Na Amrat Kombo, Zanzibar @@@@
UPEPO wa mabadiliko unaendelea kuvuma katika siasa za Zanzibar, safari hii ukivumisha na sauti ya mwanamke.
Kadri Uchaguzi Mkuu wa 2025 unavyokaribia, idadi ya wanawake wanaotia nia kugombea nafasi za udiwani, ubunge na uwakilishi imeongezeka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na mwaka 2020.
Ni dalili ya ujasiri, elimu na hamasa ya kijinsia katika uongozi wa kitaifa ,ishara kwamba wanawake sasa wanajitokeza kwa kujiamini zaidi kushika hatua za maamuzi.
Mwelekeo huu si wa bahati, bali ni matokeo ya juhudi za muda mrefu za serikali, mashirika ya kiraia na jumuiya za kimataifa kuhimiza usawa wa kijinsia katika uongozi.
Kwa mujibu wa takwimu za uchaguzi wa mwaka 2020, Zanzibar ilirekodi idadi ndogo ya wanawake waliofanikiwa kushinda nafasi za uongozi. Kati ya wagombea wa ubunge walioteuliwa na vyama, wanaume walikuwa 257 na wanawake 81, ambapo wanawake walioweza kushinda walikuwa wanne pekee.
Lakini mwaka 2025 hali imebadilika. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imekamilisha uteuzi wa wagombea kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ambapo Wagombea wa Urais wa Zanzibar 11, wagombea wa Baraza la Wawakilishi 484 ,Wagombea wa Udiwani 341.
Takwimu hizi zinaonyesha ongezeko kubwa la wanawake walioteuliwa na vyama kugombea nafasi hizo, jambo linalothibitisha kuwa sauti ya mwanamke sasa inasikika kwa nguvu zaidi kwenye uwanja wa siasa.
Kwa upande wa vyama vya siasa navyo mambo yamebadilika kila chama kimeimarisha ongezeko la viongozi wanawake .
Kaimu Katibu Mkuu wa chama cha National Reconstruction Allince NRA, Ulimwengu Mkandama, amesema mwaka huu umeleta mafanikio makubwa kwa chama chake.
“Mwaka 2020 tulikuwa na wabunge tisa wanawake, lakini mwaka huu 2025 tumefikia 21, wakiwemo wawili wenye ulemavu. Tulikuwa na madiwani wanne, sasa tumekuwa saba, na tumepata wawakilishi watatu wa kike”.Amesema Mkandama
Mikataba mbalimbali imekuwa nguzo muhimu katika kufanikisha mwamko huu ,Mkataba wa CEDAW (1979) , unazitaka nchi wanachama, ikiwemo Tanzania, kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi bila ubaguzi.
Azimio la Beijing (1995) Linahimiza serikali kuondoa vikwazo vinavyowanyima wanawake fursa ya kushiriki kwenye maamuzi na kuweka mikakati ya kufikia uwiano wa kijinsia.
Kwa upande wa chama cha ACT Wazalendo, Msemaji wa Sekta ya Maendeleo ya Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Halima Ibrahim Mohmmed , amesema katika Chama chao hawakubaki kuwa nyuma wamendelea kuwahamasisha wanawake kushiriki kwenye uongozi na kuendelea kuitika mwaka huu.
“Mwaka 2020 tulikuwa na wagombea watano wa ubunge, mwaka huu wameongezeka hadi sita. Wawakilishi walikuwa wanne, sasa ni watano. Hii inaonyesha mwamko wa kweli wa wanawake katika chama chetu na ninaimani takwimu hii itaongezeka .” Amesema Halima
Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) Hususan Lengo la 5, linasisitiza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika ngazi zote za uongozi.
Mkataba wa Maputo (2003) Unazihimiza nchi za Afrika kuweka sera na sheria zinazowawezesha wanawake kushiriki katika nafasi za maamuzi ya kisiasa.
Chama cha NCCR-Mageuzi pia kimeonyesha mabadiliko , kwani mwaka 2020 hakukuwa na wagombea wanafasi mbalimbali ikiwemo uwakilishi, ubunge, urais, pamoja na udiwani lakini mwaka huu mambo yamebadilika.
“Mwaka 2020 hatukuwa na muamko wa kugombea nafasi za urais, uwakilishi, ubunge pamoja na udiwani. Lakini mwaka huu tumepata nguvu mpya tunagombea nafasi zote, ikiwemo urais, wawakilishi wanne, madiwani wanne na wabunge wanne.”Amesema Laila
Mashirika ya wanawake Zanzibar yamepongeza muamko huo ikiwemo TAMWA-Zanzibar imetambua mchango wa wanawake 13 wanaotegemewa kugombea nafasi ya urais na umakamu wa rais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 sawa na asilimia 36 ya wagombea wote 36 walioteuliwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (INEC) kwa ngazi hizo mbili.
Kwa upande wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wagombea wanawake ni watatu, Dk. Samia Suluhu Hassan Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais anayetetea kiti chake, Mwajuma Mirambo Chama cha Union For Multiparty Democracy (UMD), Swaumu Rashid Chama Cha United Democratic Party (UDP) .
Huku nafasi ya Mgombea Mwenza imevutia wanawake 10, akiwemo Chumu Juma Abdallah Chama Cha Alliance For Africa Farners Party (AAFP), Fatma Abdulhabib Fereji (ACT-Wazalendo), Devotha Minja (CHAUMA) na wengineo.
TAMWA imesema kati ya wagombea hao, tisa wametokea Zanzibar mmoja katika nafasi ya urais na nane kama wagombea wenza, jambo linaloashiria historia mpya ya ushiriki wa wanawake katika nafasi za juu za siasa.
“Takwimu hizi zinaonyesha wazi kuwa wanawake wa Zanzibar wanaendelea kuvunja vikwazo katika uongozi wa kisiasa, jambo linaloashiria historia mpya ya ushiriki wao katika nafasi za juu za maamuzi,”
MWISHO



Comments
Post a Comment