NA FATMA
HAMAD, PEMBA@@@@
WAJASIRIAMALI
kisiwani Pemba wameomba kupatiwa elimu ya usarifu wa bidhaa, ili waweze
kutengeneza zenye ubora na viwango, ambazo zitauzika katika soko la ndani na nje ya Pemba.
Wajasiriamali hao walitoa ombi hilo katika mafunzo ya ujuzi wa
kidijitali yaliyofanyika kituo cha uwalimu TC Wingwi wilaya ya Micheweni Pemba.
Biamu Omar Mbrouk mwanakikundi cha hapa kazi cha Wingwi, kinachojishughulisha
na utengenezaji wa sabuni, mafuta na unga wa mwani, alisema wamekua wakitengeneza
bidhaa, ingawa zinashindwa kupata soko, kutokana na kukosa ubora.
Alisema mwani umebainika kuwa ni moja ya dawa inayotibu magonjwa
mengi katika mwili wa mwanadamu, hivyo ni vyema kupatiwa elimu, ili wawe wazalishaji
bora.
‘’Tunatamani siku moja kuona kwamba, na sisi tunaziuza
Tanzania bara na hadi nchi za nje bidhaa zetu, kwani kutatuwezesha kutambulika
na pia kuinua uchumi wetu,’’alisema.
Ali Khatib Ali mjasiriamali wa kikundi cha Tumuombe Mola cha Makangale,
kinachojishughulisha na ufugaji wa vitango bahari, alisema wanahitaji kupatiwa
elimu juu ya usarifu wa mazao, ili kuzalisha kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu.
Alisema kuna utaalamu wa kulima na kuchakata wakati
wanapovuna, ingawa bado wanafanya tu, jambo linalopelekea kukosa bei
wanayoihitaji.
Alisema, endapo
watapatiwa elimu kutawasaidia kufuga kwa uwelewa, na kupata bei nzuri inayolingana
kilimo hicho, ambacho kitawawezesha kujikimu kimaisha.
Nae Abdalla Salim Massoud mwanakikundi cha Ipo sababu, kinachojishughulisha
na ukulima wa mwani, alisema wanahitaji kupatiwa elimu ya utengenezaji wa pagi
za plastiki, kwa ajili ya kufungia mwani wao, ili waondokane na na changamoto
ya uharibifu wa mazingira.
‘’Tunapokata pegi za mikanda au mibura haturuhusiwi, kwani
tunaharibu mazingira, hivyo tunahitaji kupatiwa elimu tutengeneze pegi za plastiki,
ili tuondokane na usumbufu tulionao sasa,’’alishauri.
Alisema Kampuni ya mwani ya Sea weed Corporation walishawahi
kwenda na kufanya utafiti wa kutengeneza pegi hizo, ingawa hadi sasa hawakurudi
tena kwa ajili ya kuwaendeleza.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mratibu wa Fawe Winnifred
Yatuma Manawi, Mjumbe wa bodi ya hiyo Zanzibar Biubwa Mohamed Msellem,
aliwataka wajasiriamali hao, kuyatumia
mafunzo watakayopewa, ili waweze kuleta mabadiliko.
‘’Nyinyi wajasiriamali ambao mmebahatika kushiriki mafunzo
haya, naomba muyachukue na muyafanyie kazi, ili muendeleze vikundi vyenu na muweze
kuzalisha kwa mazao kwa wingi,’’alisema.
Alisema lengo la FAWE, ni kuwakomboa wanawake na vijana kiuchumi,
hivyo ni vyema kuhakikisha wanayafanyia kazi, ili wawe wazalishaji na
watengenezaji wazuri wa bidhaa.
Mafunzo hayo ya siku mbili kwa vikundi vya wajasiriamali
yameandaliwa na Jumuia inayoshughulikia na kutoa masuala ya wanawake na watoto,
vijana na watu wenye ulemavu (FAWE)chini ya ufadhili wa UN WOMEN.
MWISHO


Comments
Post a Comment