IMEANDIKWA NA KHAULAT SULEIMAN, PEMBA@@@
MKAGUZI wa shehia ya Pandani Wilaya ya Wete Pemba, Inspekta wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi amewataka vijana kufanya kazi za kuwapatia kipato ili kuepukana na vitendo viovu, ambavyo ni hatarishi na vinaweza kuharibu malengo yao.
Ameyasema hayo mara baada ya kukabidhi viatu Sultan Hamad Issa ambaye ni mjasirimali mwenye mlemavu wa ngozi mkaazi wa shehia ya Pandani wilaya ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema, kuna baadhi ya vijana wenye ulemavu wanashindwa kujishughulisha na badala yake kutegemea wazee, jambo ambalo linaongeza mzigo katika familia, kwani ulemavu mwengine unamuwezesha kijana kufanya kazi na kuweza kujikwamua kiuchumi.
‘’Nampongeza kijana huyu kwa kushirikiana na wenzake na kujiajiri kwa kuanzisha kikundi cha mifugo, ili kuweza kupata za mkopo, mafunzo na kitendea kazi ambavyo vinaweza kuboresha mradi wao,’’ alisema Mkaguzi huyo.
Aidha, alimpongeza kijana huyo kwa kuamua kushirikiana na wenzake katika kujitafutia riziki na kuachana na dhana potofu ya kwamba watu wenye ulemavu hawana nguvu ya kufanya kazi, hivyo alimshauri asikate tamaa aendelee kupambana kwa maslahi yake na taifa.
“Anzisheni vikundi ili kuona ni kwa namna gani unaweza kupata fursa, fanyeni kazi kwa bidii bila ya kubaguana mtafika mbali, muache kujishirikisha kwenye vikundi viovu, madawa ya kulevya, ubakaji na wizi, hii itawavunjia malengo yenu,’’ alisema.
Nae Sultan Hamad Issa alimshukuru mkaguzi huyo kwa msaada wake kwani changamoto hiyo ilikua ikimkabili kwa muda mrefu, jambo ambalo lilikua likimpatia majeraha katika miguu yake hususan katika kipindi cha mvua.
‘’Nashukuru sana kwa msaada huu kwa sababu sasa nitafanya shughuli zangu za ufugaji bila ya kupata madhara yeyote,’’ alisema mfugaji huyo.
Baba mzazi wa kijana huyo Hamad Issa Salum alisema kuwa, kijana wake amekua ni msaada mkubwa kwake kwani anapenda kujituma katika shughuli mbali mbali, ili kuweza kupata riski ya halali na kusaidia familia yake.
Sheha wa shehia hiyo Khamis Rashid Ali aliwataka wanachi kuendelea kutoa mashirikiano na Jeshi la Polisi katika kupambana na vitendo viovu kwa ajili ya katika ujenzi wa taifa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment