MARYAM THANI: MWAKILISHI ALIEPANIA KUMALIZA CHANGAMOTO KATIKA JIMBO LAKE, Anasema, ataendelea kugombea uongozi kuhakikisha jimbo lake linapata maendeleo zaidi
NA ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
KATIKA jamii inayokuwa kwa kasi, uongozi wa wanawake umekuwa muhimu zaidi kuliko wakati mwengine wowote.
Leo tunazungumza na mwakilishi wa Jimbo la Gando wilaya ya Wete kupitia chama cha Mapinduzi CCM, Maryam Thani Juma ambae aliepania kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika jamii.
Mwanamama huyo amefanya mambo mengi katika vipindi viwili vya uongozi wake tangu mwaka 2015 hadi sasa ambapo wananchi wa jimbo lake wanannufaika nayo.
Maryam ni mwanamke jasiri alieweza kuvuka vikwanzo vingi na hatimae kufanikiwa kuingia kwenye chombo cha maamuzi baada ya kuchaguliwa na wananchi kwa kishindo.
Baada ya kuwafikishia wananchi wake maendeleo, ilipofika mwaka 2020 alipoingia tena kwenye kinyang’anyiro cha kugombea, alifanikiwa pia.
HARAKATI ZAKE UONGOZI ZILIANZIA WAPI?
Mwakilishi huyo alianza uongozi kwenye chama akiwa kama Katibu wa Uchumi na Fedha katika tawi la Kizimbani Wete Pemba, baadae akawa Mjumbe wa Kamati Tekelezaji ya Vijana Wilaya ya Wete kwa wakati huo.
Baada ya kujiamini na kuona kwamba kuna kipaombele kwa wanawake kwenye nafasi za uongozi, ndipo alipochukua fomu ya kugombea uwakilishi katika jimbo lake.
Aliingia hamasa kubwa na ilipofika mwaka 2015 alichukua fomu ya kugombea na alifanikiwa.
Maryam anasema huku akitabasamu kuwa aliemshawishi kuingia jimboni kugombea zaidi ni mume wake, ingawa mwenyewe pia alikuwa ameshajiwekea malengo, kwani aliona wenzake wanafanikiwa.
‘’Nilipoona kwamba wenzangu wanafanikiwa, ndipo nikaingia shauku ya kugombea, lakini pia na mume wangu alinishawishi na kuniunga mkono,’’ anaeleza.
‘’Nilijuliza…kwa nini nisiweze kugombea? wakati nina haki kisheria, ndipo nikasema mwaka huu naomba Mungu, nashkuru nilifanikiwa mwaka huo huo,’’ anaeleza.
Maryam anataja lengo lake la kugombea kuwa ni, pale alipoona wanaume wengi kwenye nafasi, utetezi wao unakuwa mdogo sana.
Aliona ni vyema aingingie kwenye vyombo vya maamuzi ili aweze kuwainua wanawake wenzake, kutetea na kuzipatia ufumbuzi changamoto za kwenye jamii na kuwafikishia huduma mbali mbali.
Na hilo amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani katika jimbo lake, ndani ya vipindi viwili vya uongozi wake tayari amewafikishia maendeleo wananchi wake.
Anasema, malengo yake ya baadae ni kuendelea kuwatumikia wananchi, kuwasimamia na kuibua changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi kwa maslahi yao na Taifa.
MAFANIKIO YALIYOPATIKANA
Mwakilishi nafahamisha, Baraza la Wawakilishi ni chombo cha kuwatetea wananchi, hivyo kuna mambo mengine ambayo anaweza kuyafanya mwenyewe, ingawa baadhi ni lazima wayasemee tu ili Serikali ikatekeleze kwenye maeneo yake.
Kupitia utetezi wake BLW, tayari wameshajengewa skuli ya ghorofa ya Sekondari Idrisa Abdulwakil iliyopo Kizimbani, hospitali ya wilaya Kinyasini, ujenzi wa tenki ya maji safi na salama lililopo Raha.
Alisaidia uchimbaji wa visima vinne ambapo vitatu walipata msaada kupitia kwa wahisani na kimoja alichimba kwa fedha zake mwenyewe pia alifanya utetezi wa barabara za ndani na tayari wameshaanza kwa hatua za mwanzo.
‘’Pia nimesaidia katika masuala ya elimu kwa kukarabati madarasa na takribani skuli zote zilizomo ndani ya jimbo langu nimezifanyia ukarabati kwa kujenga vyoo na madarasa,’’ anaeleza
Kupitia fedha za mfuko wa jimbo, mwanamama huyo alijenga skuli ya maandalizi iliyopo kijiji cha Kwale Mpona yenye mabanda mawili na wanafunzi wanaendelea kupata elimu.
Anasema, alifanya ukarabati wa vyoo na maskuli mbali mbali pamoja na uchimbaji wa visima vinne, ambapo visima vitatu alisaidiwa na wahisani na kimoja ametumia fedha zake mwenyewe.
Jambo jengine alilolifnya, ni kuwapatia wajasiriamali wanawake vitendea kazi wakiwemo wakulima wa mwani na kuvipatia fedha vikundi nane (8) kwa ajili ya mtaji, ambapo kila kikundi kilikabidhiwa shilingi 200,000.
Maryam alisaidia timu za mpira kwa kuandaa kombe, ambapo alitumia zaidi ya shilingi milioni nne na nusu kwa lengo la kuziendeleza timu na kuwapa hamasa wachezaji.
‘’Vile vile niliandaa kombe la mbuzi, hii ni kwa ajili ya kukuza vipaji vya wanamichezo wetu,’’ anasema.
‘’Pia kuna vikundi nilividhamini wakati walipokwenda kuchukua mkopo kwenye benki ya CRDB lakini wengine hawakwenda kulipa, hivyo nililazimika kutoa pesa yangu mfukoni kuwalipia,’’ anaelezea.
CHANGAMOTO WAKATI WA KUGOMBEA
Anahadithia, zaidi ni kwa wanaume kwani walimkebehi na kumuona hawezi kuongoza wala wanawake hawapaswi kuwa viongozi huku wakinasibisha na dini, jambo ambalo sio sahihi.
Kwa sababu vitabu vya historia vimeainisha wanawake waliopewa nafasi za uongozi katika majukumu mbali mbali, akiwemo bibi Khadija, mama Aisha na wengine.
‘’Niliwaonyesha mifano hai ya maendeleo waliyoyafanya wanawake kwa sababu ni mengi kuliko ya wanaume na nikawaambia wanawake wanaweza kuongoza na kuleta maendeleo ya haraka,’’ anafahamisha.
Anasema, maneno yao hayakumkatisha tamaa na ndio aliposimama imara kugombea na anaendelea kuwatumikia wananchi wake.
Katika kutatua changamoto za jimbo lake, amekuwa akiwashirikisha wananchi na viongozi wa jimbo lake katika shughuli zote na ndio maana malengo yake yanafanikiwa kwa haraka.
Anasema, tangu awe kwenye nafasi hiyo hajawahi kukumbana na changamoto yeyote, anafanya kazi zake pasi na kuyumbishwa, kwani amekuwa ni mwenye kujiamini na yupo imara katika utekelezaji wa majukumu yake.
‘’Hakuna anaenirejesha nyuma katika harakati zangu kwa sababu napambania mabadiliko na wala sisikilizi maneno ya watu wasipenda maendeleo, ninahakikisha mafanikio yanapatikana kwenye jimbo langu,’’ anaeleza.
Mwakilishi huyo ni mzaliwa wa Gando Wilaya ya Wete Pemba na alipata elimu yake ya msingi na sekondari mpaka kidato cha pili katika skuli ya Gando.
Ambapo kidato cha tatu na cha nne alisoma katika skuli ya sekondari Utaani Wete na kumaliza mwaka 2002, ambapo kwa sasa ana mume na watoto watano, wakike wawili na wakiume watatu.
ASASI ZA KIRAIA
Aliekuwa Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, wana mpango mkubwa wa kuwajengea uwezo wanawake na jamii, ili wawe na muelekeo chanya kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.
“Na tumeona kwamba wanawake wengi waligombea katika chaguzi zilizopita, ingawa hawakushinda wote lakini walionesha moyo mzuri na walioshinda wanaendelea kufanya vizuri katika majimbo yao,” anaeleza.
Kwa Pemba, TAMWA imeshawapatia mafunzo wanawake 70 wenye nia ya kugombea na wamewaunganisha na wanawake mashujaa ambao tayari wameshagombea nafasi mbali mbali, ili kuwajengea uzoefu na kuwatoa hofu.
Hafidh Abdi Said ambae ni Mkurugenzi wa PEGAO anaeleza, wanawake wachache wanaokaa katika nafasi za uongozi, wanaonekana juhudi kubwa wanazozifanya katika kutekeleza majukumu yao.
‘’Tulipofanya utafiti kwenye vyama, walituambia kwamba wanapochaguliwa viongozi wanawake hata chama kinaimarika zaidi kwani wanachangia kwa kiasi kikubwa,’’ anasema.
FAMILIA/NDUGU WA KARIBU
Rashid Ali Hamad ambae ni mume wa mwakilishi huyo anasema alimuona mke wake ana ndoto za kufika mbali ndio maana akamuunga mkono na kumuhamasisha ili kufikia malengo yake.
‘’Tangu zamani mke wangu hakujipweteka, alianza na uongozi wa kwenye tawi kwa nafasi ndogo ndogo, hivyo nilijua kuwa na kwenye nafasi ya uwakilishi ataweza kuongoza,’’ anaeleza.
Anasema, anajivunia sana kuwa na mke asiekata tamaa katika mambo ya kimaendeleo, ambapo kwa sasa anasimamia jimbo kwa kipindi cha pili.
WANANCHI
Wanasema, wapo tayari majimbo yote yachukuliwe na wanawake kutokana na utendaji wao wa kazi pamoja na kuwatatulia shida zao.
"Kwa vyovyote vile mwanamke ana huruma, hivyo wanajitahidi kutekeleza zile ahadi walizozichukua kwa vitendo, hilo limetufanya tuwapende," wanaeleza wananchi hao.
Hassan Salim Ali mkaazi wa Kizimbani Wete anasema, wawakilishi wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia jamii kuwa na maendeleo, hivyo ni muhimu kuwepo hata katika majimbo yote.
"Mimi naona tulichelewa sana kutambua hili, lakini tungejua mapema naona majimbo yote tungechukua sisi, mwakilishi wetu anajitutumua kweli kweli kutatua matatizo yetu, anahitaji pongezi," anasema mwananchi Bahati Ame mkaazi wa Bopwe.
Wingi wa wanawake waliopo nchini haujawawezesha usawa wa jinsia katika nafasi za uongozi zinazotokana na uchaguzi ili kufikia 50 kwa 50.
Kwani mwaka 2020 wanawake walioingia katika Baraza la Wawakilishi ni 29 kati ya 75 ya wawakilishi wote huku wanaume wakiwa 46.
Ambapo wanawake waliogombea ni 61 na walioshinda ni nane (8), huku wanaume waliogombea wakiwa 190 na walioshinda ni 42
Kwa mujibu wa Tume ya uchaguzi Zanzibar, wanawake walioingia Baraza la Wawakilishi mwaka 2015 ni 28 sawa na asilimia 36, kati ya wawakilishi wote 84.
Kutokana na idadi hiyo inaonesha dhahiri kwamba elimu imewafikia ipasavyo wanajamii na wanawake katika ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na ndio maana idadi inaongezeka.
Kwa kutambua umuhimu wa mwanamke, sera na sheria mbali mbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake kushiriki katika demokrasia na uongozi.
Kifungu cha 21 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 64 kimeeleza kwamba, kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu mwanamke na taifa lake.
Katiba ya Zanzibar mwaka 1964 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 imeeleza wazi katika kifungu nambari 67 (1) kuwa, kutakuwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanawake kwa idadi ya asilimia 40 ya wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo.
MWISHO
Comments
Post a Comment