ZANZIBAR
Na Nafda Hindi, ZANZIBAR @@@@
WANANCHI wa Shehia ya Kigongoni Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja walalamikia umbali wa masafa marefu kwa watoto wao wakifuata huduma ya Elimu.
wameiomba serikali kuwajengea skuli karibu na makaazi yao ili
Watoto wao wapate elimu ipasavyo na kuwaepusha na hali hatarishi.
Malalamiko hayo yamekuja kufuatia ziara ya kuibua
changamoto za wananchi iliyoandaliwa na Chama cha waandishi wa Habari wanawake
Tanzania TAMWA Zanzibar kupitia mradi wa kuwainua wanawake katika Uongozi,
Strengthen Women In Leadership (SWIL)
unaotekelezwa na chama hicho.
Wazazi wa watoto hao wamesema kwa sasa Watoto wanasoma skuli ya mbali ambayo wanatembea Zaidi ya saa moja hali
inayohatarisha usalama wao na wengine kushindwa kufika skuli kuendelea na masoma na kuishia
vichakani .
“Skuli iko mbali na sisi inabidi twende Fukuchani. Kidagoni au
Kidoti hali ambayo ina hatarisha usalama wa watoto wetu, na sisi wazazi huwa
hatuna Amani mpaka watoto warudi skuli,” Mwananchi, Shehia ya Kidagoni.
Mmoja wa wananchi hao Ali Simai Silima amesema
shehia hiyo ya kigongoni hakuna skuli na badala yake Watoto wa eneo hilo
wanakwenda kusoma skuli ya kidagoni ambayo ni mbali na shehia hiyo.
“Vijana wangu wanasoma maeneo ya mbali tumejenga banda la skuli
katika maeneo ya karibu lakini baadhi ya Viongozi wa chini wametwambia tuondoshe baadhi wanafunzi hasa
watoto wadogo wamekata kwenda skuli kabisa kutokana na masafa ya mbali,”
Mwananchi.
Aidha amesema Watoto wake kusoma kwa umbali huo anakosa amani
kutokana na dunia kukumbwa na matukio mengi ya kihalifu ikiwemo udhalilishaji.
“Mtoto akitoka kwenda skuli hafiki anakwama njiani,unaambiwa
wende ukachukuwe mwanao, tunawaambia Viongozi wetu wa Jimbo kama wanatutaka
mwakani tuwapigie kura walitazame suala hili kwa umakini, sisi wazee ndio
tunaoumia.
Nae Mwalimu Mkuu wa skuli
ya Maandalizi na Msingi kidagoni Machano Khamis Machano amesema zaidi ya
wanafunzi 30 wa skuli hiyo wanakosa masomo kwa siku kutokana na changamoto
mbalimbali ikiwemo masafa marefu ya maeneo wanakoishi.
“Suala hili kwa kweli linatuumiza kichwa wanafunzi wanatoka
majumbani kwao lakini hawafiki skuli, kuna kijiji kinaitwa Kijini Mbumbwi ni
sehemu ambayo iko mbali, watoto wengi wanatoka huko tena wadogo wa Nursery na
ni pori tupu, mwendo wa saa moja huko hakuna skuli kwa hiyo wanakosa haki yao
ya msingi ya kupata Elimu.” Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Kidagoni, Machano
Khamis Machano.
Alisema wanafunzi wa skuli hiyo wanatoka maeneo ya mbali
haliambayo inawasababisha kuwavunja moyo na kuwasababisha kuishia njiani.
Alisema wanafunzi wanaosoma katika skuli hiyo wanatoka shehia ya
kigongoni ,Bwereu na kidoti ambapo kutoka maeneo hayo hadi kufika skuli ni
Zaidi ya saa moja kutembea huku njia zenyewe zikiwa haziridhishi kwasababu
hatarishi.
Mwalimu wa skuli hiyo Zainab Silima Machano aliiomba serikali
kuwawekea miundombinu mizuri ambayo itasaidia kufika skuli hapo kwa wakati
kwasababu anatoka masafa marefu na akifika skuli huwa kashachoka na kusababisha
kushindwa kuvikosa baadhi ya vipindi hususani vya asubuhi.
“Tunatoka mbali na changamoto hamna usafiri, watoto wanachelewa na
pia wanakuwa watoro na kama kipindi chako ni cha kwanza hata ukifika skuli
kushakikosa kwa kuchelewa,” Mwalim wa Skuli ya Kidagoni Zainab Silima Machano.
Baadhi ya wanafunzi wa skuli hiyo walisema hali hiyo ya umbali wa
skuli inawaathiri hasa kwenye masomo yao ambapo muda mwingi wanautumia njiani
badala ya kusoma hivyo wameiomba serikali kuwajengea skuli ya karibu ili kupata
haki yao ya elimu bila ya usumbufu.
“Tukifika skuli tumechoka tokea kiwiliwili mpaka akili na masomo
mengi tunakosa kutokana na kutembea masafa marefu, hivyo tunaomba Serikali
itusaidie,” Mwanafunzi kutoka skuli ya Kidagoni.
Akizungumzia tatizo hilo Sheha wa shehia hiyo Vuai Mtosho
Bure alisema hatua aliochukua ni kushirikiana na wananchi wake kuanza
ujenzi wa skuli ya maandalizi katika maeneo hayo ya karibu ili kuwaondoshea
usumbufu watoto wadogo kufuata huduma hiyo katika masafa ya mbali.
“Naiomba Serikali kuu na wadau wengine wa maendeleo
kuwakamilishia ujenzi wa skuli yao kwani wamekwenda katika maeneo mbalimbali
ikiwemo uongozi wa Jimbo na halmashauri lakini bado hawajafanikiwa,” Sheha
Kidagoni, Vuai Mtosho Bure.
Mratibu wa mradi wa kuwainua wanawake katika uongozi SWIL kutoka
chama cha waandishi wa Habari wanawake Tanzania TAMWA Zanzibar Mariam Ame Chum
amesema lengo la ziara hiyo katika maeneo hayo ni kuibua changamoto
zinazoikabili jamii ili ziwe kufanyiwa kazi na wananchi waweze kupata huduma
bora ambazo ni haki yao ya msingi, ikiwemo elimu , mali na miundombinu ya
Barabara.
“Viongozi wa majimbo waliochaguliwa na wanachi watimize wajibu wao
ipasavyo kuwahudumia wananchi na kupata haki zao za kidemokrasia kwa kutatuwa
changamoto mbali mbali zinazowakabili kupitia majimbo yao,” Mariam Ame Choum.
Mratibu SWIL, TAMWA,ZNZ.
Tamwa Zanzibar inatekeleza mradi huo wa kuwainua wanawake katika
uongozi sambamba na kuibu changamoto za wananchi na kuwawezesha kupaza sauti
zao kwa kudai haki zao za msingi kwa kushirikiana na ZAFELA na PEGAO chini ya
ufadhili wa ubalozi wa Norway.
Comments
Post a Comment