'Anasema
mwaka huu ndio aliopangiwa na Mungu kuingia jimboni kugombea, ...awaomba
wananchi kumchagua'
IMEANDIKWA
NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
"Alienipita
kwa kura moja 2020, nimempita kwa kura 62 kwenye kura za maoni mwaka huu 2025,
hivyo nimeshinda kwa kishindo,"
Maneno
hayo ya furaha yalimtoka mgombea uwakilishi Jimbo la Tumbe kupitia chama cha
Mapinduzi CCM Salma Khamis Tumu wakati akizungumza na mwandishi wa makala hii
huko kijiji kwao.
Salma
mwenye umri wa miaka 53 mkaazi wa shehia ya Tumbe Magharibi anasema, ameamini
kwamba riziki ya mtu haiendi kwa mwengine bali siku ikifika, itamfika tu
mwenyewe.
Pamoja
na kushindwa kwenye kura za maoni kwenye uchaguzi uliopita wa mwaka 2020,
lakini hakukata tamaa bali ajijipanga kugombea tena 2025, ambapo alipitishwa
kwa kura 134 huku mpinzani wake ambae ni mwanamme akijipatia kura 72.
Mgombea
huyo anasema, hizo ni baraka za Mungu kumjaalia kupita kwenye nafasi hiyo,
hivyo amewaomba wananchi wamchague ili awaletee maendeleo katika Jimbo lao.
"Nawashukuru
sana wajumbe kwa kuona umuhimu wangu wa kunichagua, nawaahidi kushirikiana nao
bega kwa bega kuhakikisha Jimbo letu linakuwa la mfano katika kulipatia
maendeleo kwa haraka," anasema.
Anasema,
mwaka 2015/2020 aliwahi kushika nafasi ya udiwani na kuwaletea maendeleo
wananchi wa Jimbo lake kulingana na uwezo wake, hivyo basi atakapochaguliwa
kuwa mwakilishi atahakikisha analeta maendeleo zaidi, kwani atazitumia vizuri
pesa za mfuko wa Jimbo, kuwanufaisha wananchi.
Alipokuwa
diwani, Salma alijenga mnara wa kuweka tangi la maji katika skuli ya msingi
Tumbe pamoja na kusaidia fedha kwa ajili ya kuunga umeme, hivyo amekuwa
akisaidia kutoa mchango wa hali na mali pale panapohitajika.
"Nilitoa
fedha zangu mfukoni kutekeleza hayo, lakini pia nilikuwa naibua changamoto
mbali mbali na kuzifikisha sehemu husika kwa ajili ya kutatuliwa, hivyo
tulikuwa tunashirikiana na mbunge na mwakilishi kuzitatua," anaeleza
mgombea huyo.
Anasema,
juhudi alizokuwa akizichukuwa alipokuwa diwani katika kuwafikishia wananchi
huduma bora, ndizo ambazo atazitumia wakati atakapopata nafasi ya uwakilishi,
kwani amejipanga kutekeleza mambo mbali mbali kuhakikisha changamoto zote za
Jimbo zinamaliza.
Amejipanga
kujenga vyoo kwenye skuli mpya ya msingi ya Tumbe, ili watoto waanze kuitumia
kujipatia elimu, jambo ambalo litwapunguzia masafa makubwa ambayo ni
kikwazo kwao hasa ukizingatia ni wadogo.
"Skuli
hiyo ilianza kujengewa kwa nguvu za wananchi wakisaidiwa na viongozi wa majimbo
pamoja na Serikali, lakini kwa sasa inahitaji vyoo ili ianze kutumika, hivyo
nikichaguliwa nitajenga vyoo watoto wapate kusoma karibu, kwani skuli
wanayosoma ni mbali," anasema.
Mgombea
anafafanua, Ilani ya chama cha Mapinduzi CCM imeeleza, itajenga hospitali ya
kisasa kwenye Jimbo lao, hivyo atakapokuwa kiongozi atalisimamia hilo kuona
kwamba inajengwa kwa ajili ya kuwapatia huduma bora wananchi.
Atahakikisha
pia kinajengwa kituo cha mafunzo ya Amali ili vijana wajiendeleze kielimu, hali
itakayowasaidia kupata ajira, kwani kiwanja kipo kimeshapimwa kwa ajili ya
ujenzi na Serikali imeahidi kukijenga kituo hicho.
"Sitowaacha
nyuma wanawake katika kupata haki zao za msingi sambamba na kuwasimamia watoto
wasitelekezwe, kwani ndio chanzo cha kudhalilishwa na kukosa huduma zao za
msingi," anaeleza.
Salma
amejipanga kuhakikisha vikindi vya ushirika vinapata mikopo ya kujiendeleza
kiuchumi huku akikusudia kuwasimamia watu wenye ulemavu kupata haki zao stahiki
na kupata huduma bora na rahisi popote wanapohitaji huduma za kijamii.
Vile
vile anafafanua kuwa, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa ahadi ya kuwanunulia boti
wavuvi ili wajipatie kipato, hivyo atakapofanikiwa kuwa mwakilishi atalikumbushia
suala hilo mara kwa mara kwa ajili ya kutekelezwa na wapate kuendeleza na
shughuli zao za uvuvi bila kikwazo.
Anawataka
wananchi wa Tumbe wazidishe imani kwake na wamchague, kwani amejipanga
kuwatatulia changamoto zote zinazowakabili ikiwemo ukosefu maji safi na salama,
ambayo bado ni tatizo kwa baadhi ya vijiji.
"Wananchi
watarajie mazuri baada ya kunichagua kwani nitashirikiana na viongozi wangu wa
Serikali katika kuhakikisha tunamalizia kero zote kwenye Jimbo letu,"
anasema.
Anawaomba
wananchi kwenda kumpigia kura yeye pamoja na viongozi wengine wa chama chao
ifikapo Oktoba 29, ili wapate kuongoza na kuwaletea maendeleo katika nchi.
Mgombea
huyo anasema ameshawahi kushika nafasi mbali mbali za uongozi baada ya kujiunga
na chama hicho mwaka 1992, ambapo alianza kuwa Katibu wa CCM tawi la Tumbe na
pia kuwa Katibu wa UWT Jimbo la Tumbe.
"Pia
nilipokuwa diwani nilikuwa Makamo Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni
kwenye Baraza la Madiwani na nafasi hizo niligombea na kufanikiwa," anaeleza.
Kupitia
nafasi hizo alizozisimamia, mgombea huyo uwakilishi zimemjenga ujasiri na
uthubutu wa kusimama na kuweza kuongea, hali iliyomfanya aendelee kugombea
nafasi za juu za uongozi ili apate kuwatetea wananchi, kwa ajili ya kupata
maendeleo katika maeneo yao wanayoishi.
Mume
wa mgombea huyo, Ali Kombo Hindi anamuelezea mke wake kuwa ni mpambanaji na
anatekeleza majukumu yake vizuri katika nyadhifa zote alizowahi kuzisimamia,
hivyo anaamini na hiyo nafasi ya uwakilishi ataisimamia vizuri.
"Kwa
kweli tangu aingie kwenye harakati za uongozi mke wangu anatekeleza wajibu wake
vizuri na nina hakika akifanikiwa kuwa mwakilishi ataliletea maendeleo Jimbo
letu," anaeleza.
Anasema
kuwa, suala la uongozi kwa wanawake ni muhimu sana kwani wana huruma na waoga,
hivyo wanajitahidi kutekeleza yale yanayoyakiwa katika kuhakikisha jamii
inakuwa bora na yenye maendeleo.
"Katika
familia tunampa ushirikiano mkubwa na ndio maana akapata ujasiri wa kusimama na
kuingia jimboni kugombea, tutaendelea kumuunga mkono ili afanikiwe,"
anasema baba huyo.
Katibu
wa CCM Jimbo la Tumbe Mohamed Mwewe Omar anamfahamu mgombea huyo kuwa ni
mwanaharakati wa shughuli mbali mbali za kimaendeleo, kijamii na kisiasa na
ameshashika nafasi mbali mbali za uongozi wa kuchaguliwa pamoja na kuteuliwa.
Mohamed
anamuelezea Salma kuwa ni mwanamke anaejitolea, anaependa kushiriki na
kushirikishwa, hivyo atakapopata nafasi hiyo ya uwakilishi itakuwa ni chachu ya
maendeleo katika Jimbo lao na nchi kwa ujumla.
"Tumemuona
katika nyadhifa alizosimamia mwanzo, alitekeleza ipasavyo majukumu yake na
kusimamia kero kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi," anafahamisha Katibu huyo.
Katibu
huyo anamtaka mgombea huyo, atakapopata dhima ya kulisimamia Jimbo baada ya
kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu, ajitahidi kutekeleza yale yote aliyowaahidi
wananchi kipindi cha kampeni, kwani muungwana ni vitendo, hivyo inatakiwa vitendo
vionekane.
"Pia
akubali kushauriwa kwani ushauri ni njia muhimu ya kufikia mafanikio,"
anaeleza.
Salma
ameolewa na ana watoto na wajukuu, ambapo harakati zake za kuongoza zilianzia
mwaka 1992 mara tu baada ya kujiunga na chama.
Mgombea
huyo ametekekeza haki yake ya kushiriki katika demokrasia na uongozi, kama
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1964 ilivyoeleza kwenye kifungu cha 21 (2) cha na
kifungu cha 67 (1) cha Katiba hiyo kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.
MWISHO.
Comments
Post a Comment