Na AMRAT KOMBO , ZANZIBAR @@@
Kwa miaka mingi, siasa imekuwa ikitazamwa kama uwanja wa wanaume. Lakini kwa Chumu Juma Abdallah, mwanamke mwenye umri wa miaka 40, mtazamo huo unabadilika taratibu, Kutoka kuwa kijana aliyekuwa na shaka ya uwezo wake.
leo amekuwa kiongozi anayetazamwa kwa heshima, akigombea Uwakilishi wa Viti Maalum na nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Alliance for African Federal Party (AAFP) kwa upande wa Zanzibar.
“Nilianza nikiwa ninaogopa, nikiamini siwezi, lakini viongozi wangu walinipa moyo. Waliniambia ninaweza, nami nikaamua kuthibitisha,” Amesema Chumu.
Safari ya Chumu kielimu ilianza mwaka 1990 katika Skuli ya Msingi Hurumzi, kisha akaendelea na Skuli ya Sekondari Hamamni mwaka 2000. Mwaka 2002, alijiunga na Chuo cha Muslimu Mazizini, hatua aliyosema ilimsaidia kujijenga katika maadili na kujiamini.
Akiwa mtoto wa nne kati ya watoto nane wa Mzee Abdallah, Chumu anakumbuka jinsi wazazi wake walivyokuwa na mashaka kuhusu azma yake ya kuingia kwenye siasa.
“Mwanzoni hawakuamini, lakini walipoona jinsi ninavyopambana kwa nidhamu na bidii, wakaanza kuniunga mkono,” Amesema Chumu.
Mwaka 2009, akiwa kijana wa miaka 24, ndipo maisha yake ya kisiasa yalipoanza kwa bahati. Alivutwa na hamasa ya wananchi na wanachama wa Alliance for African Federal Party (AAFP) waliovutiwa na ujasiri wake wa kuzungumza kwa hoja.
Chumu alianza kama mjumbe wa kawaida, kisha akapanda ngazi hadi Naibu Katibu Mkuu wa AAFP upande wa Zanzibar, baadaye Makamu wa Wajumbe wa Kina Mama wa chama hicho. Leo, anatafuta nafasi mbili kubwa zinazohitaji uzoefu, busara, na moyo wa utumishi , Uwakilishi wa Viti Maalum na Makamu Mwenyekiti Taifa wa chama kwa upande wa Zanzibar.
“Nafasi hizi mbili ni jukumu kubwa, lakini naamini ninaweza. Si kwa maneno, bali kwa matendo,”Amesema Chumu.
Mbali na siasa, Chumu amejitolea sana katika jamii, hasa katika kuinua wanawake na vijana. Kupitia mafunzo kutoka TAMWA–Zanzibar na semina za chama chake, amekuwa mstari wa mbele kuwajengea uwezo wanawake katika ujasiriamali na uongozi.
“Mafunzo yamenifundisha kuona thamani ya mwanamke na nguvu ya kijana. Kila mmoja ana mchango mkubwa katika kujenga taifa,” Amesema Chumu
Kwa moyo huo wa kujitolea, aliunda kikundi cha kikoba cha vijana 25 wanawake na wanaume kwa lengo la kuweka akiba bila riba na kuanzisha biashara ndogo ndogo.
“Nilitaka vijana wajifunze kuweka na kuwekeza. Leo, wengi wao wana biashara zao, jambo linalonipa faraja kubwa,” Amasema Chumu.
Chumu hakufika alipo bila changamoto. Anakiri kukutana na upinzani, mitazamo hasi, na maneno ya kubezwa hasa kutokana na kuwa mwanamke ndani ya chama cha upinzani.
“Kuna waliokuwa wananiona kama msaliti kwa sababu chama changu si tawala. Lakini mimi naamini katika kushirikiana kwa maendeleo ya nchi,” Amesema Chumu.
Kwa mtazamo wake, siasa siyo vita, bali ni jukwaa la mijadala ya kimaendeleo. Ndiyo maana anaamini uongozi lazima ujengwe katika misingi ya uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji.
Kama atapata fursa ya kutumikia nafasi anazogombea, Chumu ana mipango thabiti ya kuimarisha ushiriki wa wanawake na vijana katika maendeleo ya nchi.
Anasema malengo yake ni Kuelimisha wanawake kuwa siasa si ya wanaume pekee. Kukuza programu za mafunzo ya uongozi na ujasiriamali kwa vijana na wanawake.
“ kuanzisha vikundi vya kijamii vyenye mikopo isiyo na riba , Kuimarisha uongozi wa uwajibikaji, pamoja na wanawake , vijana nao wajue kuwa kuongoza hakuhitaji umri mkubwa, bali moyo wa kuhudumia watu.” Amesema Chumu
Ali Hassan Mussa, Katibu Mwenenzi wa Alliance for African Federal Party (AAFP), amesema ni kiongozi mwenye maono na moyo wa kujituma.
“ Chumu ni kijana mchapakazi asiogopa changamoto yoyote, ameanza kushiriki kwenye siasa akiwa mdogo , tumemuamini sana kutokana na juhudi zake na anaweza kufika mbali akiendelea na mapambano yake bila ya kukataa tamaa.” Amesema Chumu
Khamis Ali, mkazi wa Fuoni, naye amesema anapendezwa na uongozi wa mgombea huyo kwani ni mchapakazi na mwenye kujitambua .
“ Chumu ni mfano wa mwanamke mwenye uthubutu, anayejituma bila kuchoka. Tumejifunza mengi kwake na anapenda kuona vijana tunajituma.”
Naye Moza Said ambae ni mwanachama wa Alliance for African Federal Party (AAFP), amesema anapenda kuona mwanamke mwenziwe anashika nyazifa mbalimbali , kwani inamuhamasisha na yeye kushiriki katika nafasi za uongozi.
‘‘Napenda jinsi anavyojiamini na kujituma,anaonesha kuwa bora kwenye uongozi wake , hii inanifanya nami kupenda kushiriki katika nafasi za uongozi.” Amesema Moza
Licha ya majukumu mengi ya kisiasa, Chumu amesema amejifunza kuweka uwiano kati ya familia na kazi za chama.
“Ninatenga muda wa familia yangu, kwa sababu mafanikio ya kazi yanahitaji utulivu wa nyumbani,” Amesema Chumu.
Amesema anatamani kuwa kioo cha wanawake wenzake, akiwapa matumaini kuwa mafanikio yanaanza kwa kuamini ndani yako.
“Natamani siku moja wanawake waje kusema, nataka kuwa kama Chumu. Hapo nitajua juhudi zangu hazijapotea.”
MWISHO


Comments
Post a Comment