NA MARYAM SALUM,PEMBA@@@@
VIONGOZI na wanachama wa vikundi vya kuweka na kukopa Pemba, wametakiwa kuondokana na woga na badala yake kuchukua mikopo kwa ajili ya kuendeleza biashara zao.
Akifungua mafunzo ya siku mbili juu ya ushirikishwaji kwa viongozi wa vikundi vya maendeleo katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya TAMWA Pemba, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa habari TAMWA, Fat-hiya Mussa Said
alisema kuwa lengo la mradi wa Kijaluba iSave Zanzibar ni kuwainua kiuchumi wanavikundi hasa watu wenye ulemavu.
Alisema kuwa fedha zilizopo kwenye Hisa zinatakiwa kukopwa kwa ajili ya kuendeleza biashara na sio kutazamwa tu.
"Mradi wa Kijaluba iSave Zanzibar unakusudia kuwatoa woga,ili kuona fedha zilizopo kwenye hisa munazichukua kwa mkopo kwa ajili ya kuboreshea biashara zenu kwa maendeleo zaidi," alisema mratibu huyo.
Alieleza kuwa fedha zilizopo zinatakiwa zitumiwe, na matumizi yenyewe ni kwa ajili ya kuendeleza na kuanzisha biashara nyengine za maendeleo.
Alisema Mradi wa Kijaluba iSave ni mradi unaolenga kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi,kuwajengea uwezo kuhusu maisha yao wenyewe na jamii zao.
"Lengo kuu ni kukuza uwezo wa watu wenye ulemavu kiuchumi kwa kujenga mitazamo chanya juu ya ushiriki wao, na kujiingiza katika shughuli za kujipatia kipato kupitia vikundi vya kuweka na kukopa ", alisema.
Alifahamisha kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa mashirikiano kati ya Shirikisho la Jumuia za watu wenye ulemavu Zanzibar (SHIJUWAZA) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania,(TAMWA Zanzibar) kwa ufadhili wa Chama cha watu wenye Ulemavu Nchini Norway (NAD).
Mratibu huyo aliwataka viongozi hao wa vikundi ambao wamepatiwa mafunzo hayo ya biashara kuhakikisha wanakuwa walimu kwa wenzao, ili kuona lengo linafikiwa.
Alieleza kuwa mradi huo unatekelezwa katika Wilaya mbili Unguja na Pemba,ambapo kwa Unguja ni wilaya ya Kusini na Wilaya ya Chake Chake Kusini Pemba.
Kwa upande wake Ofisa Muwezeshaji kutoka katika Mradi huo Muhidin Ramadhani Muhidin wakati akiwasilisha mada ya kuchagua,kupanga, usimamizi, kwa viongozi hao alisema kuwa Mradi unajukumu kubwa la
kuhakikisha wanawabadilisha wanavikundi kiuchumi.
"Mradi wa Kijaluba utahakikisha unawatoa hofu na woga viongozi na wanachama wao kwenye vikundi vya maendeleo ili kuona wanafika mbali kiuchumi " , alisema Afisa huyo.
Alieleza kuwa lengo la Mradi ni kuwawezesha wanavikundi hasa watu wenye ulemavu, ili wawe na uwezo wakuchagua zile biashara zitakazoleta faida.
Aidha aliwataka wanavikundi hao kuyafanyia kazi mafunzo waliyopatiwa na kuwa mabalozi kwa wanachama wa vikundi vyengine, ili kuhakikisha miradi itakayokuja kuanzishwa wanafuata mfumo wa biashara yenye tija
kwa nia ya kuondokana na umasikini.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka katika kikundi cha Jembe kazi kilichopo Ole kwa niaba ya wenzake alisema mafunzo hayo yatakuwa chachu yakuleta mabadiliko kutokana na shughuli zao wanazozifanya za
kujipatia kipato.
Jumla ya vikundi 43 vimebahatika kwenye Mradi huo ambapo Wilaya ya Kusini Unguja vipo vikundi 20 na Pemba 23, Mradi huo ni wa majaribio na unatekelezwa katika kipindi cha miaka miwili kutoka Novemba 2022 hadi Disemba 2024.
MWISHO.
Safi sana kijaluba
ReplyDelete