NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
WANANCHI wa kijiji cha Vikunguni
shehia ya Ng’ambwa wilaya ya Chake chake Pemba, wamekiri kupungua kidogo kwa vitendo
vya wizi wa mifungu na mazao, baada ya ulinzi shirikishi kuimarika shehiani
humo.
Walisema, ijapokuwa
bado wapo baadhi ya wananchi wamekuwa wakiidharau na kukebehi uwepo wa ulinzi
shirikishi, lakini vitendo vya wizi wa Ng’ombe na mazao umeanza kupungua kwa
kasi.
Wakizungumza
na waandishi wa habari waliofika kijijini hapo kusikiliza kero zao, walisema
sasa mifugo imekuwa salama kwa kiasi fulani.
Walisema,
kwa sasa wanalala kwa amani na wanaweza kukaa hadi miezi mitatu bila ya kusikia
uwepo wa wizi wa mifugo na mazao kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
Mwananchi
Khamis Ali Khamis, anasema kabla ya ulinzi shirikishi kuimarishwa, kila mwezi
kulikuwa wizi wa Ng’ombe kati ya watano hadai saba.
‘’Kwa sasa
unaweza kukaa miezi mitatu, ukasikia tukio moja la wizi wa Ng’ombe kwetu sisi
hali hiyo, tunasema afadhali mno tofauti na zamani,’’alisema.
Kwa upande
wake mfugaji Mohamed Mkubwa Mohamed, alieleza kuwa walifikia wakati wanapolala
wao ndio walipokuwa wakiilaza mifugo yao.
‘’Ilikuwa
lazima Ng’ombe au Mbuzi umlaze chini ya dirisha la nyumba yako, maana ukimuacha
malishoni siku ya pili ukienda ameshaibiwa,’’anafafanua.
Wakulima Leluu
Suleiman Said, Saada Suleiman Omar na Mtumwa Ali Omar, walisema ijapokuwa wizi
haujaondoka moja kwa moja, lakini wanalima na kuvuna mazao mapevu.
Walisema,
katika kijiji chao cha Vikunguni ndizi, muhogo, mananasi ilikuwa sio rahisi kuvunwa
mapevu, maana vijana wao walikuwa wakiyaiba.
‘’Kwa mfano
kama wizi wa Ng’ombe na mazao mara nyingi hufanyika nyakati za usiku au siku ya
Ijumaa wakati waumini na dini ya kiislamu wakiwa kwenye ibada,’’wanasema.
Vijana Issa
Khamis Issa, Kombo Juma Hassan na Mundhiri Ilyasa Hilali wanasema, moja ya eneo
ambalo linapaswa kudhibitiwa ni matumizi ya dawa za kulevya.
‘’Ingawa
jambo hili vijana wa shehia moja na nyingine huchanganyika, lakini kama hawa wa
Ng’ambwa watadhibitiwa inaweza kuwa mwarubaini kwa vitendo vya wizi,’’wanasema.
Sheha wa
shehia Ng’ambwa Issa Rihani Abass, amesema alimua kuelekeza nguvu katika ulinzi
shirikishi, ili kupunguza vitendo vya jinai shehiani humo.
‘’Ni kweli
baada ya kuteuliwa kushika nafasi hii, moja ya changamoto niliyoiona ilikuwa ni
wizi wa macho macho, sasa tukajipanga na wananchi na ndio maana kuna
afadhali,’’anafafanua.
Hata hivyo
alisema, bado dhamira yake hasa ya hapo baadae ni kuona shehia ya Ng’ambwa
wananchi wanalala bila ya hofu, pamoja na wakulima na wafugaji kuendesha
shughuli zao kwa amani.
Mkuu wa
wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali, amekuwa akirejea kuali yake kwa
wananchi, kuwa njia moja nzuri ya kuzuia uhalifu kwenye maeneo yao ni kuiunga
mkono Polisi Jamii.
Shehia ya
Ng’ambwa wilaya ya Chake chake inao wakaazi 2500, inazo huduma za kijamii kama afya,
elimu, mawasiliano ya simu na huduma za barabara kwa kiwango cha kifusi.
Mwisho
Comments
Post a Comment