Na Sabiha Keis, Zanzibar
Waziri wa Ardhi na
Maendeleo ya Makaazi Zanzibar Rahma Kassim Ali amesema ongezeko la migogoro ya
Ardhi nchini linasababishwa na baadhi ya wananchi kununua Ardhi kwa kutofuata
sheria na taratibu zilizowekwa.
Kauli hiyo ameitoa
mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti kwa kipindi cha
Julai hadi Disemba 2022 kwa kamati ya Mawasiliano,Ardhi na Nishati ya Baraza la
Wawakilishi huko katika ukumbi wa Wizara hiyo Maisara, Unguja.
“Asilimia 80 ya
migogoro ya Ardhi inatokana na mauziano ya wananchi kuuziana ardhi kinyume na
sheria, na hao wanasheria ndio balaa, kiwanja kimoja kinauzwa mara mbili hata
tatu, afadhali hata masheha wakihusishwa wajua kama kiwanja hichi kimeshauzwa “
Alisema Waziri Rahma.
Alieleza kwamba mbali
na ununuzi huo wa Ardhi usifuata sheria lakini pia ujenzi holela usiozingatia
mipaka halisi ya eneo husika umekua ukichangia kuwepo kwa migogoro hiyo ambapo
Wizara yake imejipanga kwa sasa katika kudhibiti hali hiyo.
Waziri Rahma alisema Wizara
ya Ardhi tayari imeshakaa vikao mbalimbali na Taasisi zinahusiana na wizara yake katika masuala ya Ardhi ikiwemo
Tawala za Mikoa, Mamlaka ya Uwekezaji (ZIPA) pamoja na Wizara ya Kilimo na
kutoka na azimio kuwa vibali vyote vya ujenzi vitolewa katika ofisi moja ili kuondoa
changamoto iliyopo.
Aidha waziri huyo
alisema taasisi yake ya Mahakama ya Ardhi imepokea kesi mpya za migogoro ya
ardhi 108 kwa kipindi cha Julai hadi
Desemba 2022 ambapo kesi 107 zilitolewa maamuzi huku kesi 183 zinaendelea
katika Mahakama hiyo. Kesi hizo ni kwa Unguja na Pemba.
Akizungumzia mikakati
ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Mngereza
Mzee Miraji amefahamisha kwamba licha ya wizara hiyo kukabiliwa na changamoto ya fedha lakini wamejipanga kutafuta
washirika wa maendeleo kwajili ya kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo upimaji
wa ardhi, kujenga nyumba za bei nafuu na usalama wa ardhi.
“Kwanza tulikuwa na
jukumu la kuwa indentify partners, kuangalia jinsi ya kujenga nyumba za low
cost, land tenure security pamoja na kuangalia tuanzie wapi? ”Alisema Dkt
Mngereza.
Aidha Dkt Mngereza amefahamisha
kuwa katika kutatua changamoto ya ujenzi holela Wizara yake tayari
imeshatiliana saini na Kampuni ya Propertie International kutoka Tanzania Bara kwa
ajili ya kushirikiana katika kazi ya kupima na kupanga mji.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano,Ardhi na Nishati Yahya Rashid Abdalla ameipongeza Wizara hiyo
kwa namna inavyofanya kazi zake pamoja na kuishauri Wizara kuhakikisha matumizi ya Ardhi yanalingana na mahitaji husika.
Wizara ya Ardhi na
maendeleo ya Makaazi kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2022 ilikadiriwa
kukusanya jumla ya TZS Billioni 1.168 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya
mapato ndani ya Taasisi zake ambapo hadi kufikia Disemba,2022 jumla ya TZS
Millioni 700.550 zimekusanywa ambazo ni wastani wa asilimia 60 ya makadirio.
Kwa upande wa
matumizi kwa kipindi julai- Disemba 2022,Wizara ilipangwa kutumia jumla ya TZS
Billioni 2.956 kwa ajili ya kazi za kawaida Na mishahara ambapo hadi kufikia
Disemba 2022 Wizara imepatiwa jumla ya TZS Billioni 2.718 ambazo ni wastani wa
asilimia 91.9 ya fedha zilizopangwa.
Mwisho
Comments
Post a Comment