NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WATUMISHI wa umma wanaotarajiwa kustaafu wametakiwa kuwa makini wanapopokea ushauri wa watu mbali mbali, ili waepuke kupoteza fedha nyingi bila ya mafanikio.
Akifungua mafunzo kwa wastaafu hao watarajiwa, leo Machi 5, mwaka 2025 Afisa Mdhamin Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi na Utawala Bora Pemba Halima Khamis Ali alisema, kuna watu wengi watajitokeza kuwapa ushauri wa mambo mbali mbali, hivyo wawe makini katika kuupokea na kuutekeleza.
Alisema kuwa, wastaafu bado wana mchango mkubwa kwa taifa, hivyo kuna haja ya kujipanga mapema katika kujitafutia miradi ambayo itaendeleza maisha yao baada ya kustaafu.
"Kila mtu atakujia kukushauri kufanya biashara na wingine watakushauri kufanya vitu vyingine, lakini muwe makini ili fedha zenu za kiinua mgongo, zitumike kuwakomboa kimaisha na sio kuwasababishia matatizo," alisema Mdhamini huyo.
Aliwataka watumishi hao wayafanyie kazi mafunzo waliyopatiwa, kwani wanakwenda kulitumikia taifa kwa upande mwingine, kutokana na kuwa, bado wana nguvu ya kufanya kazi katika kijiletea maendeleo katika familia zao.
"Tunamchango mkubwa kwa taifa hili, kustaafu sio mwisho wa maisha, maisha lazima yaendelee, hivyo ni lazima tujipange katika kujikomboa kimaisha," alieleza.
Mapema Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Pemba Omar Nasib, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanakuwa pamoja na wastaafu hao, ambapo jukumu lao ni kuhakikisha wanapata mafao yao kwa wakati.
"Tunahakikisha mnapewa mafao stahiki na kwa wakati, ili muweze kuendelea na maisha bila ya usumbufu, hivyo muzingatie mafunzo mtakayopewa kwa maslahi yenu na taifa," alifahamisha Kaimu huyo.
Akiwasilisha mada ya matayarisho ya kustaafu na maisha baada ya kustaafu, muwezeshaji mafunzo ya wastaafu kutoka taasisi ya Uhusiano Tanzania (TIA) Williamson Ferdinand aliwataka kufikiria miradi ambayo itawakwamua kiuchumi kabla ya kustaafu kwani wataweza kujipatia fedha sambamba na kufanya mazoezi.
"Mazoezi ni muhimu kwa sababu ni afya, hivyo utakapoanzisha miradi ya maendeleo basi sio kwamba, utapata pesa tu bali hata magonjwa yatapungua," alisema muwasilishaji huyo.
Mshiriki wa mafunzo hayo Kheri Juma Basha aliwashauri wastaafu hao watarajiwa kujipanga vizuri na kufanya kazi bila ya kujiumiza, ili maisha yaendelee vizuri na yasiwe ni changamoto kwao baada ya kustaafu.
"Jambo la kwanza uzingatie utafanya nini, wakati gani na lengo gani, nje kuna fursa mbali mbali tuzichangamkie tutafanikiwa sana katika haya maisha," alishauri.
Kwa upande wake mshiriki Ali Mohamed Ali aliwaelekeza wenzake kujikita kwenye ufugaji wa nyuki kwani utaweza kuinua kipato chao kwa haraka kutokana na kuwa kila kinachotokana kwa ufugaji huo, ni mali.
"Milioni zako tatu tu unaweza kuwekeza kwenye mradi huu, kila anaehitaji aje nimuelekeze, hakuna kitu kinachotoka kwa nyuki kisiwe na kipato," alisema mshiriki huyo.
Katika mafunzo hayo mada mbali mbali ziliwasilishwa ikiwemo mpango mkakati kabla na baada ya kustaafu, lishe na ulaji unaofaa, msongo wa mawazo, matayarisho na taratibu ya mstaafu pamoja na afya ya akili.
MWISHO.
Comments
Post a Comment