|
KUANZIA mwaka 1983 hadi 1992, hatua mbali mbali
zilichukuliwa, ikiwani pamoja na maamuzi ya mwisho ya Umoja wa Mataifa, kuitangaza
Disemba 3 ya kila mwaka, kuwa siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu.
Siku hiyo, pamoja na mambo
mengine, kundi la watu wenye ulemavu hujadili, mafanikio na changamoto zao,
zikiwemo za huduma za afya.
Kisha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliunda
Mkakati wa Kitaifa wa Ujumuishi wa mwaka 2010 hadi 2015, na sera ya taifa ya watu
wenye ulemavu ya mwaka 2004, ukitaja ulazima wa huduma za afya kwa watu wenye
ulemavu.
Ipo sera ya kitaifa ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2018
kwa upande wa Zanzibar, ambayo Ibara ya 20, inasisitiza uimarishwaji wa
upatikanaji huduma bora na endelevu kwa kundi hilo.
Serikali ilitunga sheria ya Watu wenye Ulemavu ya mwaka
2010, ambapo ilikuja kuharakisha huduma bora na endelevu za afya kwao.
Kwa Zanzibar, ilikuwa na sheria ya watu wenye ulemavu, nambari
9 ya mwaka 2006, ambayo imefutwa na sasa kuwa na sheria mpya nambari 8 ya mwaka
2022.
Kifungu cha 28 (1) (c) cha
sheria hiyo, kimeainisha haki ya kupata huduma na elimu ya afya, kwa watu wenye
ulemavu, ikiwemo matibabu, matengenezo au marekebisho yanayohusiana na aina ya
ulemavu wao.
Kulikuwa na Mpango Mkakati wa sekta ya afya wa miaka
tisa, ambao uliishia mwaka 2019, nao ulitaja hatua za kuchukuliwa, ili
kuwakinga na utapiamlo wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
Kimataifa upo Mkataba wa haki za watu wenye ulemavu,
ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliusaini mwaka 2007, na
kuthibithisha mwaka 2009, ambao unalazimisha huduma za afya, kwa watu wenye
ulemavu.
Ibara ya 25, inasisitiza nchi wanawachama,
zitumbue kuwa, watu wenye ulemavu, wanayo haki ya
kunufaika kwa kiwango cha juu, cha huduma na elimu ya afya.
‘’Nchi wanachama zitatoa huduma za afya,
zinazohitajika kwa watu wenye ulemavu, hasa kutokana na aina ya ulemavu wao, yakiwemo
maeneo ya vijijini,’’umefafanua Mkataba huo.
Ukaongeza
kuwa, nchi hizo zitawataka wataalamu wa afya, kutoa huduma za kiwango sawa, kwa
watu wenye ulemavu, kama wengine.
HALI IKOJE KWA
VIZIWI NA ELIMU YA AFYA YA UZAZI?
Omar Haji Omar wa Mtambile wilaya
ya Mkoani mwenye watoto sita, akizungumza na wandishi wa makala hii, chini ya mkalimani
wake, anasema hajapata elimu ya afya ya uzazi kwa aina ya miundombinu yake.
‘’Mimi nishahudhuria kliniki
mara tatu, lakini sijawahi kupata elimu ya afya uzazi, hasa kwa aina yangu ya
ulemavu,’’anasema.
Khamis Massoud Khamis mwenye watoto wawili,
mkaazi wa Kilamatinde anasema, hata yeye na mke wake wameshahudhuria klikini
mara mbili, lakini hawapati elimu ya afya ya uzazi.
‘’Mara ya kwanza nilipokwenda
tunawasiliana na daktari kwa njia ya maandishi, mpaka nikifahamu, lakini kwa
kutumia mkalimani sijawahi,’’anasema.
Mkewake Khamisi, Aisha Muhidin
Kombo, anasema njia anayotumia kupata elimu ya afya ya uzazi ni kujisomea
vipeperushi, lakini sio kupitia madaktari.
‘’Ni kweli mimi nimezaa mtoto
kila baada ya miaka mitatu, lakini elimu hii ni ya mazoea tu, sio kama
nimefundishwa na madaktari,’’anasema.
Fatma Juma Mohamed (50) mwenye
watoto 10, mkaazi wa Mchanga mdogo Wete, anasema mimba moja baada ya kuonekana
na tatizo, alikwenda hospitali na mkalimani.
Maimuna Issa Haji na mwenzake
Husna Kombo Omar wa Micheweni wanasema, wanapokwenda kliniki, hakuna mkalimani wa
lugha ya alama na kukosa taarifa sahihi.
‘’Natamani hasa nipate elimu
ya afya ya uzazi kwa kina, ili nijue mambo kadhaa, lakini inakuwa vigumu maana,
wale ni wataalamu wa afya tu, sio wa lugha ya alama,’’anasema.
Mkalimani wa lugha ya alama
Pemba Asha Suleiman, anasema hajawahi kualikwa na wizara ya Afya, ili kuwa
makalimani wakati elimu ya afya uzazi ikisomeshwa.
Mwenyeikiti wa Chama cha
Viziwi wilaya ya Chake chake Mohamed Khamis Shehe, anasema hakuna hata mkutano
mmoja wao peke yao, waliowahi kualikwa wa utoaji elimu ya afya ya uzazi.
Mjumbe wa Umoja wa Watu wenye
Ulemavu Zanzibar, Hidaya Mjaka Ali, anakiri kuwa, elimu ya afya ya uzazi bado
ni changamoto kwao.
‘’Ni kweli wizara ya Afya,
imeyafikia makundi yote, lakini kwa wenzetu wenye uziwi kwa mkutano wao peke
yao, hilo halijafanyika,’’anasema.
Mratibu wa Baraza la Taifa la
watu wenye Ulemavu Zanzibar ofisi ya Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, anakiri kuwa
wizara ya Afya, haijawahi kuliita kundi la watu wenye uziwi, kuwapa elimu hiyo.
‘’Mbinu tunayoitumia kwa watu
wenye uziwi, ili wafikiwe na elimu ya afya ya uzazi, ni kuwatumia maafisa wa
Baraza, ambao wameshapata elimu na kukutana na viziwi,’’anasema.
Changamoto inayojitokeza kuwa
ni uwepo wa viziwi zaidi ya 400 kisiwani Pemba, ingawa yupo mkalimani mmoja
anayetambulika rasmi.
Muhudumu wa afya shehiani Kisiwani
panza, ‘CHV’ Haroub Makame Bakar, anasema kwao ni changamoto kuwafikishia elimu
viziwi, kutokana na wao, kukosa mafunzo ya lugha ya alama.
‘’Sisi ‘CHV’ tupo watano
kwenye shehia hii, lakini hakuna hata mmoja ambae anaelimu, japo ndogo ya lugha
ya alama, inakuwa vigumu kuwasiliana nao,’’anasema.
WIZARA YA AFYA INASEMAJE?
Afisa Mdhamini wizara ya Afya
Pemba Khamis Bilali Ali, anasema anapotokezea mjamzito mwenye uziwi,
huwasiliana na mamlaka husika, kwa ajili ya kupatiwa mkalimani.
‘’Ni kweli wataalamu wetu wa afya
hawana utaalamu wa ukalimani, lakini akitokezea mjamzito na mwenzawake
wanahitaji ukalimani, tunawasiliana na wenzetu katika hilo,’’anasema.
Eneo jingine, anasema wapo
wajawazito ambao ni viziwi, lakini panakokua na shida ya kupata elimu zaidi,
huhudhuria kliniki na waume zao.
‘’Wakati mwengine hufuatana na
ndugu au jamaa zao wanaoelewa lugha ya alama, ili madaktari wanapowasiliana,
iwe rahisi kupata majibu,’’anaeleza.
Anaona bado ipo fursa kwa wale
viongozi wa jumuia za watu wenye ulemavu, kuwasilisha maombi kwao, ikiwa
wanahitaji elimu ya afya uzazi, chini ya mkalimani wao.
Mtaalamu wa afya ya uzazi
kutoka hospitali ya Chake chake Rahila Salim Omar, anasema haki ya afya ya
uzazi ndio msingii wa kuwa na afya njema.
Anaona, bado baadhi ya
wanaume, wamekuwa wazito kuwasindikiza wenza wao, kuhudhuria kliniki, jambo
ambalo husababisha matatizo kadhaa wakati wa kujifungua.
NINI ATHARI YAKE?
Aisha Hussein Khamis, anasema
kama wao wataendelea kutengwa kwenye elimu ya afya uzazi, kunaweza kukalizwa
matatizo kadhaa, ikiwemo kifo kwa mama na mtoto.
Mwanajuma Majid Ibrahim,
anasema athari nyingine ni kukosekana kwa mfumo wa lihse husika kwa mjamzito,
kunakotishia kuzaliwa mtoto mwenye utapiamlo.
Mbarouk Juma Daudi wa Kengeja,
anasema athari nyingine ni kuongezeka kwa uzazi wa papokwa papo,
kunachochangiwa na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi.
Afisa Mdhamini wizara ya Afya
Khamis Bilali Ali, anasema moja ni kuongezekwa kwa wimbi la wanaojifungulia
majumbani.
Afisa wa Chama cha Viziwi
wilaya ya Chake chake Mohamed Khamis Shehe, anasema ni kuwaweka wao katika
msingi wa kukumbwa na magonjwa nyemelezi.
NINI KIFANYIKE?
Mratibu wa Baraza la Taifa la watu
wenye ulemavu Zanzibar ofisi ya Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, anasema ni wizara ya
Afya, kurudi kwa kundi la watu wenye ulemavu, ili kuliemisha kwa mujibu wa
miundombinu yao.
Mkalimani wa lugha ya alama
Asha Suleiman, anashauri vipindi na taarifa zote za kwenye tv zinapoendeshwa,
kuwepo kwa mkalimani.
Mzazi mweye kijana mwenye
uziwi, anasema ni kutekelezwa kwa sheria kama zilivyo, ili kundi hilo lipate
haki zao.
TAMWA ZANZIBAR INAFANYA NINI?
Chama cha Waandishi wa habari Wanawake
Tanzania TAMWA- Zanzibar na Tanzania bara wanashirikiana, katika kuendesha
mradi wa mwaka mmoja, wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuandika, habari
za afya ya uzazi.
Kwenye mafunzo yaliofanyika Pemba, Mratibu
wa mradi huo Zaina Abdalla Mzee, anasema tafiti zilionesha, kuna vipindi na
habari kidogo, katika vyombo vya habari, juu ya haki ya afya ya uzazi.
Mradi huu wa majaribio, ambao unafadhiliwa
na Shirika la Wellspring Philonthropic fund la Marekani, unaendeshwa katika
wilaya za Chake chake, Magharibi ‘B’ na Kati.
Moja ya shabaha kuu, ni kuhakikisha wanawake
na wasichana walioko mjini na vijijini, wanakuwa na elimu sahihi ya afya uzazi,
kupitia vyombo vya habari.
TAKWIMU
Wakati hayo yakifanyika, Wizara ya Afya
Zanzibar, imebainisha kuwa, katika kipindi cha mwezi Julai, 2022 hadi Machi,
2023, kuna vifo vya mama 46 na vya watoto wachanga chini ya siku saba 1,567
viliripotiwa.
Vifo hivyo ni sawa na kila wilaya moja ya
Zanzibar kati ya 11, kuwepo wa vifo vya mama watano, sawa na 142 nao kufariki
katika wilaya hizo, katika kipindi hicho.
Aidha mwaka huo huo, wapo wajawazito 52,891,
sawa 4,808 kutoka kila wilaya moja ya Zanzibar, waliohudhuria kliniki ya
upimaji mimba, angalau mara moja.
Kati yao, wajawazito 9,017 walihudhuria
kliniki wakiwa na ujauzito chini ya wiki 12, huku kukiripotiwa wajawazito 38,097,
Unguja 26,405 na Pemba 11,692 kujifungulia hospitali.
Mwisho
Comments
Post a Comment