Sheria
nambari 5 ya Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu ya mwaka 1988, ambayo
imefanyiwa marekebisho mwaka 1997, bado baadhi ya vifungu vyake vinaminya uhuru
wa habari nchini.
Kifungu cha 27 (1) ni miongoni mwa
vifungu kinachompa Mamlaka Ofisa yeyote wa Polisi, kukamata gazeti lolote,
popote litakapoonekana limechapwa au kuchapishwa au ambalo kwa maoni yake tu, atalituhumu
kwamba limechapwa au kuchapishwa kinyume na sheria.
Ambapo kifungu cha 27 (3) pia
kinampa Mamlaka hakimu kumuamuru Ofisa yeyote wa cheo cha mkaguzi au zaidi, ikiwa
ana sababu ya maana ya kuamini kwamba, atachelewa kupata hati ya upekuzi
anaweza kutekeleza uwezo alio nao kwa mujibu wa sheria.
Vifungu hivi kwa nyakati za sasa,
havipaswi kuwepo katika sheria hiyo kutokana na kuwa sio rafiki kwa uhuru wa
vyombo vya habari nchini.
Wadau mbali mbali, wamekaa pamoja
kuvifanyia uchechemuzi baadhi ya vifungu vinavyokandamiza uhuru wa vyombo vya habari,
tangu mwaka 2010 ingawa bado vinaendelea kutumika, hali ambayo inawakwaza
wanahabari.
Lengo la kuvifanyia uchechemuzi
vifungu hivyo, ni kuhakikisha kwamba, vinafanyiwa maboresho na vyengine
vinaondoshwa kabisa, ili viwape uhuru wanahabari katika kufanya kazi zao.
Mwandishi wa habari wa kujitegemea
Mohamed Khalfan Ali anasema, sio vizuri kuwepo kifungu hicho kinachompa Mamlaka
Ofisa Polisi kwa kutuhumu tu, kwani kitawapa nguvu ya kudhalilisha waandishi na
vyombo vya habari.
"Hiki kifungu kinapaswa
kuondoshwa kabisa, Ofisa Polisi asipewe Mamlaka hayo kwa sababu, watavunjia
vyombo vya habari heshima yake na kuvidhalilisha", anasema.
Maryam Salum Habib mwandishi wa
habari wa Gazeti la Zanzibarleo Pemba anasema, Mamlaka hayo aliyopewa Ofisa wa
Polisi anaweza kukamata gazeti, atakapojisikia tu kukamata na sio kwa kufanya kosa.
"Kifungu hicho kinampa Mamlaka
endapo tu atatuhumu gazeti limechapishwa kinyume na sheria, hivyo akiwa na
chuki zake bianafsi anaweza kufanya hivyo, kwa vile kifungu kinamlinda",
anafahamisha.
Meneja wa radio Jamii Micheweni Ali
Massoud Kombo anasema, sio sahihi kwa Ofisa Polisi kupewa Mamlaka hayo, kwani uhuru
wa habari, itakuwa bado haujakuwepo nchini.
"Ikiwa afisa atakuwa na ugomvi
na mwandishi, anaweza kufanya upekuzi au kukamata gazeti, hali ambayo itasababisha
taharuki katika vyombo vyetu,’’ anasema.
Diwani wa Jimbo la Ole kupitia CCM
Khadija Henock Maziku anasema, ilipaswa kifungu kieleze, wakishatuhumu wafanye
uchunguzi kwanza, ndipo wakamate gazeti.
"Hii ya kuchukua uamuzi wa
kukamata gazeti bila kufanya uchunguzi, ni kudhalilisha chombo cha habari na
waandishi wake, watakapotuhumu wanatakiwa wafanye upelelezi wa siri, ndipo
mengine yaendelee", anashauri.
Anafafanua kuwa, ikiwa watafanya
hivyo kutokana na kifungu kinavyoeleza, watawajengea woga waandishi wa habari
na kusababisha kufanya kazi zao vibaya.
"Baada ya kuthibitisha kuwa
kuna ukiukwaji wa sheria ndipo watangaze na kulikamata gazeti, na baadae
wawajibishwe lakini sio kwa kutuhumu tu, hiyo sio sawa,’’ anasema.
Hafidh Abdi Said ambae ni Mwenyekiti
wa CHADEMA Wilaya ya Chake Chake anasema, baadhi ya vifungu vya sheria iliyopo ni
kwa maslahi ya wachache, ndio maana zinawakwaza wengine.
Anasema, baadhi ya vifungu havipo
kumlinda mwandishi na vyombo vya habari, na wala havina maslahi kwao, hivyo
kuna haja ya kufanyiwa marekebisho.
"Kifungu hicho hakifai kuwepo
kwa wakati huu tulionao, kwani waandishi watashindwa kufanya kazi zao na
wananchi watakosa haki yao ya kupata habari,’’ anaeleza.
Mwanasheria wa serikali Ali Amour
Makame anasema kwamba, sio sahihi kifungu hicho kuwepo kwa sababu, kisheria
halitakiwi kuwepo neno ‘kwa maoni yake’
na haifai kwa Afisa Polisi kupewa mamlaka hayo kwani, habari inaweza kuwa
sahihi kwa mujibu wa maadili yao, lakini yeye isimfurahishe.
‘’Elimu za Polisi tunazijua, iweje
wapewe mamlaka hayo kwa taaluma nyengine?, hii sio sahihi, kinachoshangaza
zaidi ni pale sheria hii ilipoeleza kwamba kwa maoni yake, akituhumu, hichi
kitu hakipo kwenye sheria’’, anafafanua.
Akielezea kuhusu upekuzi na
ukamataji, kifungu hicho kinaenda kinyume na vifungu vya sheria nyengine,
ambavyo vinaeleza namna ya kufanya upekuzi na ukamataji wa vitu vinavyodhaniwa
kuwa ni makosa.
TAMWA
–ZANZIBAR, MCT NA INTERNEWS
Fat-hiya Mussa Said ambae ni Mratibu
wa TAMWA Pemba anaefahamisha, Polisi wana mamlaka ya kulinda raia na mali zao
na kulinda amani ya nchi, ndio maana walipewa mamlaka hayo, lakini kwa wakati
wa sasa kifungu hicho kinahitaji maboresho.
"Kitakapoboreshwa kifungu
hicho, waandishi watakuwa huru kufanya kazi zao za kihabari na wananchi
watapata habari, uhuru wa kutoa maoni na kujieleza", anasema.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari
Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga anasema, waandishi wasipozielewa sheria zao,
mchakato wa kupitisha utakuwa kwenye mikono ya wanasheria na wanasiasa na hivyo
watapendekeza wanavyotaka.
Afisa Mdhamini MCT Zanzibar Shifaa
Said Hassan anasema, pamoja na kuzieleza sheria hizo na mapungufu yake tangu
2010, lakini bado inaendelea kutumika, jambo ambalo linawapa wakati mgumu
katika kuendeleza tasnia ya habari nchini.
"Haya mamlaka aliyopewa Ofisa
Polisi sio sahihi kwa kweli na wala haileti picha nzuri, mimi naona ni udhalilishaji
wa waandishi na vyombo vyetu, tuendelee kuzisemea sheria hizi ili vifungu
vinavyotukwaza viondoshwe", anafafanua Shifaa.
"Ni miaka 12 sasa harakati za
kupigania uwepo wa sheria nzuri za habari zinafanyika kwa maslahi ya jamii na
Taifa kwa ujumla, lakini bado hatujafikia tunapopataka", anasema Zanziba Mzee Mratibu wa Internews Zanzibar
wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar.
Anasema, kuna vifungu vingi ambavyo
vinahitaji kufanyiwa marekebisho ikiwemo cha 27 (1), (3), kwani vinawanyima
waandishi uhuru na kuwakosesha wananchi haki ya kutoa maoni na kujieleza.
Ndio maana Internews kwa sasa
imeshirikiana na wadau wake ikiwemo MCT, TAMWA Zaznibar na waandishi wa habari,
ili kuviibua vifungu vyenye kero na kufanyiwa marekebisho.
‘’Nguzo kubwa ya kuleta mabadiliko
katika kila jambo, basi ni kufanya kazi kwa karibu na vyombo vya habari, kama
tunavyofanya sisi Internews juu ya upatikanaji wa sheria rafiki ya habari
Zanzibar,’’anasema Zaina.
Hata hivyo, amewasisitiza waandishi
kuendea kutengeneza vipindi, Makala, ujumbe mfupi mfupi na habari za kawaida,
ili kuvieleza vifungu kandamizi kwa uhuru wa habari
ATHARI ZA VIFUNGU KANDAMIZI KW
AUHURU W AHABARI ZANZIBAR
Hanifa Salim Mohamed ambae ni
mwandishi wa gazeti la Zanzibarleo Pemba anasema, athari zinazoweza kujitokeza
ni pamoja na waandishi kufanya kazi kwa hofu, hali ambayo itasababisha
kutofanya kazi vizuri.
"Itakuwa hatuko huru katika
utendaji wa kazi zetu, kwa sababu tutafanya kazi kwa woga na hii itapelekea
kushindwa kuibua yale ambayo yanaikwaza jamii", anasema.
Hafidh Abdi Said ambae ni Mwenyekiti
wa CHADEMA Wilaya ya Chake Chake anasema athari yake ni kwamba, watu
watashindwa kutoa maoni yao kwani watahofia kukamatwa pamoja vyombo hivyo vya
habari kufungwa, hivyo hata maendeleo yatakuwa ni duni.
"Vyombo vya habari ndivyo
ambavyo vinaleta maendeleo katika nchi yeyote duniani lakini ikiwa kutakuwa na
sheria ambazo ni kandamizi, tusitegemee kuleta mabadiliko ya kimaendeleo",
anasema.
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya
Mussa Said anasema, athari itakayojitokeza ni kwamba watu watakosa haki yao ya
kujieleza na kupata habari.
"Vyombo vya habari vinapokuwa
huru na hata wananchi watakuwa huru kuelezea yale yanayowakwaza na hapo ndipo
yatakapotatuliwa na kufikia pale tunapopataka ambayo ni nchi yenye
Maendeleo", anaeleza.
Mwanasheria wa Shirika la Magazeti
ya serikali Zanzibar Juma Khamis Juma, anafafanua kuwa, wananchi watakosa
taarifa ambazo ni haki yao kuzipata kwa mujibu wa Katiba.
‘’Sio habari zote zitakazoandikwa
zitawafurahisha hao Maofisa Polisi na wengine, kwa hiyo ikiwa ana chuki na
chombo au mwandishi wa habari, atalikamata gazeti na kulisababisha lisifanye
kazi zake’’, anafafanua.
Tatu Abdalla Mselem ambae ni Mratibu
wa TUJIPE Pemba anasema, waandishi wa habari itakuwa hawafanyi kazi zao vizuri
kwa sababu watakuwa na hofu katika kukusanya, kuandika na kurusha habari zao.
‘’Ilikuwa mamlaka kisheria wapewe
wanahabari wenyewe kwani Ofisa Polisi anaweza kuwa na chuki zake binafsi akatumia
mamlaka anayopewa, Maafisa hao wachukuliwe kama wadau na sio kupewa mamlaka
kwani chombo cha habari ni cha kujitegemea’’, anaeleza.
NINI KIFANYIKE
Mkuu wa taaluma wa Chuo cha uandishi
wa habari na mawasiliano ya Umma Zanzibar Imane Duwe, anasema kwanza kufutwa
kwa sheria hiyo kongwe na kuwa na sheria rafiki kw auhuru wa habari.
Mwananchi Asha Salim Ali mkaazi wa
Wete anasema, ili kuwe na uhuru wa vyombo vya habari kuna haja ya kuvifanyia
maboresho vifungu vyote vinavyominya uhuru wa habari.
Khamis Mohamed mkaazi wa Gombani
Chake Chake anafahamisha kuwa, Ofisa wa Polisi asipewe mamlaka hayo na badala
yake iundwe bodi maalumu ya kuweza kuchunguza tuhuma na itakapothibitika chombo
kimekiuka sheria ndipo kichukuliwe hatua.
"Mimi iliyonishangaza ni hii
kwamba Ofisa Polisi hata akituhumu tu anaweza kukamata gazeti au hata kitabu
cha mwandishi, kwa kweli hii sio sahihi hata kidogo", anafahamisha.
Mwanasheria Ali Amour Makame anashauri,
gazeti hilo litakapokamatwa libaki kwa Mrajisi katika uchunguzi wake ndipo
aweze kubaini kwamba habari gani sio sahihi lakini sio kupewa mamlaka hayo
askari yeyote.
Ali Massoud Kombo anasema, Jeshi la
Polisi lisipewe Mamlaka hayo, hivyo wadau waendelee kutoa mapendekezo ili
kuhakikisha vyombo vya habari vinakuwa huru na hapo ndipo vitafanya kazi zao
vizuri.
Baadhi ya vifungu vya sheria ya Wakala
wa Habari, Magazeti na Vitabu bado vinaminya uhuru wa vyombo vya habari, hivyo
kuna haja ya kufanyiwa maboresho ili waandishi wafanye kazi zao vizuri.
MWISHO.
Comments
Post a Comment