NA HAJI NASSOR, PEMBA::
KUMBE masuala ya haki za binadamu,
yalianza kuingizwa katika mikataba mbalimbali ya kitaifa mwaka 1950.
Na kwenye Azimio la kulinda Haki za
Binadamu Ulimwenguni lilifikiwa mwaka 1984 na Afrika mwaka 1981.
Baada ya
hapo, mikataba ya kikanda ilipitishwa, kwa dhamira ya kutoa ulinzi wa haki za
kiraia na kisiasa, haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, kwa ufanisi zaidi.
Maazimio
mbali mbali, yaligusia juu ya suala la uhuru wa maoni na kujieleza, likiwemo
azimio la ‘UDHR, katiba ya Zanzibar ya mwaka
kifungu cha 18 (1) na (2) kama nayo imeeleza:
“Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila
mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta
kupokea na kutoa habari na dhana kupitia chombo chochote, bila ya kujali mipaka
ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati”
Hata kifungu cha (2) ‘’kila raia anayo
haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani
kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shuhuli za wananchi, na pia juu ya masuala
muhimu kwa jamii”
Zipo sheria nyingi kwa namna moja ama nyingine, zinaathiri
uhuru wa habari na haki ya kujieleza kwa mfano sheria ya Usalama wa Taifa,
Sheria ya Baraza la Wawakilishi, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Makosa ya
Mtandaoni.
SHERIA YA MAGAZETI ZANZIBAR
Sheria ya Usajili wa Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya
mwaka 1988 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 8 ya mwaka 1997, ambapo sheria hii imekua na mapungufu mengi, yanayokwamisha
haki ya uhuru wa vyombo vya habari na uandishi wa habari Zanzibar.
Kwa mfano kifungu cha 27(1),(2) na (4)
kinachoelezea uwezo wa kukamata magazeti na kupekua majengo.
Kifungu kidogo (1) ofisa yeyete wa Polisi anaweza
kukamata gazeti lolote, popote litakapoonekana, lililochapwa au kuchapishwa, au
ambalo kwa maoni yake atalituhumu kwamba limechapwa au kuchapishwa, kinyume na
sheria hii.
Kifungu kidogo(2) hakimu yoyote anaweza kwa hati, kumruhusu ofisa yoyote wa polisi wa cheo
cha mkaguzi au cheo cha juu yake, akiwa na msaada au bila ya msaada, kuingia na
kuepuka sehemu yoyote ambayo kwa maoni yake anadhani kwamba limo gazeti
lililochapwa kinyume na sheria hii.
Aidha kifungu kidogo (4) gazeti lolote lililokamatwa chini ya kifungu
litapelekwa haraka iwezekanavyo kwa hakimu, ambaye anaweza, ikiwa atajitosheleza
kwamba gazeti lilichapwa au kuchapishwa kinyume na sheria hii.
INTENEWS/
TAMWA –ZANZIBAR ZINAFANYA NINI?
Chama cha Waandishi wa habari Wanawake
Tanzania TAMWA-Zanzibar kwa ufadhili wa Shirika la Internews, kwa sasa wapo
katika kufanyia uchechemuzi wa sheria hiyo, katika vifungu mbali mbali ambavyo ni
kandamizi, ili kuweze kupatikana kwa sheria mpya.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzuri Issa Ali, anasema kuna baadhi ya vifungu
katika sheria ya hiyo vimekua sio rafiki kwa waandishi wa habari, hali
inayopelekea baadhi ya waandishi kufanya kazi kwa woga.
“TAMWA imekua
ikikutana na wadau mbali mbali wa habari kujadili, mapungufu yaliyomo ndani ya
sheria hiyo na kutoa maoni yao, ili mwisho wasiku maoni hayo yawasilishwe na
kuwa na sheria rafiki kwa waandishi,”amesema.
Mratibu wa
Internews Tanzania ofisi ya Zanzibar Zaina Mzee, anasema wameamua kuunga za
pamoja na TAMWA-Zanzibar ili kuhakikisha Zazibar inakuwa na sheria bora.
Anasema,
mwelekeo hasa ni kutaka kufutwa kwa sheria hiyo Magazeti pamoja na ile ya Tume
ya Utangaazaji nambari 7 ya mwaka 1997, ili Zanzibar kuwe na sheria moja.
‘’Ndio maana
Internews hailali, iko huku na kule, kuhakikisha sekta ya habari Zanzibar
inaongezewa thamani kwa kuwepo kwa sheria rafiki,’’anasema Mratibu huyo.
Hapa akaongeza
kuwa, anawategemea sana waandishi wa habari na wadu wao, ili kuona wanaviibua
na kuvisemea vifungu kandamizi kwa uhuru wa habari.
‘’Suala la
kupata, kusambaaza habari lipo kikatiba zaidi, sasa kama sheria imetungwa
inakinzana na haki hiyo, haina nafasi kwa sasa,’’anasema.
WAANDISHI
WA HABARI WENYEWE
Berema Suleiman Nassor, wa Zenj Fm redio
Unguja, anasema kifungu hicho kinapaswa kufanyiwa marekebisho ya haraka, kwani
kinampa mamlaka makubwa polisi wakati zipo taasisi za kihabari zinazopaswa
kusimamia kitu hicho.
Kuwepo kwa mamlaka hayo kutapelekea
waandishi, wauzaji, wasambazaji na makampuni kuwatia hofu kila wakati kuhofia
kukamatwa.
Jabiri Idrissa kutoka Mwanahalisi
mtandaoni, anasema tasnia ya habari, inaenda kuwa mhimili wa nne usio rasmi,
kumpa mamlaka polisi au chombo chengine sheria kwenda kufanya upekuzi au kuwadhalilisha
waandishi.
“Kama kuna mamlaka inahisi gazeti
limeaandika vibaya au limekwenda kinyume na sheria za habari, vizuri kufuata
taratibu za kisheria na sio kuwakamata moja kwa moja au kuwavamia.
Mwandishi
wa habari kutoka Gazeti la Zanzibarleo Pemba Habiba Zarali Rukuni, anasema mamlaka
hayo kwa ofisa wa Polisi, anaweza kukamata gazeti atakapojisikia tu kukamata na
sio kwa kufanya kosa.
Meneja
wa radio Jamii Mkoani Said Omar Said, anasema sio sahihi kwa ofisa Polisi
kupewa mamlaka hayo, kwani uhuru wa habari utakuwa bado haujakuwepo nchini.
“Kama
mwandishi amegombana na afisa wa polisi, mitaani na ubarabarani si anaweza kuutumia
ugomvi huo kuja kufanya upekuzi na kusababisha sito fahamu kwa waandishi na
chombo cha habari.”amesema.
WADAU WA HABARI
Katibu wa Jumuiya ya Waandishi wa Habari Pemba
PPC Ali Mbarouk Omar, aliwahi kusema kuwa, vifungu vya sheria hiyo haviko sawa
na vinakandamizi mno tasnia ya habari, kwa kutoa mamlaka ya moja kwa moja kwa
vyombo vya ulinzi.
Mkurugenzi wa KUKHAWA Pemba Hafidh Abid
Saidn, anasema uwezo uliopo katika kifungu ni mkubwa na unanyima uhuru wa
waandishi wa habari na taasisi zao kufanya kazi zao ipasavyo.
“Hii sheria inaonekana ni kongwe sana na
imeshapitwa na wakati, sasa ni wakati wa maendeleo lazima sheria hii ifanyiwe
mabadiliko makubwa ili iweze kuendana na mabadiliko yaliyopo,”amefahamisha.
Mratibu
wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said, anasema Mamlaka ya Polisi ni kulinda raia
na mali zao na amani ya nchi, hivyo mamlaka yaliomo katika kifungu 27 kifungu
kidogo (1)(2) na (4) yanapaswa kufanyiwa maboresho.
“Kitakapoboreshwa
kifungu hicho, waandishi watakuwa huru kufanya kazi zao za kihabari na wananchi
watapata habari, uhuru wa kutoa maoni na kujieleza", anasema.
Khalfan Amour Mohamed ambae ni mwanasheria, anasema kifungu cha
27 kifungu kidogo (1) hakipo sawa na kinanyima uhuru wa habari kwa waandishi na
taasisi ya kihabari.
“Kichekesho zaidi anaposema ‘kwa maoni yake’ neno hili
halitakiwi liwepo kisheria na kupewa mamlaka makubwa Polisi,’’alieleza.
Anasema kifungu kidogo (2) kinaenda kinyume na vifungu vya
sheria nyengine, ambazo zinaelekeza namna ya kufanya upekuzi na ukamataji wa
vitu vinavyodhaniwa kuwa ni makossa.
Anafafanua kuwa, sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai Zanzibar
namba 7 ya mwaka 2018, na Sheria ya Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na madawa
ya kulevya Zanzibar, zimeweka utaratibu wa kufanyika upekuzi.
Naye Afisa Sheria kutoka Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria
Zanzibar Ofisi ya Pemba Bakar Omar Ali, anasema kifungu hicho hakipo sawa na
kinahitaji kufanyiwa marekebisho.
Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali Zanzibar Ali
Haji Mwadini, anasema sheria inayonyima uhuru wa waandishi wa habari kufanya
kazi zao vizuri na kikamilifu, haijengi.
Mjumbe wa Kamati tendaji kutoka Pemba Press Club Gaspary Charles,
amesema sheria kumpa nguvu ofisa wa polisi uwezo wa kukamata na kufanya upekuzi,
ni kipimo kikubwa cha ukiukwaji wa uhuru wa habari nchini.
Katibu
Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania(MCT) Kajubi Mukajanga, anasema waandishi
wasipozieleweka sheria zao, mchakato wa kupitisha utakuwa kwenye mikono ya
wanasheria na wanasiasa na hivyo watapendekeza wanavyotaka.
Asha
Khamis Juma na mwenzake Tatu Abdalla Msellem, wanasema jamii kwa kiasi kikubwa
inavitegemea vyombo vya habari kuweko huru na kuwaibulia mambo wasiyoyaona.
Mchambuzi
wa sheria za habari Zanzibar Imane Duwe, anasema wakati wa Zanzibar sasa
kuachana na sheria kandamizi umekwisha.
MWISHO
Comments
Post a Comment