pongezi nyingi kwa hatua aliyoichukua kwani
ameoneshwa uthubutu wa kutaka kuwaletea maendeleo katika Jimbo lao.
"Wananchi
sasa wanataka maendeleo, hivyo wanachagua mtu ambae atawaletea maendeleo, ndio
maana nikaamua kuingia kwenye mchakato ili niwatimizie lengo lao"
anafahamisha.
Mgombea
huyo anaeleza, anafanya mikutano ya kampeni sambamba na kupiga kampeni za
nyumba kwa nyumba ili kuhakikisha anapigiwa kura ya ndio ifikapo Oktoba 29
mwaka huu.
Anasema,
atakapofanikiwa kushika nafasi hiyo ya uwakilishi, atazidisha ushirikiano na
wananchi kwani itakuwa ameshabeba dhamana nzito, hivyo atahakikisha lile lengo
la kutatua kero za jamii na kuleta maendeleo linakamilika kwa haraka.
Atazitumia
pesa za mfuko wa Jimbo katika kuboresha na kuleta mabadiliko ya kimaendeleo
kwenye Jimbo lao, ili wananchi wanufaike na fedha hizo ambazo zinaletwa
makusudi kwa ajili ya kuendesha shughuli za huduma za kijamii.
"Nitakuwa
tayari muda wote, nitatatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Jimbo langu,
hivyo naomba wanichague, kwani neema ipo njiani," anaeleza.
Mwanaidi anawaambia wananchi wa Jimbo hilo watarajie mazuri kwani wamepata kiongozi bora, anaejali maslahi ya jamii, hivyo atawathamini sana.
Atatekeleza
vyema majukumu yake ya kazi bila kuathiri majukumu ya kifamilia, hiyo italeta
thamani kubwa kwake na kuwa mfano kwa jamii iliyomzunguka hasa kwa wale wenye
mawazo hasi kwamba mwanamke hawezi kuongoza.
Anafafanua
kuwa, elimu ya uongozi hajawahi kupata sehemu yeyote, isipokuwa baada ya kupita
kwenye kura za maoni, wagombea wote waliitwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar
kupatiwa mafunzo, ambapo na yeye alipata nafasi hiyo.
"Lakini
kupitia vyombo vya habari nilikuwa nilisikia kuhusu umuhimu wa mwanamke
kuongoza na ndio maana nilipoona jamii sasa imebadilika kwa kupata uwelewa na
mimi nisiwe nyuma kwenye hilo," anafafanua.
Anawaomba
wananchi wazidishe ushirikiano kwake na wamchague ili apate nafasi ya kwenda
kuwatetea kwenye chombo cha maamuzi.
Mwanaidi
alikuwa mwanachama wa kawaida tangu alipojiunga na chama hicho mwaka 2001 akiwa
kidato cha nne na hakuwahi kushika nafasi yeyote ya uongozi.
"Harakati
za kusaka uongozi nimeanza mwaka huu wa 2025 na ndio nimebahatika kuingia
kwenye mchakato, namshukuru sana Mungu kwa kunijaalia hii nafasi,"
anasema.
Mgombea
huyo anaeleza, tangu ajiunge na chama hicho hajawahi kupata changamoto yeyote
na hata hapo alipogombea pia, hiyo ni kuonyesha wazi kwamba sasa elimu ya
uongozi kwa wanawake tayari imeshawaingia akilini wananchi.
Mtu
wa karibu wa mgombea huyo, Farida Juma Khamis anasema mwanaidi ni mwanachama
mwenzake wa muda mrefu ambae wanashirikiana kwa hali na mali katika kukijenga
chama chao.
Anasema,
mgombea huyo hajawahi kushika nafasi yeyote ya uongozi ingawa mwaka huu amepata
mwamko wa kugombea na hasa kwa vile chama chao kinatoa fursa kwa wanachama
wote.
"Naamini
atakapofanikiwa kuwa mwakilishi atatekeleza vizuri majukumu yake katika Jimbo
na kuhakikisha analiletea maendeleo, pia chama chetu kimesema kitasimama imara
kuhakikisha atakaefanikiwa anatimiza ahadi alizoziweka kwa wananchi wakati wa
kuomba kura, hivyo kupitia msukumo huu atafanya wajibu wake vizuri,"
anaelezea.
Farida
amlisisitiza Mwanaidi kuwa, atakapofanikiwa kuwa mwakilishi basi zile siku
ambazo vikao vya Baraza vitafungwa, arudi kwa wananchi kusikiliza kero zao, ili
atakaporudi aziwasilishe, hiyo itamfanya aaminike zaidi na mara nyengine apite
jimboni bila kupingwa.
Mwenyekiti
wa chama hicho Mkoa wa Kaskazini Pemba Raya Juma Othman anasema, mgombea huyo
yupo vizuri katika kutekeleza majukumu yake ya kazi, hivyo atakapofanikiwa
kupata nafasi hiyo ahakikishe anatimiza ahadi alizoziweka kwenye kampeni.
"Mpango
wa chama chetu ikiwa wagombea wote watakafanikiwa, watahakikisha wanaleta
mafanikio kwenye majimbo yao, kwa sababu tutakuwa nao bega kwa bega na
kumuelekeza, hivyo hatowasahau waliomchagua," anasema Mwenyekiti huyo.
Alimuomba
mgombea huyo, akifanikiwa kuwa mwakilishi awe anaejali maslahi ya wananchi wake
na ikiwa atakosa basi asivunjike moyo, kwani chama kipo pamoja nae na kitampa
msukumo itakapofika uchaguzi mwengine wa mwaka 20230.
Mgombea
huyo ameolewa na ana watoto watano, ambapo ana elimu ya kidato cha nne
aliyosoma katika skuli ya Secondari ya Fidel Castro.
MWISHO.

Comments
Post a Comment