NA HAJI
NASSOR, PEMBA
SASA ni majira ya saa 8:00 jioni, jua limeshateguka, vivuli
vya miti mikubwa ndio mwemvuli wangu, nipo hapa kituo cha afya cha Uwondwe
shehia ya Mtambwe kaskazini, wilaya ya Wete Pemba.
Mbele yangu, namuoma mjamzito, akitokea chumba cha muuguzi wa
afya ya mama na mtoto, huku mkononi akiwa na gamba la kliniki, akionekana na
tabasamu.
Nilipomkaribia aliniambia, sasa huduma za mama na mtoto,
wanazipata ndani ya kituo hicho, na hasa baada ya kumalizika kwa ujenzi wa
barabara yao ya Bahanasa- Mtambwe.
Barara hiyo, ni kati ya zile tano (5), ziilizojengwa kwa
ufadhili wa Mfuko wa Changamoto za Millenia na watu wa Marekeani ‘MCC’ ikiwa ni
ile ya Kipangani- Kangani, Chwale- Likoni, Mzambarau takao pamoja na Pandani
hadi Finya zenye urefu wa kilomita 35 kwa ujumla.
Kwa uwepo wa barabara hiyo, wananawake wa Mtambwe, wanasema
moja ya huduma zilizoimarika ni upande wa afya ya mama na mtoto, na sasa ni
miaka tisa (9), wamesahau machungu, dhiki na shida.
HUDUMA ZA
AFYA
Wanawake, wanasema sasa wamesahau kubebwa kwa magunia, gari ya
Ng’ombe kupelekwa bandarini kwa ajili ya kuingizwa kwenye mitumbwi, ili kufikishwa
hospitali ya wilaya ya Wete.
Hamida Juma Mohamed wa Uwondwe shehia ya Mtambwe kaskazini,
anasema hawakuwa na thamani wanapotaka kujifungua, maana wanaume walikuwa ndio
gari zao za muda, kwa kuwabeba hadi bandarini, kabla ya kuingizwa kwenye mitumbwi.
‘’Kabla ya ujenzi wa barabara hii, iliyofadhiliwa na ‘MCC’
ilikuwa hapa Mtambwe, hakuna huduma za kujifungulia, tulilazimika kwenda Wete,
tena kwa mtumbwi,’’anasema.
Muhudumu wa afya, kituo cha afya Uwondwe Zainab Hassan Shehe,
anakiri kuwa, ujenzi wa barabara yao, ndio mwarubaini wa kupatiwa huduma za
uzazi kijijini kwao.
‘’Kwa mwezi, tupokea kati ya wajawazito 60 hadi 65, kuwapatia huduma
za mama na mtoto, na wanaojifungulia hapa hujitokeza kati ya 10 hadi 15, jambo
linalo ni faraja, hasa baada kuwepo kwa barabara hii,’’anasema.
Anaona, mwisho wa wajawazito wa Mtambwe kubebwa kwa magunia,
gari za Ng’ombe na vitanda imekoma, baada ya kuwepo wa barabara hiyo na
kufuatia kujengwa kwa kituo cha kujifungulia.
Lakini sio Mtambwe pekee, wanawake wanaokiri kuimarika kwa
huduma hizo, hata Mwanaisha Bakari Haji wa Kangagani, anasema sasa adha ya
kwenda Wete au Chake chake imekwisha.
‘’MCC kutujengea barabara yetu, kutoka Kipangani hadi kijiji
kwetu, imetupunguzia machungu ya usafiri, maana ilikuwa gari za Ng’ombe au
kubebwa kwenye magunia, ni jambo la kawaida,’’anasema.
Asia Haji Hussein wa Pandani, anasema dhiki kubwa walikuwa
wakiipata miaka tisa iliyopita, juu ya kufuata huduma za uzazi Wete na
Micheweni, sasa wameshazisahu, baada ya kujengewa barabara yao.
Kama alivyo Asia, hata Mwashamba Kombo Lali wa Finya, anasema watoto
wake watatu, amejifungulia kituoni kwao, baada ya serikali kuimarisha huduma za
uzazi na hasa uwepo wa barabara kwa kiwango cha lami.
‘’Baada ya kumalizika kwa ujenzi wa barabara yetu, sasa huduma
za afya zipo saa 24, lazima tuwashukuru MCC na serikali ya Mapinduzi, kwa
kushirikiana katika hili,’’anasema.
Bakar Faki Pandu ‘85’ mkaazi wa Chwale Madenajni, barabara ya Likoni
hadi bandari ya Kojani, anasema huduma za afya zilizorota, na waliopokuwa wakitaka
kumsafirisha mgonjwa kwenda hospitali ya Wete.
‘’Ujenzi wa barabara hii ya MCC kwetu wananchi wa Chwale,
Likoni na Kojani imekuja kutuimarishia usafiri, na hasa tunapokwenda kwenye
hospitali iwe cha Chake chake Wete,’’anaema.
Na hata Mwakame Hija Hamad, anasema aliwahi kuzaa njiani mwaka
2012, kutokana usumbufu wa barabara waliokuwa nao, ingawa sasa imekuwa mtelezo
kwao.
Aisha Ussi Hamad, anasema pamoja na kuimarisha huduma za afya Kisiwa
cha Kojani, lakini hata wanapokuwa na kesi kubwa za kwenda hospitali za Wete au
Chake chake, usafiri upo saa 24.
‘’Kabla ya ujenzi wa barabara hii, ilikuwa ukipata tatizo la
kwenda hospitali za Wete, kunausumbufu mara mbili, moja usafiri wa mtumbwi na
kisha unakumbana na ubovu wa barabara, lakini sasa shida tumeisahau,’’anasema.
Suleiman Makame Issa wa Kojani, anasema usafiri na
usafirishaji umekuwa rahisi kwao, iwe kwa wanaokwenda mjini, hospitali au
kufuata huduma nyingine, makao makuu ya serikali ya wilaya.
‘’Sasa tunalala Kisiwa cha Kojani na kuwahi shughuli kama za
matibabu hospitali kuu za Wete au Chake chake, jambo ambalo, lilikuwa ni adimu
kwa miaka kadhaa,’’anasema.
HUDUMA ZA
ELIMU
Mwalimu mkuu msaidizi wa skuli ya Msingi Uwondwe, akihudumu
miaka 31 sasa, Maryam Ali Hamad, anasema sasa wamekuwa na majengo ya kisasa na
kutanua wigo, wa upatikanaji elimu.
‘’Sasa skuli imeongezewa majengo, kutoka matatu ya awali hadi
matano, hivyo hata idadi ya wanafunzi nayo imeongezeka, lakini hata huduma za
umeme zimeimarika,’’anasema.
Anakumbuka, wakati anasoma skulini hapo, wanafunzi wenzake walikuwa
wakichelewa kwa saa moja, na hasa kwa siku za mvua, kutokana na uchakavu wa
barabara yao.
Wanafunzi Khamis Juma Ali, Omar Haji Omar, Is-haka Mjaka Sauod
na mwenzake Khadija Kombo Yussuf wa skuli za Pandani, Finya, Uwondwe, Kangagani,
wanasema barabara imewasaidi kuendeleza ushirikiano na skuli nyingine.
‘’Kila muda tunapokea wanafunzi na ugeni wa tasisi nyingine,
kutokana na kuwepo kwa barabara ya uhakika, jambo ambalo limetuamsha ari ya
kusoma kwa kushindana,’’anasema.
Afisa Mdhamini wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba
Mohamed Nassor Salim, anasema uwepo wa barabara hizo, kwao zimerahisisha
usafirishaji wa vifaa vya ujenzi wa skuli na vitabu vya kujisomea.
‘’Gharama ya kusafirishia vifaa kama vitabu, chaki, mitihani na
vifaa vya ujenzi imeondoka hasa kuanzia mwaka 2014, baada ya udunguzi wa
barabara tano za mkoa wa kaskazini Pemba, ‘’anaeleza.
HUDUMA ZA
UMEME
Afisa Mawasiliano na Huduma kwa wateja wa Shirika la Umeme
Zazibar ‘ZECO’ tawi la Pemba Haji Khatib Haji, anasema barabara hizo zimechangia
kwa asilimia 100, usambaazaji wa huduma ya umeme vijijini.
‘’Vijiji vya Kangagani tumesambaaza umeme eneo lenye wa urefu
wa kilomita 2, sambamba kufanya matengenezo, kupeleka umeme wa njia kuu na
mdogo wa kilomita 3.5 kisiwa cha Kojani pamoja na Likoni Chwale, kwa kutumia
barabara za MCC,’’anasema.
Kwa muda mrefu, walikuwa wanashindwa kuwafikishia huduma hiyo
wateja waao, hiyo ni kutokana na miundombinu kuwa chakavu na hasa uzito wa gari
na vifaa vyao.
Upande mwengine anasema, barabara ya Bahanasa- Mtambwe
mwishoni 2020 /2021, waliitumia wakati
wanasafirishia vifaa vya huduma ya umeme wa sola, kwa wananchi wa kisiwa cha
Kokota wilaya ya Wete.
Wananchi Omar Khamis Haji na mwenzake Siti Omar Hamdu wa Finya
wanasema, kwa vyovyote vile, uwepo wa barabara yao kwa kiwango cha lami, kwao
imerahisisha kuunga huduma ya umeme.
Asha Haji Hamza wanasema, sasa imekuwa rahisi kwake, anapokuwa
na changamoto kwenye shirika la umeme, kufuatilia mjini Chake chake au Wete, na
hapo kabla ya ujenzi wa barabara, lilikuwa zito kwake.
HUDUMA ZA
KISHERIA
Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi
Pemba, Safia Saleh Sultan, anasema kabla ya kufunguliwa kwa barabara hizo mwaka
2014, walikuwa wakipokea wanawake kati ya watano (5) hadi 10 kwa mwezi, waliyokuwa
wakihitaji masaada wa kisheria.
‘’Baada ya kufunguliwa, sasa wanawake wamehamasika na tumekuwa
tukiwapokea kati ya 35 hadi 40 kwa mwezi, kutoka vijiji vya Kangagani, Kojani,
Mtambwe, Finya na Pandani zilimopita barabara za MCC,’’anasema.
Mwananchi wa Mzambarau takao, Moza Abass Mohamed anaona uwepo
wa barabara hiyo, imerahisishia kufuatilia hudumza kisheria, kituo cha Polisi
Wete.
‘’Mwaka 2019, niliibiwa ndizi na kuku wangu saba, lakini kwa
vile barabara ipo vyema, nilihamasika kufika kituo cha Polisi, kufuatilia haki
zangu, lakini kwa zamani, isingekuwa kuwa rahisi,’’anasema.
Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Kangagani Awena Salim
Kombo, anasema wanawake sasa wanafika kituo cha Polisi Mchanga mdogo,
wanapokutana na changamoto za kisheria.
‘’Hata usiku sasa mtu anakodi bajaji au boda boda na kupeleka
malalamiko yake, ambapo zamani kwa uchakavu wa barabara haikuwa rahisi hata
kidogo,’’anasema.
SERIKALINI
Afisa Mdhamini wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Pemba
Ibrahim Saleh Juma, anasema tokea kufunguliwa kwa barabara hizo, miaka tisa (9)
iliyopita hawajawahi kuzifanyia matengenezo, kutokana na uimara wake.
‘’Matengenezo tuliyoyafanya, ni barabara ya Bahanasa- Mtambwe
kwenye daraja, baada ya kuharibika kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwaka
2017 na kwa sasa barabara zote tano, ziko madhubuti,’’anasema.
Aliyekuwa kuwa Mhandisi mkaazi wa ujenzi wa barabara Pemba, wakati
wa ujenzi wa barabara za MCC, Khamis Massoud Khamis, anasema uimara wa barabara
hizo, ulitokana na aina ya ujenzi.
Ujenzi wa barabara hizo umetofautiana na nyingine, maana
tabaka mbili za juu ‘sub base and base’ zilichanganywa kokoto nyembamba na saruji,
kwa ujazo wa mita moja, kwa mfuko mmoja wa saruji.
Barabara za ‘MCC’ hazikutumia utaalamu wa lami moto ‘asphalt
congreatE’ bali zilitumia mfumo wa lami ya kuchemsha ‘surface
dressing’ na kisha humwagwa, baada ya muda humiminiwa kokoto zenye
ujazo wa milimita 15 hadi 20, na kuzama kwenye lami hiyo.
‘’Baada ya kushindiliwa hadi kuzama kwa kokoto, humwagwa tena
lami zikiwa na kokoto ndogo ndogo, zenye ujazo kati ya milimita 8 hadi 10,
lengo ni kuziba nafasi ilizoachwa wazi na kokoto kubwa za awali,’’anafafanua.
Jengine ni kutumia shilingi bilioni 1.1 kwa urefu wa kilomita
1, wakati ujenzi wa barabara za kawaida kwa urefu huo, hutumia gharama ya shilingi
bilioni 1.
‘’Ujenzi wa aina hii ya barabara za MCC, hutakiwa kufanyiwa
matengenezo kila baada ya miaka 10, ingawa kwa kwetu zinaweza kuzidi kutokana
na kutokuwepo kwa gari, nyingi zenye uzito wa zaidi tani 15, kama uhimili wa
barabara hizi inavyotakiwa,’’anasema.
Aliyewahi kuwa Afisa Mdhamini wa wizara hiyo Hamad Ahmed
Baucha, anasema barabara hizo, zilisimamiwa na wenyewe kuanzia uchoraji wa
michoro, hadi kwenye ulipaji wa fidia.
Mwisho
Comments
Post a Comment