NA HAJI NASSOR, PEMBA@@@@
JAJI Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan
Abdalla, amepiga marufuku kwa makarani wa mahakama, kuandika hati za madai kwa
wananchi, kwani kufanya hivyo, ni kinyume na sheria za utumishi.
Jaji Mkuu
huyo aliyasema hayo leo Machi 16, 2023 ukumbi wa mahakama kuu Pemba, wakati akizungumza na
mawakili wa kujitegemea na wale wa serikali, kwenye kikao kazi, cha kupokea
ushauri kuelekea mwaka mpya wa mahakama.
Alisema,
tayari Mahakama kuu imeshapiga marufuku kwa muda mrefu kwa makarani wa mahakama,
kuchukua kazi za kuandika hati za madai, kwani wanakuwa wanazitumia vibaya
rasilimali za serikali.
‘’Kuhusu
baadhi ya watendaji wa mahakama, na hasa makarani kuandika hati za madai ‘plaint’ tumeshapiga marufuku kwa muda
mrefu, na natarajia sasa watendaji wawe wameshalisikia hili,’’alieleza.
Katika hatua
nyingine, Jaji Mkuu huyo wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, alisema serikali
iko katika hatua za mwisho za kuandaa mpango, wa utozaji kodi itokanayo na
malipo ya mawaikili wa kujitegemea.
Alifafanua
kuwa, Mawakili wamekuwa wakidai kuwa wanatoa huduma kwa wananchi, ingawa nao
wamekuwa wakiwatoza fedha nyingi, bila kutozwa kodi.
‘’Mjiandae
sasa kutoa kodi kwenye malipo mnayowatoza wananchi wanaotaka huduma, za uwakili
kwenye mahakama zetu mbali mbali, ili nayo serikali ipata mapato
yake,’’alieleza.
Aidha Jaji
mkuu huyo wa Zanzibar, aliwataka mawakili hao, kuendelea kulinda maadili na
nidhamu za kazi zao, ili waendelee kuwa kimbilio kwa wananchi.
‘’Katika
siku za hivi karibuni, kumeibuka wimbi la baadhi ya Mawakili kuchupa maadili
yao, ikiwemo kutoleana lugha chafu na mahakimu, jambo ambalo halijengi taswira
nzuri,’’alieleza.
Kuhusu
ucheleweshaji wa mwenendo wa kesi, ‘proceeding’
alisema kwa sasa jambo hilo, halitarajii kutokea, baada ya kuongeza vitendea
kazi.
‘’Hivi
karibuni tumeshanunua kompyuta 10 na kuongeza idadi ya watendaji, lengo ni
kuona tunafanikisha utendaji wetu wa kazi, ikiwemo uandishi wa mwenendo wa
kasi,’’alieleza.
Mapema
Mrajisi wa mahakama kuu Pemba, Faraji Shomari Juma, alisema mkutano huo
umesadia kuwaamsha Mawakili hao, katika utendaji wao wa kazi.
Alieleza
kuwa, vikao kama hivyo, husababisha watendaji hao kuelezea mafanikio na
changamoto zao, katika kufanikisha kazi za kutoa huduma kwa jamii.
Akitoa neno
la shukran, Wakili wa kujitegemea Zahran Mohamed Yussuf, alimuahidi Jaji Mkuu
huyo kuyafanyia kazi maagizo aliyoyatoa kwenye mkutano huo.
Nae Mwanasheria
dhamana wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, Ali Haidar Mohamed alisema
ushirikiano uliopo baina ya mahakimu na mawakili wa kujitegemea, unajenga ari
kubwa ya kazi.
Jaji Mkuu wa
Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, yupo kisiwani Pemba, kwa ziara ya maalum ya
kukutana na watendaji wake, ambapo pia alizungumza na mawakili wa serikali na
wale binafsi.
Mwisho
Comments
Post a Comment