NA HAJI NASSOR, PEMBA:::
SASA ni miaka 26 tokea kuasisiwa kwa
sheria ya Tume ya Utangaazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, licha ya
kujumuisha na marekebisho yake.
Sheria hii,
imekuja kusimamia, kuangalia mwenendo wa vyombo vya habari Zanzibar hasa redio,
televisheni na vile vya kisasa vyenye kurusha maudhui yao mtandaoni.
Sheria hii
yenye vifungu 30, vilivyobebwa na sehemu sita kuu, inavyovifungu kwa hakika sio
rafiki, kuelekea uhuru kamili wa habari hapa Zanzibar.
SHERIA KWA UJUMLA
Kama ilivyo
sheria nyingine zote, kwenye sehemu ya kwanza imeundwa na vifungu vitatu, maana
kile cha nne, kimefutwa na kati ya hivyo kimoja kinatoa jina la sheria na maana
ya maneno.
Kwa mfano, mtangaazaji ni mtu ambaye amepewa leseni
chini ya sheria hii ya kutoa huduma za utangaazaji katika vyombo vya habari.
Kwenye
sehemu ya pili ya sheria hii, yenyewe imeundwa na vifungu kuanzia cha tano (5)
hadi cha 10, na kubwa zaidi lililopo ni pamoja na uanzishwaji wa Tume ya
Utangaazaji Zanzibar.
Jengine ni kinga
kwa wajumbe wa Tume, majukumu ya maafisa wa tume, muundo wake pamoja na saifa
za Katibu Mtendaji.
Sehemu ya
tatu ya sheria, imejitegemea kwa vifungu vinne (4) kuanzia kile cha 11 hadi cha
14, ni eneo lililotajwa uwepo wa zuio la utangaazaji, usiokuwa na leseni, masharti
ya kuomba, utoaji wake na kiwango cha matumizi na kuongeza muda wake.
Sehemu ya
nne (4), inaangalia zaidi uratibu na usimamizi wa utangaazaji, huku sehemu ya
tano, ikundwa na vifungu saba (7) na ikiangalia zaidi amsuala fedha.
Sehemu ya
sita ya sheria hii ya Utangaazaji Zanzibar nambari 7 ya mwaka 1997, imeundwa na
vifungu vitano (5) kuanzia kile cha 26 hadi 30, ambacho kinaelezea kufutwa kwa
sheria nambari 25 ya mwaka 1961.
VIFUNGU HASIDI KWA UHURU WA HABARI
ZANZIBAR
Vipo vifungu
kadhaa, lakini kimoja wapo, kinachotishia na kuutia doa uhuru wa habari hapa
Zanzibar ni kile cha 13 (5).
‘’Mtu yeyote
asiyeridhika na uamuzi wa Tume kutoa au kataka maombi, anaweza kukata rufaa kwa
Waziri kwa namna ya njia itakavyoelezwa na kanuni,’’kinaeleza kifungu hicho.
Ambapo hapa,
momba leseni (kwa mfano mwandishi wa habari), anapokataliwa kupewa leseni na
Katibu Mtendaji wa Tume, akate rufaa kwa waziri, ambae ndie aliyemteua Katibu
huyo.
Wadau wa
sheria wanasema, jambo hilo lina utata, maana Katibu Mtendaji wa Tume ya
Utangaazaji na waziri anayehusika na utangaazaji, ni kiungo kimoja.
Mwandishi
Talib Ussi Hamad, anasema hilo ni sawa na kesi ya Nyani, hakimu kuwa Nyani na
mtoa ushahidi Nyani, na uamuzi utakwenda kwa Nyani.
Mwandishi
Salim Said Salim, anasema kifungu hichi hakijakaa vyema, kwenye kuimarisha
uhuru wa kujieleza na wa kutoa maoni hapa Zanzibar.
Mwandishi wa
Shirika la Utangaazaji Zanzibar ‘ZBC’ Khadija Kombo anasema, kama Tume imekataa
kutoa leseni, kifungu kingelekeza vyenginevyo, kwa mfano kukimbilia mahakamani.
Kifungu
chengine chenye maneno yenye ukakasi na ukuaji wa wa uhuru wa habari ni cha 27
(1), ambapo waziri husika au mwengine aliyeidhinishwa, anaweza kutoa amri
kumtaka mpewa leseni (mmiliki wa chombo cha habari),
atangaaze jambo lolote ambalo kwa maoni ya Waziri, lina maslahi kwa umma au
uslama wa taifa.
Hapa wadau
wa habari wanasema, kifungu hicho kipo kishari shari zaidi, maana kimebainisha
uwezo wa Waziri, kumlazimisha mpewa leseni kutangaaza jambo ambalo anaona tu ni
kwa maslahi ya umma au usalama wa taifa.
Mdhamini wa Baraza
la Habaeri Tanzania ‘MCT’ Zanzibar Shifaa Said Hassan, anasema neno kwa maslahi
ya umma, sheria hiyo haijalitafsiri, hivyo waziri anaweza kutumia mwanya huo
kutangaaza jambo ovu.
Hata
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA- Zanzibar
Dk. Mzuri Issa Ali, anasema, neno usalama wa taifa, sheria hiyo kwenye vifungu
vyake 30 na sehemu sita halikutajwa.
‘’Hapa mpewa
leseni, amewekwa njia panda, maana Waziri akiamka vibaya anaweza kutumia mwanya
huo, na kutoa taangazo ambalo halina maudhui na nchi, huku sheria ikimlinda,’’anasema.
Mwandishi wa
kituo cha Redio cha Zenj fm Berema Suleiman Nassor, anasema hilo linajenga hofu
kuanzia kwa wamiliki wa vyombo vya habari na mwandishi mmoja moja.
Mwanasheria
wa Shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar na mhariri wa habari wa shirika
hilo, Juma Khamis Juma, anasema kwenye utekelezaji na tafsiri za vifungu vya
sheria, hakutakiwi kuwepo neneo lenye utata.
‘’Kwa mfano
neno waziri anaweza, akiona inafaa, akihisi na mengine yanayofanana na hayo,
huwa ni hatari kuwepo kwenye maelezo ya utekelezaji wa sheria,’’anasema.
Ndio maana Mratibu
wa Shirika la Internews Zanzibar, Zaina Mzee, anasema vifungu ambavyo vinampa
uwezo mkubwa waziri, au vina maneno yenye utata, kwa sasa wanasimama kutaka
viondolewe.
Kama sheria
ni haki ya kikatiba, ni vyema isiwe na maneno au amelezo yanayoashiria kumpa
mtu mmoja uwezo, kama vile anajiamulia kufanya mambo yake binafsi.
‘’Muda wa
kuwa na sheria yenye maneno ya kukuza uhuru wa habari na uhuru kujieleza ndio
huu kwa Zanzibar, na ndio maana tumeungana na TAMWA-Zanzibar na waandishi wa
habari kuhakikisha hilo linafanyika,’’anasema.
‘’Nguvu ya
kutaka sheria mpya ya habari, sisi tunavitegemea vyombo vya habari, na ndio
maana tunavishirikisha kila hatua, ili kusaidia kuzieleza mamlaka ubaya wa sheria
zinazosimamia habari ulivyo,’’anaeleza.
WANANCHI
Khamis Iddi
Mabrouk na mwenzake Issa Haji Khamis wa Kangagani, wanasema waandishi
wasipokuwa huru, hata wananchi hawatokuwa huru, kufanya uamuzi sahihi.
Hidaya Mjaka
Ali wa Vitongoji mwenye ulemavu wa viungo, anasema, wanavitarajia mno vyombo
vya habari, kuibua changamoto za jamii, na hilo litawezekana ikiwa wako huru.
Sheha wa
shehia ya Mchanga mdogo Asaa Makame Said, anasema vyombo vya habari, havipaswi
kuwekewa sheria zenye utata, kwani watashindwa kutekeleza kazi zao vyema.
NINI ATHARI YAKE?
Moja wadau
wanasema, ni kuwafanya waandishi wa habari kufanyakazi kwa woga na nidhamu
iliyopindukia mipaka, huku ikieleweka kuwa, wao kazi yao ni kuitekeleza Katiba.
Mwandishi
Malik Shahran wa ZCTV anasema, suala la habari ni haki ya binadamu, si vyema
kuwepo kwa sheria inayoonesha nguvu za mtu mmoja kufanya uamuzi.
‘’Maneno
kama Waziri akiweza, atakavyoona inafaa au kwa maoni yake, yanapekelea wengine
kukosa hamu ya kuingia kwenye sekta ya habari,’’anasema.
Mwandishi wa
Mwanahalisi mtandaoni Jabir Idrissa, anasema athari kubwa ni wawekezaji sekta
ya habari, kukosa hamu ya uwekezaji, na kundi kubwa kukosa ajira.
Miraji Manzi
Kae wa redio Jamii Makunduchi, anasema woga wa waandishi kukosa kufichua maovu,
wakati mwengine, hutokana na uwepo wa sheria kandamizi.
NINI KIFANYIKE?
Mwenyekiti
wa Klabu ya waandishi wa Habari Zanzibar ‘ZPC’ Abdalla Mfaume, anasema moja ni
kuzisemea sheria na vifungu kandamizi, ili waandishi wa habari wafanyekazi zao
kama ilivyo, kwa makundi mengine.
Rahma
Suleiman wa Gazeti la Nipashe, anasema waandishi na wadau wa habari, waungane
kusindikiza mswada wa sheria habari Zanzibar ulipofikia, upelekwe hatua
nyingine.
Mchambuzi wa
sheria za habari Zanzibar Imane Duwe, anasema maneno kama ‘uwezo wa Mkurugenzi, Waziri,
akiona inafaa, akihisi, kwa maoni yake’ kwenye sheria mpya ya habari
yasitumike.
Mdhamini wa
Baraza la Habari Tanzania ofisi ya Zanzibar Shifaa Said Hassan anasema, wakati
umefika Zanzibar kuwa na sheria bora na rafiki.
Mkurugenzi
wa TAMWA-Zanzibar Dk. Mzur Issa Ali, anasema ujio wa sheria mpya ya habari,
vifungu vinavyompa uwezo mkubwa waziri vifutwe.
Hata mwandishi
wa Redio Jamii Mkoani Khadija Rashid Nassor, anasema kila mmoja akitekeleza
wajibu wake, sheria hiyo kandamizi itaondoka.
Mwisho
Comments
Post a Comment