NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
ACHA kufukua makaburi, kujua
yaliopita kwa siasa za Pemba.
Maana chaguzi sita za vyama vingi, zilizokwishapita, ukiamua kufuakua makaburi, wapo watakolia, watakaofuta machozi na wingine
kupoteza fahamu.
Acha kabisa, kuuliza, kufungua
ripoti, kusaka takwimu, kuingia kwenye mitandao ya kijamii au kusililiza
rikodi, za maovu yaliopita.
Wewe jua tu, kuwa taifa la Tanzania
tokea pale lilipofanya uchaguzi wa kwanza mwaka 1995, sasa linaingia uchaguzi mkuu
wa saba Oktoba 29, mwaka huu.
SIASA ZA MWAKA HUU ZINATOFAUTI GANI?
Juzi nilishuhudia siasa za
kiungwana, kistaarabu na za kisheria, kwa wafusia wa vyama vya CCM kubishana
kwa hoja za sera, na wenzao wa ACT-Wazalendo.
‘’Huyu Dk. Mwinyi anafaa, maana
kwanza ni daktari atawafanyia uchunguuzi na kisha kuwatibu nyote ACT-,’’ni
maneno ya kisera kutoka kwa wanaccm wa Chambani Mkoani.
Ali Khamis Juma, aliwaamba wafuasia
wa ACT-Wazalendo kuwa, wampe tu kura Dk. Mwinyi, maana ameshafanya mingi, ili
pate kuyaendeleza.
Asha Said Khalfan nae wa CCM, aliwataka
wafuasi wote wa vyama vyingine, kubakia na vyama vyao, lakini kura kumpa Dk.
Mwinyi.
Utani huo, wa sera huku kila mmoja
akiwa na picha za mgombea wake, ghafla wafuasi wa ACT-Wazalendo, nao walijibu
kwa kumnadi mgombea, wao kiaina.
‘’Jamani kila kitu cha nchi hii,
kinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, sasa nyinyi CCM mnashindwaje kumpigia kura
baba OMO,’’alihoji Hija Kombo Ali wa Mgagadu.
Yeye ni mfuasi wa ACT-Wazalendo,
akawanadia sera wafuasi wa CCM, waliokuwa wakiwasubiri wenzao, kuelekea kwenye
uzinduzi wa kampeni Jimbo la Kiwani.
‘’Si mnamuona kwenye picha
alivyopendeza, na huyu ni mwanasheria nguli na dunia inamjua, mnashindwa nini
kumpigia kura, ili tuongozwe kisheria,’’alihoji.
Mafunda Hamad Juma nae mfuasi wa ACT,
alisema wagombea wote ni wazuri, ingawa anayetoka kwenye chama chao, ni mzuri
zaidi na ana haiba ya kuwa raisi.
Hayo, yalikuwa madogo, eneo la
Ukutini wafuasi wa ACT-Wazalendo wao walitangaaza sera za chama chao, kwa
mtindo wa kunyanyua picha juu kwa pamoja.
Huku wanaccm nao, walitumia picha
wagombea wao na kuonesha ishara ya mitano tena, kwa Dk. Mwinyi na kumtaja mama
Samia, kuwa anatosha.
Kijana Said Juma Omar wa Ngwachani,
anasema siasa za kushindanisha sera na uzuri wa picha za mgombea kwa Pemba, ni
ishara nzuri.
‘’Maana tulishazoea ikifika mwezi
mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, kisiwa cha Pemba, huwa mshike mshike na kujaa na woga
hata chumbani mwako,’’anasema.
Maryam Haji Mohamed wa Wawi, anasema
kwa sasa hali ya Pemba, iko shuwari kama vile hakuna uchaguzi mkuu siku chache
zijazo.
‘’Kinachonifurahisha ni kuona, mwaka
huu uchaguzi huwenda ukawa mwepesi kiamani, na kila mmoja kuvaa sare ya chama
chake, bila ya hofu,’’anasema.
Leila Hassan Hija wa Pujini, anasema
sasa unifomu za vyama, hazionekani tena kama ni uadui, bali ni nguo kama zilivyo
nyingine.
Adam Said Hamad wa Mchanga mdogo,
anasema kwa sasa, hakuna tena maskani za vyama, ambazo zinapiga marufuku
wafuasi wa vyama vingine, kupiga soga.
‘’Hapa kwetu tunaangalia tv katika
banda lolote la vyama, na hata kama utavaa sare za CCM unaingia kwa ACT na yeye
anaingia kwa CUF,’’anasema.
WENYE MAMLAKA
August 20, mwaka huu ndani ya
ukumbi wa Manispaa Chake chake, Jeshi la Polisi Zanzibar lilikutana na waandishi
wahabari, likiwataka kuhakikisha kalamu zao, hazizai chuki.
Kamishina wa Polisi Zanzibar ‘CP’
Kombo Khamis Kombo, akasema inawezekana kufanyika kwa kampeni na wafuasia
kubaki na vyama na sera zao, bila uvunjifu wa amani.
‘’Katika kutunza amani hasa kipindi
cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi, kila mmoja ana nafasi ya kuondoa
viasharia vya uvunjifu wa amani, mkiwemo waandishi wa
habari,’’alisisitiza.
Waandishi wa habari wenyewe, Septamba 15, mwaka huu walishauriwa
kutumia kalamu na vipaza sauti vyao vizuri, kutangaza habari, zinazohusiana na
uchaguzi, kwa lengo la kulinda amani.
Aliyewapa kauli hii, alikuwa ni Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar
Thabit Idarous Faina, wakati alipokuwa akitoa mafunzo kwao, kwa lengo la
kuwajengea uwezo, juu ya usambazaji wa habari bora.
‘’Kalama za waandishi na hasa wanaotumia mitandao ya kijamii,
zinaweza kuwa chanzo kikuzuri cha kutuliza jazba na wafuasi wakashindanisha sera,’’alisema.
Hata wanawake waliotia nia kutoka vyama vya siasa, kumbe nao walishauriwa
kunadi sera za vyama vyao, sio matusi.
Maana Mkurugenzi wa mradi wa kuwawezesha wanawake katika masuala
ya uongozi na demokrasi kutoka PEGAO, Hafidh Abdi Said, alisema machafuko
na vurugu, sio utamaduni wa Zanzibar.
WAGOMBEA
Septemba13, mwaka huu mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT -Wazalendo Othman Massoud Othman, kwenye
uzinduzi wa kampeni Tibirinzi, alitaka kwanza amani itawale.
‘’Kwanza amani na kisha ndio chama, maana
kinyume chake, hakutatawalika, hakutohesabika kura na wala hizi kampeni hazitofanyika,’’alisema.
Hata mgombea urais wa Zanzibar, kutoka ADA-TADEA Juma Ali
Khatib, amesona sio busara kwa wafuasi wake, kujibu mashambulizi.
‘’Nyinyi msikubali kuchokozeka, na kuiacha Pemba hii kuwa na
uvunjifu wa amani, maana athari yake huwapata wanawake na
watoto,’’aliwakumbusha.
Jambo kama hili, liligusiwa na mgombea urais wa Chama cha ‘ADC’
Hamad Rashid Mohamed, kwa kuwataka wanachama wa vyama vya
siasa, kuondokana fujo zinazopelekea madhara kwa sababu tu ya siasa.
Huwenda wananchi wa Pemba, kwa kukumbuka madhara ya kisasa ya
chaguzi sita zilizopita, na ndio maana leo, tukiwa ndani ya siku zisizidi 25,
Pemba ni shuwari.
Kwani wagombea kadiri wote, pamoja na kunadi sera, lakini jambo
la kuomba amani na utulivu, kama vile ni lazima kulitaja na kulisisitiza.
Kwani hata mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha NRA,
Khamis Faki Mgau, nae alishasema wazi kuwa, suala la amani ndio kipaumbele
chake.
‘’Kwanza amani, pili amani, tatu amani kisha ndio chama changu,
maana nimepanda ya juu ya jukwaa kwa amani iliyopo,’’anasisitiza.
Kwenye kampeni za CCM uwanja wa Gombani Chake chake, mgombea
uraisi wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, akawatoa hofu wananchi juu ya
amani.
‘’Nendeni mkakipigie kura CCM, Oktoba 29, mwaka huu na msiwe na
hofu yoyote ya vunjifu wa amani, kwani ndio hazina yetu,’’anasema.
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia
Suluhu Hassana, alilirejea neno la kutunza amani, akisema vikosi vipo kwa kazi
hiyo.
VIONGOZI WA DINI
Sheikh Said Ahmana Mohamed, kutoka Ofisi ya Mufti, akawakumbusha
wagombea, kwamba wasikubali kuwa sehemu ya machafuko, watabeba dhima kwa
Muumba.
‘’Tumia
ulimi wako, maneno yako, mdomo wako na maarifa yako, kutowagombanisha watu,
wala kuwaingiza kwenye madhara, likitokezea unabeba dhima,’’aliwakumbusha.
Mseminari
kutoka Kanisa Katoliki ‘RC’ Barnabas, alisema kwenye kongamano la amani Mkoani,
kuwa kanisa haliridhishwi na uwepo wa fujo.
‘’Fujo,
uvinjifu wa amani, vita havina mwisho mzuri kwa wananchi, na ndio maana
tunataka amani kwanza, kisha mingine,’’anasema.
NYARAKA
Katiba
ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzani, Ibara yake ya 26, ikifafanua haki kwa wananchi
wa kutii sheria za nchi, kama ilivyo ya Zanzibar ya mwaka 1984, kifungu cha 23,
kikisitiza wajibu wa kulinda mali.
Ibara
ya 29 ya Mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu, inayataka mataifa
kuhakikisha kuwa, watu wenye ulemavu wanashiriki
kwa ukamilifu katika medani ya siasa kwa amani.
‘’Kulinda haki ya watu wenye ulemavu,
kupiga kura kwa siri wakati wa uchaguzi na bila kudhalilishwa, kuchukua dhamana
za uongozi na kutekeleza masuala yote ya umma, katika ngazi zote za serikali,’’unafafanua mkataba huo.
Sheria ya Watu wenye Ulemavu nambari 8 ya
mwaka 2022, kifungu cha 28 (1),(e), kikisisitiza haki kadhaa kwa watu hao,
ikiwemo ya kisisasa bila ya kubaguliwa.
Ndio maana, sheria ya Uchaguzi nambari 4 ya
mwaka 2018, kifungu cha 63 (3), kikabainisha kuwa, kampeni zitafanyika hata kwa
njia ya misafara ya vyombo vya moto na mkutano, kwa amani.
Kanuni za maadili ya uchaguzi ya mwaka
2025, Ibara ya 16, (1), kimepiga marufuku kwa kiongozi wa chama, mwanachama,
mshabiki, mfuasi wa chama kufanya fujo na vitendo, vya hujuma katika kampeni.
Kanuni hizi zinafafanua kua, ni kosa
kuharibu mwenendo wa uchaguzi na kampeni za wagombea wengine, pamoja na kufanya
vitendo vinavyopelekea kuibua chuki, vitisho, fujo, udhalilishaji wa makundi maalumu
katika kutekeleza malengo ya kisiasa.
Mwisho




Comments
Post a Comment