HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANAFUNZI kidato cha sita, skuli ya
sekondari ya Kiwani wilaya ya Mkoani Pemba, wamesema tayari Mgombea urais wa
Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ‘CCM’ Dk. Hussein Ali Mwinyi,
amesharejea tena Ikulu, kufuatia utekelezaji mkubwa wa Ilani, sekta ya elimu.
Walisema, kujengwa skuli ya kisasa ya ghorofa na
yenye vifaa vya kisasa vya sayansi, ni ishara ya kukubalika kwake, na tayari
wanamuona ameshaingia ikulu kwa awamu ya pili.
Wakizungumza na waandishi wa habari wa Unguja,
Tanzania bara na wenyeji Pemba jana Septemba1, 2025, kwenye ziara maalum ya kuangalia utekelezaji wa Ilani
ya CCM ya mwaka 2020/2025, walisema kwenye sekta ya elimu Dk. Mwinyi, hana mpinzani.
Walieleza kuwa, ndani ya jimbo hilo la Kiwani pekee,
zipo skuli zaidi ya tatu za ghorofa, ikiwemo yao, yenye vifaa vyote husika.
Mmoja kati ya wanafunzi hao, Saleh Muhisn Haidar,
alisema Dk. Mwinyi ni kiongozi mwenye maono na anayefikiria mbali, katika sekta
kadhaa, ingawa ya elimu amevunja rikodi.
Alifafanua kuwa, baada ya uwekezaji huo wa skuli
yao, watahakikisha wanafanya vyema kwenye mitihani yao taifa, na kuwa matokeo
ya mfano.
‘’Kwenye sekta kadhaa kama vile kilimo, afya Dk. Mwinyi
amefanya makubwa, ingawa kwenye elimu niseme, amevunja rikodi na sisi
tunamuahidi kumrejesha tena Ikulu,’’alieleza.
Kwa upande wake mwanafunzi Rauhiya Ahmed Juma,
alisema kwa sasa, skuli yao imekuwa ikiwapa hamasa ya kusoma kwa bidii, kutokana na
kupatiwa vifaa vya kisasa.
Katika hatua nyingine, alisema
baada ya kumalizika kwa ujenzi wa skuli hiyo, sasa wameanzishiwa kidato cha tano
na cha sita, pamoja kujengewa dakhalia.
Mapema Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo Ali Simai Makame, alisema
kwa hakika Dk. Mwinyi kwenye sekta ya elimu, hawana cha kumlipa, ila asubiri
mazuri, kwenye kisanduku cha kura mwezi Oktoba mwaka huu.
Alieleza kuwa, alichokifanya Dk. Mwinyi kupitia Ilani
ya CCM ya mwaka 2020/2025, haijawahi kutokezea, na kumfanya kila mdau wa elimu,
kuridhia maendeleo hayo.
‘’Ukiangalia ndani ya kipindi cha miaka minne,
amefanya makubwa, ikiwemo ujenzi wa skuli hiyo, jambo lililotupa hamasa ya kazi,
sisi waalimu,’’alifafanua.
Skuli hiyo ambayo inavyumba vya kusomea 45, vinne
vya waalimu, stoo tano, maabara mbili na kubeba wanafunzi 909, kutoka wanafunzi wa zamani 235, waalimu 13 na sasa kuwepo waalimu 26.
Wananchi wa Kiwani akiwemo Mohamed Juma Maalim,
alisema kama kuna watu hawajaona matunda ya Dk. Mwinyi, kwa miaka minne, wafike
kijijini kwao.
‘’Tuna skuli ya kisasa yenye vifaa kamili, na kwa
kazi hii aliyotufanyia, yeye ameshaingia Ikulu asubiri kuapishwa tu,’’alisema.
Nae Aisha Haji Mohamed, alisema kwa sasa watoto wao wanapata haki yao ya elimu, wakiwa ndani ya skuli ya bora na ya kisasa, jambo ambalo hawakulitarajia.
‘’Mimi naona Dk. Mwinyi, hana haja ya
kufanya kampeni, aanze tu kujipanga nini anataka kutufanyia kuanzia mwaka 2026,’’alifafanua.
Mwezi Novemba mwaka 2024, Rais wa Zanzibar Dk.
Hussein Ali Mwinyi, akiwa uwanja wa mpira Konde, alisema, ameshayatekeleza kwa
vitendo, aliyowaahidi wananchi, kama ujenzi wa madarasa 2,773.
Ilani
ya CCM ya mwaka 2020/2025 iliitaka serikali kujenga madarasa 1,500 ingawa ilishavuuka
lengo hilo tokea mwaka 2024, kwa asilimia 184.
Dk.
Mwinyi aliyasema hayo, mara baada ya kuifungua skuli ya skondari ya ghorofa
tatu Konde, kwenye shereha za miaka minne ya uongozi wake.
Serikali ilipanga hadi kufikia mwaka 2025, iwe imeshajenga vyumba 2,000 vya madarasa katika skuli za Unguja na Pemba, ili kuondoa mikondo miwili.
Alisema kama kuna watu wanapiga porojo waangalie
takwimu kutoka wizara ya elimu, zitadhihirisha ahadi zake.
Akizungumza
mafanikio mingine, alisema ni kuongezeka kwa bajeti ya mikopo ya elimu ya juu,
kutoka shilingi bilioni 11.5 hadi shilingi bilioni 33.4, jambo liliongeza wigo
kwa wanafunzi.
Kuhusu ajira za waalimu, alisema
wapo waliokwishaajira 3,384 na mwaka huu wa fedha wengine 1,239 wataajiriwa.
Alisema hayo yanafikishwa, kutokana na kuimarika kwa bajeti ya mendeleo ya wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa kufikia shilingi bilioni 518 sawa na ongezeko la asilimia 552.
Mwisho
Comments
Post a Comment