IMEAKWANA ZUHURA JUMA, PEMBA
MKAGUZI wa shehia ya Pandani Wilaya ya Wete, Inspekta wa Jeshi la
Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Khalfan Ali Ussi ameutaka uongozi wa kampuni ya
ujenzi wa barabara ya MECCO kuchukua tahadhari juu ya vitendo vya uhalifu
vinavyoweza kutokea na kuhakikisha vifaa vyao vinakuwa salama.
Alisema kuwa, licha ya kuwepo kwa hali ya usalama katika eneo hilo
la ofisi yao lakini hawapaswi kuacha kuchukua tahadhari juu ya uwezekano wa
kutokea vitendo vya kihalifu, ili vifaa vyao vibaki salama na waweze kutekeleza
majukumu yao vizuri.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua eneo la ofisi hiyo
katika shehia ya Pandani ikiwa ni muendelezo wa kudhibiti uhalifu kwenye maeneo
mbali mbali, Inspekta huyo alisema, atahakikisha anadhibiti uhalifu na kila
mwanajamii anakuwa mlinzi kwa mwenzake.
"Walinzi wawe makini kuhakikisha mali zote zinakuwa salama na
iwapo kutatokea uhalifu basi msisite kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi,
lakini pia ikibainika kuna uzembe waliousababisha basi ni lazima watawajibishwa
kwa mujibu wa Sheria, hivyo mnapaswa kuwa makini na hilo," alisema.
Aidha aliishauri kampuni hiyo kuishi vizuri na jamii
iliyowazunguka, ili waheshimu na kulinda mali za kampuni hiyo ambazo zinatumika
katika kuharakisha maendeleo ya uchumi wa nchi.
"Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dk. Hussein
Ali Mwinyi imewekeza fedha nyingi kuilipa kampuni hiyo kwa ajili ya ujenzi wa
barabara Kongwe ya Wete, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kutoa ushirikiano ili
kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanakuwepo, kwani barabara ni moja ya
kichocheo cha kukuza uchumi," alisema Mkaguzi huyo.
Mapema Meneja wa ofisi hiyo Mohamed Rashid Khamis alisema, kwa
sasa hakuna changamoto yeyote ya kihalifu iliyojitikeza na wanashirikiana na
wanajamii katika mambo mbali mbali, jambo ambalo linawapa faraja ya kufanya
kazi vizuri.
Alisema kuwa, wananchi wa eneo hilo wanachukia sana uhalifu, jambo ambalo limesaidia kuweka hali ya usalama katika maeneo yao huku kila mwanajamii akionekana kama ni askari wa ulinzi shirikishi.
Akitoa shukran kwa niaba ya wafanyakazi wengine Afisa Utumishi
kutoka kampuni hiyo Saumu Khatib Hamad alisema, utaratibu alionao Mkaguzi huyo
wa kusikiliza kero za kiusalama katika jamii ni za kuigwa kwani inasaidia
kudhibiti uhalifu.
MWISHO.
Comments
Post a Comment