NA ZUHURA JUMA, PEMBA:
MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Matar Zahor
Masoud amesema, wananchi wanashindwa kujua wajibu wao na badala yake
wanailalamikia mahakama kwamba haitendi haki.
Alisema kuwa, ipo haja ya wananchi
kushirikiana na mahakama katika kutoa ushahidi na kuacha tabia ya kulalamika
kwamba mahakama hazitendi haki.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho
ya siku ya sheria yaliyofanyika katika Uwanja wa Tenis Chake Chake, alisema
kuwa bila ya ushahidi hakimu hawezi kumtia hatiani mshitakiwa, hivyo juhudi
zinahitajika katika kutoa ushahidi ili keshi zipate hatia.
"Kwanza tuzisimaie kesi zetu vizuri,
tuzifiatilie na tutoe ushahidi, hii itasaidia kesi kupata hukumu, lakini ikiwa
tunakaa tu hatufiki mahakamani baadae analalamika sio sahihi", alisema.
Aidha alisema, mfumo wa huduma ya haki mtandao
watakaotumia mahakama utarahisisha usikilizaji wa mashauri, jambo ambalo
litasaidia upatikanaji wa haki kwa haraka.
Kwa upande wake Jaji kutoka Mahakama Kuu
Zanzibar Abdulhakim Ameir Issa alisema kuwa, ukuaji wa tehama duniani
unarahisisha ukuaji wa uchumi kwani inasaidia kudhibiti mianya ya upotevu wa
mapato na ndio maana na wao wakaamua kutumia haki mtandao kwa kukuza uchumi na
ustawi wa jamii.
"Mfumo wa tehama ni mzuri kwani
utawaimarishia katika mfumo mzima wa uendeshaji kesi na wananchi watapata haki
zao kwani huduma zitaimarika", alisema.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar Jecha Vuai Jecha alieleza kuwa, lengo la siku ya sheria ni kuisaidia
jamii kupata uelewa wa sheria pamoja na kupata haki stahiki.
"Ili kwenda sambamba na mahitaji ya sasa,
Serikali imerahisisha huduma za kijamii na upatikanaji wa haki, kujenga
mazingira wezeshi kwa wananchi, lengo ni kuona wanapata haki zao",
alieleza.
Nae Wakili Mbobevu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi
wa Mashitaka Pemba Ali Haidar Mohamed alifahamisha kuwa, huduma za mtandao
zitaweza kujenga imani kwa wananchi, kupata haki, kuongeza mapato na kuimarisha
utendaji ambao utaondoa mianya ya rushwa.
Akisoma risala ya Chama Cha Wanasheria za
Zahran Mohamed Yussuf alisema kuwa, miongoni mwa majukumu yao ni kurekebisha
jamii, kusimamia haki na kutekeleza majukumu ya kazi pasi na ubaguzi, jambo
ambalo linasaidia upatikanaji wa haki kwa urahisi.
Maadhimisho hayo ya siku ya sheria yamefanyika
katika Uwaja wa Tenis Chake Chake Pemba, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni
'HAKI MTANDAO KWA KUKUZA UCHUMI NA USTAWI WA JAMII'.
MWISHO.
Comments
Post a Comment