KATIBU Mkuu Wizara ya
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee Wazee na Watoto, bi Abeida Rashid Abdallah
amewataka walezi wa watoto na wahudumu wa wazee kujifunza mbinu mpya kupitia
mitandao ya kijamii ili kuboresha huduma wanazozitoa.
Ameyasema hayo wakati akifungua
mafunzo ya kuwajengea uwezo walezi wa watoto Mazizini, wahudumu wa wazee Welezo
na Sebleni yaliyofanyika katika ukumbi wa Wazee Sebleni Mkoa wa Mjini Magharibi
Unguja.
Bi Abeida amesema endapo
watajifunza mbinu za malezi kupitia teknelojia kutarahisisha utekelezaji wa
majukumu yao na kukuza ubunifu kwa makundi wanayoyahudumia pamoja na kusaidia kutoa huduma bora zitakazoimarisha
maendeleo ya Wizara na nchi kiujumla.
Amewataka wahudumu wa
makundi hayo kuongeza nguvu ya ziada kwenye huduma sambamba na kutanguliza
imani ya dini zao kwa lengo la kupata malipo hapa duniani na mbele ya Mola wao.
Sambamba na hayo
amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha anatoa huduma bora zinazostahiki
kwenye makundi hayo kwa muda muafaka.
Naye Mkurugenzi Idara ya
Ustawi wa Jamii na Wazee bwana Hassan Ibrahim Suleiman, amesema pamoja na kazi
nzuri wanazozifanya wahudumu hao Wizara imeona umuhimu wa kutoa mafunzo ili
kuwaongezea ujuzi mpya katika kazi.
Aidha amewataka
kutoridhika na elimu walizokuwa nazo na kuacha kufanya kazi kimazoea na badala yake kuongeza ujuzi mpya kupitia fursa
mbali mbali za mafunzo wanazozipata.
Mapema Mkurugenzi Idara
ya Uendeshaji na Utumishi Dkt. Salum Khamis Rashid, amesema Mafunzo hayo
yamekusudia kuwaonyesha mipaka ya kazi zao na kuwajenga uwezo ili kutoa huduma
nzuri katika kazi.
Kwa upande wa
muwasilishaji mada wa mafunzo hayo,
Bi Amina Abdulkadir Ali na bi Rahma Ali
Khamis, wamesema kwa kutambua umuhimu wa makundi hayo Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imekua na mazingatio ya sheria, mikataba ya Kitaifa na Kimataifa ili
kutambua haki za watoto na wazee hapa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya
washiriki wa mkutano huo ndugu Arafa Thiney Nasibu amesema, mafunzo hayo
yataboresha utendaji wa kazi zao kwa mazingatio makubwa sambamba na
kuwaelimisha wengine wanaohusika na malezi ya watoto na wazee.
Comments
Post a Comment