BY MUNIRA KAONEKA, ZANZIBAR@@@@
Katika
jitihada za kuimarisha uhifadhi wa mikoko na matumizi endelevu ya rasilimali za
asili, Jumuiya ya Community Forests Pemba (CFP) imefungua mafunzo maalum kwa
Watoa Mafunzo ya Jamii (ToTs) kuhusu uhifadhi wa mikoko na usimamizi wa
rasilimali za jamii. Mafunzo haya, yalifanyika kuanzia tarehe 19 hadi 21
Februari katika ofisi za CFP Unguja, na yalilenga kuwawezesha washiriki kuwa
viongozi wa uhifadhi wa mazingira katika jamii zao.
Mafunzo
haya yameandaliwa ili kuongeza uelewa wa washiriki kuhusu umuhimu wa mikoko,
mbinu za kuhifadhi misitu, na namna ya kushiriki katika usimamizi wa rasilimali
za asili kwa njia endelevu. Kupitia mafunzo haya, ToTs watapata ujuzi wa
vitendo na mbinu za kufundisha ambazo zitawawezesha kuwa mabalozi wa mabadiliko
katika maeneo yao.
Akifungua
rasmi mafunzo haya, Mkurugenzi Mtendaji wa CFP alisisitiza kuwa uhifadhi wa
mikoko ni jukumu la jamii nzima. “Uhifadhi wa mikoko na urejeshwaji wake ni
kazi ya pamoja, na ni muhimu kwa maendeleo endelevu. Tunapaswa kuwa mabalozi wa
kulinda rasilimali hizi ” alisema. Pia, aliishukuru jamii kwa kujitolea na
kushiriki katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.
Mafunzo
haya yalihusisha jumla ya washiriki 35, wakiwemo wanaume wanne (4) na wanawake
31, huku wanawake wakipewa kipaumbele kwa kuwa mara nyingi wao ndio waathirika
wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi lakini hawashirikishwi ipasavyo katika
maamuzi. Washiriki walitoka katika maeneo ya Unguja Ukuu (17) na Uzi (18).
Walichaguliwa kwa ujuzi wao na namna wanavyojitolea kwenye utunzaji wa mikoko,
wakiwemo wanachama wa kikundi cha uhifadhi wa mikoko cha Unguja Ukuu, Mikoko
ni Urithi Wetu.
Mafunzo
haya yaliendeshwa na maafisa wa CFP waliobobea katika uhifadhi wa mikoko,
wakiwemo Khadija Abdulrahman Hamdu (Afisa wa Mikoko) na John Ngonyani (Afisa wa
CoFMA). Washiriki walipata elimu kuhusu:Umuhimu wa mikoko katika mazingira na
jamii, Mbinu za uhifadhi na urejeshwaji wa misitu ya mikoko, matumizi endelevu
ya rasilimali za mikoko na changamoto zinazokumba uhifadhi wa mikoko na jinsi
ya kuzitatua.
Kwa mujibu
wa Afisa wa Mikoko kutoka CFP Khadija Hamdu, “Mafunzo haya yatasaidia katika
kuengeza ujuzi na uelewa wa wanajamii katika masuala ya mikoko. Pia yatasaidia
katika kupunguza athari zitokanazo na uharibifu wa mikoko.”
Baada ya
vipindi vya darasani, washiriki watafanya ziara ya mafunzo kwenye misitu ya
mikokoi ili kujifunza kwa vitendo mbinu bora za uhifadhi wa mikoko.
“Mafunzo yalikua mazuri na
tumejifunza mengi na sasa nina ujasiri wa kufanya yale niliyohitaji kufanya
(kwenye utunzaji wa mikoko)”alisemaBi.Rukia Haji Hamisi, mvuvi na mkulima kutoka Uzi
Baada ya mafunzo haya, washiriki wanatarajiwa kuwa viongozi
wa uhifadhi wa mikoko katika jamii zao kwa kuelimisha wanajamii kuhusu faida za
uhifadhi wa mikoko na jinsi inavyoweza kuwanufaisha kiuchumi, kushiriki katika
urejeshwaji wa mikoko kwa kupanda miche mipya, na kuhamasisha ushiriki wa
wanawake katika uhifadhi wa misitu kupitia nafasi za uongozi.
Comments
Post a Comment