IMEANDIKWA NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
UZAZI wa mpango ni suala lenye kuleta
utata kwa baadhi ya wanajamii ambalo huchukuliwa kwa sura tofauti.
Kwani kuna baadhi yao huamini kwamba, uzazi wa mpango ni kufunga kizazi moja kwa
moja, jambo ambalo sio sahihi, kwa sababu ni sawa tu na kusema... ‘kumuachisha mtoto’.
Na
kuachishwa mtoto ni kumpa nafasi mama aliejifungua kupumzika kwa ajili ya
kuimarisha afya yake na mtoto, hivyo ni sawa na uzazi wa mpango.
Jamii
ifahamu kwamba kutumia uzazi wa mpango ni muhimu sana katika kuimarisha afya za
akinamama na watoto, kwani dini ya kiislamu imehimiza mtoto kunyonyeshwa miaka
miwili.
Qur-an
tukufu katika Suratul-Baqara aya ya 233 imeeleza kuwa, ‘Wazazi wa kike wanyonyeshe
watoto wao miaka miwili kwa mwenye kutaka kutimiza kunyonyesha…’
Hiyo
inaonesha wazi kwamba, kuachisha mtoto kwa miaka miwili ni muhimu sana kwa
akinamama kutokana na faida inayopatikana ndani yake.
Lakini kuna
baadhi ya akinababa huipa kisogo aya hiyo na kuamua kuwatishia talaka wake zao
wanaohitaji uzazi wa mpango, jambo ambalo sio jema.
‘’Wanachukulia
ile nafasi waliyonayo, kwa vile wamepewa mamlaka makubwa kwa wake zao, wanayatumia
vibaya kwa kuwawekea vikwazo,’’ anasema Salha Hassan Ali Mkaazi wa Mzambarauni
Wete.
Anaeleza, na
hiyo ni kwa sababu hawajali yale maumivu wanayopitia wajawazito mpaka
kujifungua kwao, ndio maana wamekuwa wanyanyasa wanawake.
Amina Khamis
Hamad mkaazi wa Tumbe anaeleza, mwanaume anaejitambua na aliesoma dini yake
vizuri basi hawezi kumkataza mke wake kutumia uzazi wa mpango, kwani anajua
umuhimu wake katika makuzi bora ya mtoto na mke wake.
Fatma Kombo
Khamis (sio jina lake halisi) mkaazi Gombani Chake anaeleza, mume wake wa
mwanzo aliwahi kusema kuwa, mke wake yeyote ambae atatumia uzazi wa mpango basi
ndio talaka yake.
‘’Mimi
hakunitamkia lakini alisema mbele yangu kuwa, nimeshamwambia mwenzako kuwa mke
wangu yeyote atakaetumia uzazi wa mpango ndio talaka yake,’’ anasimulia fatma.
Saumu Said
Mkiji mkaazi wa Pujini anasema, wanaume wengi hawataki wake zao watumie uzazi
wa mpango na huwawekea kikwazo cha kuwatishia talaka, hivyo hubakia kudhoofika
kiafya ili tu alinde ndoa yake.
Anasema, hakuna
jambo wanaloliogopa wanawake kama kutishiwa talaka na ndio maana hata ikiwa
ananyonyesha mtoto kwa miezi mitatu tu basi anachagua kustahamili huku akiumia
lakini sio kuachwa.
‘’Afya ya
mama na mtoto hudhoofika kwa sababu walio wengi hawana huduma nzuri kwenye
familia na pia hawapati muda wa kuwashughulikia watoto wao,’’ anaeleza.
Mwananchi
Massoud Juma Abdalla mkaazi wa shehia ya Shungi anasema, wengine wanahofia
kukimbia kwa uzazi kwa wale wenye uzazi mdogo na ndio maana, waume zao hawataki
kupanga kizazi.
‘’Wanaume
wengine huwa wakali sana mpaka kufikia kuwatundikia wake zao talaka, hii sio
sawa kwa sababu maumivu anayoyajua ni mwanamke,’’ anasema.
Mzume Juma
Faki mkaazi wa Shanake Micheweni alikiri kukataa kutumia uzazi wa mpango yeye
na mke wake kwani wanaamini kwamba watoto wengi ndio watakaowaleteamanufaa ya
baadae.
‘’Sio mimi
tu na hata mke wangu hatutaki tutumie uzazi wa mpango kwa sababu, tukipata
watoto wengi jambo nusu yake watakuwa na imani ya kutulea tutakapokuwa watu
wazima, ‘wahenga walisema…mapofu mengi mzigo’.
Khamis
Makame Khamis wa Shanake Micheweni anasema, wanaume wa shehia yao hupanga uzazi
kwa kuoa mke mwengine, kwani inasaidia yule wa kwanza kupumzika.
‘’Labda
mwanamke awe mgonjwa lakini ikiwa ni mzima hatukubali uzazi wa mpango, lakini
tunajitahidi kuwatafutia samaki kwa wingi, hivyo afya zao zinaimarika,’’ anaelezea.
Mama mmoja
ambae hakutaka jina lake litajwe mkaazi Sizini anahadithia, kuna dada mmoja
mkaazi wa Micheweni mwenye watoto kumi alijiunga na uzazi wa mpango bila kumpa
mumewe taarifa.
Anasema,
baada ya kurudi mumewe alimwambia, jambo ambalo lilimkasirisha sana na kupelekea
kumshambulia kwa maneno machafu mpaka kumwambia kuwa hamtaki tena ndio maana
aliamua kujiunga na uzazi wa mpango.
‘’Lakini
huyo alijiunga na uzazi wa mpango kwa sababu mume wake huyo hampi huduma na
huondoka kwenda nje ya Pemba kwa biashara zaidi ya miezi mitatu, hivyo aliona ni
bora ajiunge kuliko kudhalilika na watoto,’’ anasimulia mama huyo.
Anaeleza
kuwa, akinababa wengi hawataki wake zao wajiunge na uzazi wa mpango huku
wakiwachia majukumu wake zao na wao kwenda na shughuli zao, jambo ambalo
linawadhalilisha sana wanawake na watoto.
Mratibu wa
Afya ya Uzazi Pemba Dk. Rehema Abdalla Abeid anasema, suala la uzazi wa mpango
kwa akinababa bado ni changamoto, kwani mwanamke hata uwape ushauri basi mpaka
amwambie mumewe apate ruhusa.
‘’Sasa
wanawake wengine wanaojiamini kutumia, ndipo pale hutishiwa talaka, kutengwa na
hata sisi watoa huduma hutishiwa maisha,’’ anasema.
Kwa sababu
wanafuatilia mpaka wanamjua daktari aliemshauri mke wake, hivyo hujenga nae
uhasama kwani wanakuwa sio waelewa.
Daktari huyo
anaeleza kuwa, ndio maana wanataka wanaume washiriki kliniki na wake zao kwa
sababu vifo vya mama na watoto vimekuwa vingi na moja wapo ya sababu ni uzazi
wa papo kwa papo.
Mratibu wa
Ofisi ya Mufti Pemba sheikh Said Ahmad Mohamed anasema, ikiwa mke hana sababu
za kisheria basi mume ana haki ya kumkataza, ingawa sio vizuri kumtishia talaka
kwani talaka sio jambo la kuchezea.
‘’Hii
inaleta shida sana na kupelekea kesi kama hizo za kutundika talaka kujaa, kwa
sababu mwanamke ikiwa hakutaki tena na umeshamuwekea kikwazo cha talaka,
atakwenda kujiunga tu,’’ alisema.
Anaeleza
kuwa, mwanamke anatakiwa kutii amri halali za mume wake na asipotii itakuwa
amemuasi, jambo ambalo ni dhambi kubwa.
‘’Lakini
ikiwa ana tatizo la kiafya na akaambiwa na daktari kwamba anatakiwa kupanga
uzazi, basi mwanamme hana budi kukubaliana na hayo, lakini ikiwa atamkataza
itakua amefanya ukatili kwa mke wake,’’ anafafanua.
Waziri wa
Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui katika hotuba yake ya mwaka wa fedha
2021/2022 ameeleza kuwa, watumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango
wamepungua kutoka kinamama 63,261 kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 na
kufikia kinamama 61,379 kipindi kama hicho kwa mwaka 2021/2022.
Kwa mujibu
wa chapisho la Huduma kwa Mtoto Zanzibar la Januari 28, 2021 linaeleza kuwa, kiwango
cha matumizi ya njia ya kisasa ya uzazi wa mpango kwa wanawake wenye umri wa
miaka 15-24 ni kwa asilimia 2 kisiwani Pemba, ambapo kinatofautiana kati ya
asilimia 1 hadi 12 kwa Unguja.
Katika
ukurasa wa Jumuiya ya Wauguzi Zanzibar uliochapishwa Agosti 2019, umefafanua
kuwa, licha ya elimu inayotolewa na sera mbali mbali zilizowekwa na Serikali ingawa
matumizi ya mbinu za kisasa za uzazi wa mpango visiwani Zanbzibar yapo chini
ikilinganishwa na Tanzania bara.
Ambapo Tanazania
bara yaliongezeka karibu mara tatu kati ya mwaka 1996 hadi 2015 huku visiwani
Zanzibar yakiongezeka kwa kiasi kidogo kutoka asilima 8 hadi 14.
MWISHO.
Comments
Post a Comment