NA
ZUHURA JUMA, PEMBA@@@@
WANAJAMII
wametakiwa kuwa makini katika suala la kutoa ushahidi mahakamani, kwani ndio
unaoweza kumtia hatiani mshitakiwa au kumuachia huru.
Azungumza na wananchi wa Daya shehia
ya Mtambwe Kusini, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Wete Maulid Hamad Ali alisema,
ushahidi ni kitu muhimu katika kesi, hivyo kuna haja ya kutoa ushahidi kwa kina
pale unapohitajika.
Alisema kuwa, kuna makosa mbali mbali
yanayotendeka katika jamii ikiwemo ya udhalilishaji, wizi na madawa ya kulevya,
hivyo wasipokuwa makini katika kutoa ushahidi, washtakiwa wataendelea kuachiwa
huru huku wanajamii wataendelea kulalamika.
‘’Ushahidi ndo ambao utamtia
mshtakiwa hatiani au kuachiwa huru, kwa sababu unaangaliwa uzito wa ushahidi,
hivyo tuwe makini tunapokwenda mahakamani kutoa ushahidi,’’ alisema Hakimu
huyo.
Aidha aliwataka vijana kuacha kutumia
madawa ya kulevya kwani yanasababisha kujiingiza katika mambo maovu ikiwemo
kuiba na hatima yake kuishia chuo cha mafunzo.
Alisema kuwa, vijana wanapaswa kujielewa na kujitambua, ili waepukane na mambo yatakayowapeleka pabaya na badala yake wajishughulishe na vitu ambavyo vitawaletea maendeleo yao na taifa.
Kwa upande wake Mratibu kutoka Jumuiya
ya Wasaidizi wa Sheria Wilaya ya Wete (WEPO) Rashid Hassan Mshamata aliwataka
wazazi kukaa karibu na watoto wao na kuwafuatilia nyenendo zao ili
watakapofikwa na matatizo waweze kutambua haraka.
‘’Udhalilishaji upo wa aina nyingi,
hivyo endapo pia mnawakaripia watoto pia ni udhalilishaji na hasara yake ni kwamba
hata afanyiwe ukatili popote hawezi kukwambia, tuishi nao kirafiki,’’ alieleza.
Akijibu suali la mmoja wa washiriki
wa mkutano huo kuhusu suala la mashoga kutochukuliwa hatua, Mratibu huyo alieleza
kuwa ni vyema wanajamii wapeleke taarifa kunakohusika na kuwa tayari kutoa
ushahidi, kwani ipo sheria inayoruhusu kustakiwa na kutiwa hatiani.
‘’Tatizo lenu nyinyi, wafanyaji na
wafanywaji mnawajua lakini mnakaa kimya, baadae mlailamu Serikali kwamba
haichukui hatua, je mmewapeleka kwenye vyombo vya sheria wakaachiwa?,’’
alieleza.
Nae Msaidizi wa sheria Said Rashid
Hassan akijibu swali katika kutano huo alisema, mwanamke nae anaweza kutiwa
hatiani ikiwa amepatika na kosa la kuruhusu, kusaidia ama kushawishi kubakwa
kwa mtoto wa kike au hata kuazima sehemu ambayo litafanyika jambo hilo.
Mapema washiriki wa mkutano huo
walisema kuwa, kuna haja ya kuwakamata wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na
kuwashitaki kwani ndio wanaopelekea kuwaharibu watoto wengine katika jamii.
‘’Kwa kweli hao wanaofanya mapenzi ya
jinsia moja wanaharibu jamii nzima, wanahitaji kufungwa maisha yao, hapa
tutakuwa tumewasaidia watoto wasilawitiwe,’’ alisema Sid Mohamed Hamad mkaazi
wa Daya.
Mwananchi Silima Othman Haji wa
shehia hiyo aliiomba Serikali kudhibiti madawa ya kulevya yasiingie nchini, ili
jamii iwe na maendeleo na kupata taifa lenye vijana imara na wachapa kazi.
MWISHO.
Comments
Post a Comment