NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
KILA kukicha Seirikali, taasisi binafsi na jamii zinapaza sauti zao ili kuhakikisha wanaondoa vitendo vya udhalilishaji ambavyo kwa asilimia kubwa hufanyiwa wanawake na watoto.
Suala la kukemea vitendo vya udhalilishaji sasa limejaa kwenye mioyo ya watu kwa sababu halipewi nafasi katika jamii zetu, licha ya wachache wanaolifanya na kutia aibu Taifa letu.
Tayari wanajamii waliowengi wameshapatiwa elimu na wanajua athari zinazojitokeza iwapo mwananchi atafanyiwa vitendo vya udhalilishaji na ndio maana wapo tayari kuyazungumzia na kuyakemea kwa nguvu zote.
Wanawake wanaogombea ni miongoni mwa wanakumbwa na changamoto za udhalilishaji ambazo hupelekea kuwaathiri kisaikolojia, kimwili, kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Mwandishi wa makala haya alitaka kujua ni athari gani zinazowakumba wanawake wanaogombea nafasi za uongozi iwapo watadhalilishwa.
Ibrahim Mustafa Mussa ambae ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa wilaya ya Wete kupitia chama cha Mapinduzi CCM anasema, udhalilishaji kwenye vyama unakwaza ushiriki wa wanawake katika siasa kwa sababu wanaweza kuhofia kudhalilishwa na hivyo kupunguza uwakilishi wao katika vyombo vya maamuzi.
Anasema, udhalilishaji kwa wanawake wanaogombea husababisha kuathirika kisaikolojia kwani wanaweza kupata msongo wa mawazo, hofu na kupoteza hali ya kujiamini, jambo ambalo linawaathiri wao na hata familia zao.
‘’Athari nyengine ni kudorora kwa haki za binadamu kwa sababu unapomnyanyasa mtu, unakiuka haki zake za kibinadamu, kwa hiyo hili linaweza kuonyesha kuwa jamii bado haijatoa nafasi sawa kwa jinsia zote kushiriki katika uongozi,’’ anaeleza.
Wanawake huleta mtazamo mpya katika utawala na maendeleo ya kijamii, hivyo ikiwa hawatoshiriki kwa kuhofia kudhalilishwa, basi jamii inakosa mawazo mbadala ambayo yanaweza kusaidia katika maendeleo ya nchi.
Mwananchi Safia Suleiman Iddi mkaazi wa shehia ya Msuka anasema, athari yake ni kuhamasisha matendo ya ukatili wa kijinsia, kwa sababu yanapotokea wanawake huonekana hadharani, hivyo yanaweza kusababisha watu wengine kuona kama ni ya kawaida.
‘’Udhalilishaji huu unaathiri nakudhoofisha demokrasia, wakati mwanamke anapotishwia au kuzuiwa kushiriki siasa kwa hofu ya kudhalilishwa, basi demokrasia inapoteza usawa na uwakilishi mpana wa wanawake,’’ anaeleza.
Saada Saleh Ali ambae ni Mwenyekiti wa Vijana Wilaya ya Wete kupitia chama cha Mapinduzi CCM anaeleza, udhalilishaji huo unawaathiri sana kwenda hatua nyengine mbele kwa sababu yule wanaemkusudia atawasaidia wakati mwengine ndie unawaendea kwa lengo jengine.
‘’Unajikuta anakuja mtu anakwambia yule anaekusaidia ana lengo fulani na ni baya, hivyo ile hamasa inapungua kwa sababu vile vishawishi ambavyo atakuonesha utaona bora ukae upande kulinda utu wako na heshima yako,’’ anaelezea.
‘’Wakati mwengine yule yule ambae ana viashiria vibaya lakini wewe hujamjua lengo lake, basi watu wataanza kukushutumu, kukusema na kukupakazia kuwa unafanya nae ngono, kwa kweli inauma sana,’’ anahadithia.
Saada anajua, hayo ni miongoni mwa changamoto na hapaswi kukata tamaa, kwani baadhi ya watu wanaamini hawawezi kufanikiwa ikiwa hawajadhalilishwa, jambo ambalo sio kweli.
Anasema, mara nyingi wanaume wanapokuhujumu na kukufikiria vibaya wanashirikiana na wanawake, hali inayosikitisha sana kwani wao walipaswa wawaunge mkono.
Moza Massoud Ali ambae ni Mwenyekiti Vijana Mkoa wa Kaskazini Pemba kupitia chama cha ACT Wazalendo anasema, udhalilishaji unawaathiri sana na kurudisha nyuma harakati zao za kugombea kwa sababu ikiwa mwanamme atakukatalia kitu ambacho wewe mwenyewe umejiamulia, anakuwa na nguvu kubwa ya kukuharibia.
‘’Anakupa vitisho na maneno yenye kukukatisha tamaa, hivyo inapelekea kukosa kujiamini kwa sababu unahisi hutofanikiwa,’’ anaeleza.
Zainab Mussa Bakar ambae ni Mwenyekiti wa Wanawake Mkoa wa Kusini Pemba upitia chama cha Demokrasia na Mendeleo CHADEMA anasema, udhalilishaji unawaathiri kisaikolojia kwani wao wamejipanga kufikia sehemu fulani, lakini watu wanawakwamisha hatua tano nyuma kutokana na maneno.
‘’Maneno hayo yanawavunja moyo wanawake, kwa sababu wanaume walikuwa wawaunge mkono kwa nia njema, lakini kwa vile hawako tayari kupitwa na mwanamke, ndio maana wanatukwaza kila sehemu,’’ anafahamisha.
Mratibu wa chama cha Democratic Party (DP) Pemba, Abas Mohamed Khatib anasema, athari yake ni kuwavunja moyo wanawake ambao wa nia ya kugombea, hivyo anakuwa anasitasita kuingia katika harakati za kugombea.
‘’Hali hiyo husababisha kila siku kuwa na viongozi hao hao kwenye chama kwani hawabadiliki, jambo ambalo halileti taaswira nzuri kwenye jamii,’’ anaeleza.
Nini kifanyike
Maryam Saleh Juma mgombea ubunge kupitia chama cha Ukombozi wa Umma mkaazi wa Vitongoji anasema, anashauri wapatiwe elimu zaidi ya uraia, ya haki, ingawa kwa sasa udhalilishaji umepungua kasi kutokana na elimu hiyo, ukitofautisha na zamani.
‘’Tuwe na sheria ambayo ukimdhalilisha mwanamke anachukuliwa hatua za kisheria papo hapo,’’ anashauri.
Mwananchi Subira Makame Iddi mkaazi wa Kiwani anasema, kunahitajika elimu kwa viongozi na wanachama wa vyama vyote vya siasa, kwa sababu wengine hawajui kwamba mwanamke ukimfanyia jambo fulani anapata athari.
‘’Udhalilishaji upo wa aina nyingi kwa hivyo utakapomfanyia aina yeyote ile ya kumdhalilisha basi unamrudisha mwanamke nyuma katika harakati za kugombea kwani wengine ni woga,’’ anafafanua.
Mohamed Haji Kombo Katibu wa Wilaya Chake Chake chama cha wananchi CUF anasema, wanawapa elimu wanachama wao na kujenga ukaribu, jambo ambalo linasaidia sana katika kujenga uthubutu, kuhoji na kupata fursa ya kusema kinachomkwaza.
Ili kuona kuwa wanaondosha athari hizo wamekuwa wakitoa fursa sawa za kudhibiti mianya ya udhalilishaji kwa kutoa fomu bure kwa baadhi ya nafasi wanazogombea kwenye chama.
‘’Kwa vile wengine hawana uwezo kifedha, tumeona kuwa wanaweza kujidhalilisha ili tu wapate fomu, hivyo baaadhi ya nafasi tunaondoa malipo mapema bila kujali mapato ambayo tutayakosa,’’ anaeleza.
Mratibu wa chama cha Democratic Party (DP) Pemba, Abas Mohamed Khatib anasema, anaiomba Serikali kuwa karibu na vyama vya siasa, ili vyama visimilikiwe na mtu binafsi, bali wasimamie katiba zinavyowaongoza, hiyo itasaidia kuondoa udhalilishaji.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa wilaya ya Wete kupitia chama cha Mapinduzi CCM Ibrahim Mustafa Mussa anasema, ipo haja kwa wananchi kuhamasishwa kuhusu haki zao za kupiga kura na umuhimu wa kushiriki uchaguzi bila vitisho au unyayasaji.
Anasema, pia sheria zinazopinga vitendo vya udhalilishaji ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia na lugha za matusi ziimarishe na kutekelezwa kwa haki.
‘’Vyama vya siasa viwajibike kwa matendo ya wanachama wao na kuhakikisha wanazingatia maadili ya uchaguzi, hiyo itasaidia uwajibikaji bora kwa wagombea na vyama vya siasa,’’ anafafanua.
Katibu wa Jumuiya ya Utetezi wa Kijinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) Dina Juma Makota anaeleza, viongozi wa dini na jamii washirikishwe katika kuhamasisha maadili mema wakati wa kampeni na uchaguzi.
‘’Pia waandishi wa habari watumie kalamu zao vizuri kuelimisha jamii na wanawake juu ya kuthamini na kuwa na heshima ya hali ya juu, ili kuondosha dhana potofu ya kuwa wanawake wanaogombea wanafanya uhuni,’’ anaeleza Katibu huyo.
Afisa Mkuu wa Mahusiano kutoka chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA) Sofia Ngalapi anasema, wamekuwa wakitoa elimu mara kwa mara ili wanawake wajiamini na kujiepusha na matendo ambayo yatamfanya aonekane amekosa heshima.
‘’Tunajitahidi sana kuwaelimisha kuhusu mchakato mzima wa kugombea na uchaguzi, hivyo tunaamini kwamba mafunzo tunayowapa yatawasaidia kupambana na changamoto mbali mbali zinazowakumba,’’ anasema.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwenye kifungu cha 12 (1), sura ya tatu imeeleza kuwa, ‘Watu wote ni sawa mbele ya sheria’, huku katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwenye Ibara ya 21 ikieleza ikieleza haki ya kila mtanzania kushiriki kwenye shughuli za utawala, suala la kuchagua na kuchguliwa, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuwa kiongozi bila ya kudhalilishwa.
MWISHO.
Comments
Post a Comment