NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@@
MKUU wa mkoa wa kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib amesema vikao kazi kwa masheha na watendaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ‘ZSSF’ vinasaidia kuongeza ushirikiano na ufanisi wa kazi.
Alisema, unapokuwa karibu na ofisi ya tawala za Mikoa ndio umeifikia jamii kwa urahisi, na kiyume chake ni kudhoofisha utendaji kazi ofisi isiyotaka ushirikiano na masheha.
Hayo yameelezwa leo Machi 7, 2025 na Mkuu wa wilaya ya Wete Abdalla Rashid Ali, kupitia hutuba ya Mkuu huyo mkoa, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi, cha masheha na watendaji wa ZSSF, kilichofanyika ukumbi wa mikutano Jamhuri Wete.
Alisema, ushirikiano huo ambao ‘ZSSF’ wameuomba ni eneo zuri la utendaji kazi, kwani chanzo cha jamii na kuifikia kwa haraka na wepesi ni uwepo wa masheha.
Alieleza kuwa, kilichofanywa na ‘ZSSF’ kinaashiria umoja na mshikamo katika kufanikisha majukumu ya kila siku, yanayosimamiwa na viongozi wakuu wa nchi.
Alifahamisha kuwa, ndani ya wilaya na mkoa, wamekuwa hawafanikiwa, bila ya kuwatumia masheha katika kazi zao mbali mbali, na hasa ikiwa zinawahusu wanajamii.
‘’Masheha kwetu ndio ‘ingine’ ya kufanikisha kila jambo na ndio maana, wamekuwa wakifanya vyema katika majukumu yetu mbali mbali,’’alifafanua.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa, aliitaka ZSSF kufanya tathmini kila mwishoni mwa mwaka, ili kupata sheha bora na ikiwezekana kupewa motisha, katika kazi zao.
‘’ZSSF ikiwapendeza, ni vyema sasa mkaangalia uwezekano kila mwaka, masheha na hata wa Zanzibar nzima, mkawa mnawatunza kwa aliyefanya vizuri zaidi,’’alifafanua.
Mapema Kaimu Meneja ‘ZSSF’ Pemba Omar Nassib Ramadhan, alisema lengo la kikao hicho, ni kujenga ushirikiano bain yao na masheha.
Alieleza kuwa, masheha ni nyenzo muhimu katika kufanikisha kazi zao za kila siku, ikiwemo kupunguza udanganyifu wa baadhi ya wanachama wao hasa kwa kesi za ugonjwa na vifo.
‘’Hakuna mwanachama wa ‘ZSSF’ asiyeishi katika shehia moja ama nyingine hapa Zanzibar, na ndio maana sasa tunakuja kwenu, ili kuongeza ushikiriana katika kuligundua hilo,’’alifafanua.
Akiwasilisha mada ya dhima ya masheha kutoa huduma za ‘ZSSF’ Mkuu wa kitengo cha mafao kutoka mfuko huo Zanzibar, Mussa Yussuf Mussa, alisema hawana wasi wasi na masheha, katika kufanikisha kazi zao.
Alieleza kuwa, masheha walikuwepo kabla ya mwaka 1964, ingawa baadae, walianzishishiwa sheria yao kuanzia mwaka 1998, wakati wa kuasisiwa kwa ZSSF na kutakiwa kushirikiana nao kati kazo zao.
Akitaja mafao yanayotolewa na ‘ZSSF’ alisema ni pamoja na yale ya uzeeni, ulemavu, uzazi kwa wanachama wa mfuko, warithi ambayo hupewa wale warithi wa marehemu ambae hakulipwa mafao ya uzeeni.
‘’Lakini hata mafao ya upotevu wa ajira, kwa wanachama alifanyakazi na kisha kumaliza kazi yake, mfano ujenzi wa barabara, hoteli kwa ambae hakuongezwa mkataba, na bila ya kutokezea uzembe,’’alifafanua.
Kuhusu fidia kwa wanachama, alisema ni kwa yule aliyeumia kazini, mafao ambayo awali yalikuwa yakilipwa na Ustawi wa jamii, ingawa kwa sasa yamehamishiwa ZSSF.
‘’Zipo taasisi tunashirikiana nazo, katika kutoa mafao hayo, mfano ulemavu na uzazi tunashirikiana na wizara ya Afya, ingawa kwa vifo masheha ni watu muhimu kutoa kumbu kumbu zenu,’’alifafanua.
Baadhi ya sheha hao, waliahidi kushirikiana na ZSSF, kwani imekuwa karibu nao, katika kufanikisha majukumu yao ya kila siku.
Mwenyekiti wa masheha wilaya ya Wete Othman Ali Khamis, alisema daftari walilokabidhiwa, kwa ajili ya kumbu kumbu za watumishi wa tasisi binafsi, waliomo shehia mwao, watalifanyia kazi.
Mwisho
Comments
Post a Comment