NA MOZA SHAABAN, ZU@@@@
KILA siku mwanadamu amekuwa
akihangaikia afya yake na ustawi wake.
Kwa
karne zilizopita, mwanadamu alitumia mimea, mboga mboga na wanyama, ili kuponya
magonjwa na maradhi mbali mbali yaliokua yakimsibu.
Kwa
vile wakati haugandi, sayansi inayochunguza faida na athari za vitu vya
kemikali, kwa matibabu au kuzuia magonjwa, kupunguza maumivu na nyenginezo ilizuka.
Na
hapa dawa mbali mbali ambazo ni muhimu kwa matumizi ya binaadamu, zilianza
kutengenezwa hususan zile za kemikali, ili kurekebisha au kuboresha hali ya afya
ya mtu.
DAWA NI NINI ?
Dawa
za binaadamu ni kitu chochote, ambacho binaadamu anatumia kwa lengo la kutibu
au kukinga maradhi yasishambulie kinga za mwili.
Zinaweza
kuwa katika aina tofauti, kama vile vidonge, sindano, matone, creams au loshan
pamoja na za unga unga.
Kwa
mfano, dawa za antibiotics hutumiwa kutibu maambukizi ya bakteria, za antiviras
hutumiwa kutibu maambukizi ya virusi, na dawa za analgesic hutumiwa kupunguza
maumivu.
Kitaalamu
dawa haziliwi tu kama njugu, bali kuna matumizi sahihi ambayo mugonja,
anatakiwa kuyajua, na sio rahisi kujua bila kupata maelekezo kutoka mtaalamu wa
afya.
Kwa lugha nyepesi, Ili dawa ifanye kazi
mwilini, ina kiwango maalumu (dozi) na muda wa matumizi yake, iliyoandikiwa
mgonjwa kutumia baada ya daktari kuthibitisha ugonjwa uliopo.
Lakini
kwa sababu moja au nyingine wapo watu hutumia dawa bila maelekezo ya daktari, na hili limekua
kama jambo la kawaida tu,kwani watu
wengi humeza dawa bila kuzingatia vipimo.
JE JAMII INAMTAZAMO GANI ?
Hamdu
Hassan Bakari (65) wa Mjimbini, anasema udhibiti mdogo wa dawa, ni miongoni mwa
sababu zinazo pelekea watu kutumia dawa bila maelekezo ya daktari.
Anasema
hakuna udhibiti wa kutosha juu ya upatikanaji wa dawa, na kwa sasa mtu
anapojisikia kuumwa, hubisha hodi kwenye maduka ya kuuzia dawa na kununua
atakayo.
‘’Baadhi
ya maduka ya vyakula yanajihusisha na uuzaji wa dawa kama za antibayotiki
(panadoli), ambapo wao hawana usajili rasmi wa kufanya biashara hiyo,’’anaeleza.
Abdull-hamid
Shaabani Haji mkaazi wa Vitongoji Chake chake Pemba anasema, kutokumudu gharama za matibabu, ni
moja kati sababu zinazo pelekea, watu wengi kutumia dawa bila kupata maelekezo ya daktari.
Rehema
Mohamed Makame (45), mkaazi wa Mtambile Mkoani, anaeleza kuwa, usumbufu
wanaopata wagonjwa katika baadhi ya hospitali na vituo vya afya, unapelekea
watu kutofika hospitalini, ili kueleza magonjwa yanayowasibu, na kasha
kujikadiria dawa.
‘’Utamaduni mbovu wa kila mgonjwa kujikadiria
dawa, umekuwa ukiathiri kinga za mwili, na kusababisha baadhi ya wakati, dawa
nyingine kutofanyakazi mwilini,’’anaeleza.
Hata
Sada Mohamed Amour, wa Mjimbini anafafanua kuwa, waliowengi wamekuwa wakitumia dawa kiholela
kwa kule kutokujua madhara ndani ya miili yao.
‘’Watu
wengi hawana uwelewa wa kutosha kuhusu madhara yanayoweza kujitokeza, iwapo
watatumia dawa kiholela bila yakupata maelekezo kutoka kwa wahudumu wa afya,’’anaeleza.
WATAALAMU WA AFYA YA BINADAMU
WANASEMAJE?
Rashid
Suleiman Ali ambae ni Afisa tabibu kutoka kituo cha afya Kangani Mkoani nasema,
athari moja wapo anayoweza kuipata mtu, anaetumia dawa kiholela ni kusababisha
usugu wa dawa mwilini mwake ‘Resistance of Drugs’ hapo baadae.
Yussuf
Omar Masoud daktari kutoka kituo cha
afya Kangani anafafanua kuwa, utumiaji dawa kiholela uaweza kusababisha madhara
ya muda mrefu, ikiwemo viungo kupoteza nguvu
‘’Kwa
mfano, matumizi ya dawa za usingizi ‘sleeping pills’ ukivitumia bila
kufuata maelekezo ya mtaalamu, mwisho wa siku, unaweza kupata ulemavu
usiotarajiwa,’’anafafanua.
Nae
Maryam Said Abdallah Mfamasia kutoka kituo cha afya cha Buguruni Dar-es-salaam anasema,
kutumia dawa bila kufuata maelekezo ya daktari kunaweza kusababisha kuongeza
sumu mwilini.
Kwani
anabainisha kuwa, dawa hutengenezwa kwa kutumia chembe chembe za kemikali, ambazo
kimsingi ni sumu zinazoua vimelea vya ugonjwa, ingawa kwa utaratibu maalum
kutoka kwa mtaalamu.
‘’Dawa
ni sumu, iliyotengenezwa maalum kwa ajili ya kuua vimelea vya maradhi, ingawa
ukiitumia kiholela, inaua hata mtu mwenyewe kwa kule kukosa mpangilio wa
kitaalamu,’’anafafanua.
BARAZA LA FAMASIA LINASEMAJE?
Elizabeth
Shekalage ambae ni Msajili wa Baraza la Famasia nchini , anaeleza kuwa, madhara
ya kutumia dawa kiholela ni pamoja na kuleta ulemavu wa kudumu na hata kusababisha
kifo.
Kwani
ili dawa ifanyekazi mwilini, inakiwango maalumu (dozi) na muda wa matumizi wa
dawa, aliyoandikiwa mgonjwa, kutumia baada ya daktari kuthibitisha ugonjwa
uliopo.
Aidha
mtaalamu huyo, anasema kuwa, kwa dozi ikiwa kubwa, kunasababisha kuongeza
kiwango cha dawa, ambacho hakitakiwi kwenye mwili na huleta madhara ya figo,
ulemavu na hata kifo.
MITANDAO YA KIJAMII
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha
kua, ipo hatari ya idadi kubwa zaidi ya watu kupoteza maisha, kutokana na usugu
wa vimelea vya magonjwa aliyetumia dawa holela.
WHO kwenye utafiti wake wa mwaka 2019,
limekugundua kuwa, magonjwa sugu dhidi ya dawa, husababisha vifo laki 7 duniani
kote kila mwaka.
Ambapo
kwa idadi ya vifo hivyo, ni sawa na wastani wa vifo 58,333 kwa mwezi, sawa na vifo
1,944 kwa siku, huku WHO, likiendelea kutahadharisha juu ya ulaji wa dawa
kiholela.
Aidha WHO, limeonya kuwa, ikiwa mikakati
haitochukuliwa ya kudhibiti watu kujilia dawa ovyo, huwenda ifikapo mwaka 2050,
watu milioni 10, ikawa wanapoteza uhai kila mwaka duniani kote.
NINI KIFANYIKE?
Hemed
Nassor Mbarouk mkaazi wa Mjimbini Mkoani, anasema ni vyema kwa wizara ya Afya
Zanzibar, kutoa elimu kwa wananchi, juu ya athari za matumizi ya dawa kiholela.
Ali Mohamed Makame mkaazi wa Mtambile, anashauri
ni vyema kwa wataalamu wa afya, kuimarisha huduma za afya vituoni na hospitalini
ili kupunguza tatizo hilo.
Salama
Omar Ali mkaazi wa Mchanga mdogo, anashauri kuwa, wizara ya afya Zanzibar, idhibiti
uuzwaji dawa kiholela madukani, ili kuhakikisha matumizi ya dawa yanakuwa
sahihi kwa mgonjwa.
Rashid
Suleiman Ali Afisa tabibu wa kituo cha afya Kangani alisema, ni vyema kwa
wagonjwa kufika katika vituo vya afya, ili kupata vipimo na maelekezo sahihi ya
madaktari namna ya utumiaji wa dawa.
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Tanzania bara Dk.
Seif Shekalage alisema, ili kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza, ni vyema
kwa wamiliki wa maduka ya dawa, wafuate utaratibu sahihi wa utowaji wa dawa kwa
wagonjwa.
Afisa
Mdhamini wizara ya Afya Pemba, Khamis Bilali Ali, anasema ni kosa la kitabibu
mgonjwa kujikadiria dawa mwenyewe.
‘’Chakufanya
ili kudhibiti hali hiyo, hata wauzaji dawa katika maduka yanayotambulika,
wasitowe dawa pasi na buku la mtaalamu wa afya alivyoelekeza,’’anaushauri.
MWISHO
Comments
Post a Comment