NA FATMA HAMAD, PEMBA@@@@
MASHEHA wa mkoani wa kusini Pemba, wametakiwa kutoa taarifa kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), endapo kutatokea kifo cha mwanachama wa mfuko huo katika shehia zao, ili kupunguza udanganyifu hasa katika malipo ya fedha za serikali.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mafao kutoka Mfuko huo Zanzibar, Mussa Yussuf wakati akiwasilisha mada ya dhima ya masheha, katika utoaji wa huduma za ZSSF, kwenye kikao kazi kilichofanyika leo Machi 6, 2025 Tibirinzi Chakechake Pemba.
Alisema kumekuwepo na baadhi ya watu wamekua wakipeleka taairifa za vifo vya jamaa zao katika mfuko huo, ambazo sio za ukweli, hivyo endapo watapeleka taarifa wataepusha kutokea kwa udanganyifu huo.
‘’Wamekua wakitujia watu na taarifa za jamaa zao kufariki na kudai mafao yao, lakini tukifanya uchunguzi tunagundua kwamba sio ukweli ni uzushi mtupu, hivyo mtusaidie,’’alisema.
Alifafanua kuwa, endapo Masheha watatoa taarifa na kupeleka vielelezo sahihi vya marehemu, watasaidia warithi wake kupata mafao yao kwa haraka na kwa wakati.
Akifungua kikao hicho Mkuu wa wilaya ya Mkoani Dk. Hamad Omar Bakar kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Rashid Hadid Rashid, aliwataka masheha hao kuwa na ushirikiano wa hali ya juu, na ZSSF, ili kufanikisha azma na malengo ya mfuko huo.
‘’Ndugu masheha nyinyi mnadhima kubwa katika Jamii, hivyo ni vyema mkaweka ushirikiano na ZSSF, ili kuona kila mwanachama anapata mafao yake,’’alisisitiza.
Nao baadhi ya masheha walioshiriki mkutano huo, walisema watahakikisha wanalifanyia kazi agizo hilo, la kuripoti matukio ya vifo yanapotokezea shehiani mwao, ili kuepusha malalamiko kati ya wanachama na ZSSF.
‘’Tunalichkua na Tutahakikisha mabuku tuliopewa kwa ajili ya kuripoti matukio ya vifo tunayatumia na tunaripoti kwa ZSSF, kwani kutamfanya kila mwanachama, apate stahiki zake,’’alieleza.
Sheha wa Kilindi Nassor Mohamed Khamis, aliomba kwa uongozi wa ZSSF kuzifanyia marekebisho sheria zao, ili sasa masheha nao wawe wanuafaika wa mfuko huo.
Mapema Kaimu Meneja wa ZSSF Pemba Omar Nassib Ramadhan, alisema mfuko daima, umekuwa ukitoa mafao na haki nyingine kwa wakati, pindi mwanachama akitimiza vigezo husika.
MWISHO.
Comments
Post a Comment