IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
KATIBU Mtendaji Baraza la Vijana Zanzibar Salum
Issa Ameir amesema, wataendelea kuwaunga mkono vijana ili waweze kujiajiri na
kujipatia kipato kitakachowakwamua kiuchumi.
Alisema kuwa, Baraza la Vijana limeandaa utaratibu
wa kuwasaidia vijana kwa kuwapatia nyenzo muhimu za kuwawezesha kufanya kazi
kwa lengo la kutengeneza ajira ili wajikwamue kiuchumi.
Alisema hayo wakati akikabidhi vifaa kwa vijana
wajasiriamali ambao wamejiajiri, katika ofisi ya Wizara ya habari Gombani Chake
Chake Pemba.
Alieleza kuwa, dhamira yao ni kumsaidia Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika
kutekeleza ahadi yake kwa wananchi kuwapatia ajira laki tatu, hivyo kupitia
uwezeshwaji huo wa vijana kutawasaidia kujiajiri wenyewe na kuacha kutegemea
ajira Serikalini.
"Zaidi ya shilingi milioni 12,400,000
wamekabidhiwa vijana wa Wilaya zote kwa kupatiwa vifaa kwebye vikundi mbali
mbali, ikiwemo ushonaji ambao walipatiwa vyarahani, kilimo wamepatiwa mabati na
uchumi wa buluu," alisema
Aidha Katibu huyo aliwataka vijana hao kuvitumia
vifaa hivyo kwa lengo lilikusudiwa na kushirikiana pamoja ili viwasaidie
kuzalisha zaidi sambamba na kuwa tayari kuwapokea vijana wengine ambao
watatamani kujiunga na vikundi hivyo.
Mapema Mratibu Baraza la Vijana Pemba Hafidh
Rajab Khamis alisema, kupitia Baraza hilo wana mipango mikakati ambayo
inayowaongoza na kuwasaidia vijana katika ngazi mbali mbali kwa kadri
rasilimali zitakapo patikana, ili vijana wajikwamue kimaisha.
"Tutajitahidi kuwasaidia vijana kwenye vikundi
mbali mbali kwa kuwapatia vifaa vya kutendea kazi ili viwasaidie kuzalisha na
wapate fedha za kuendesha maisha yao," alieleza Mratibu huyo.
Kwa upande wao vijana waliokabidhiwa vifaa hivyo
wameishukuru Serikali kwa kuwasaidia vifaa ambavyo vitawasaidia
kuwajiri na kuboresha shughuli zao za ujasiriamali.
"Kwa kweli tumefarajika sana kupata vifaa
hivi, kwa sasa tumetatua baadhi ya changamoto ya ukosefu wa vifaa, tutavitunza
ili vidumu kwa muda mrefu," alieleza.
Katibu wa kikundi cha Maisha Vijana Seif Mohamed
Seif alieleza kuwa, kupitia vifaa hivyo walivyopewa vitasaidia kuwakwamua zaidi
na kuongeza juhudi katika uzalishaji ili kupata mafanikio zaidi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment