MKURUGENZI wa Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jamila
Mahmoud Juma, amesema mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za udhalilishaji
(database), unasaidia kutambua kasi ya ongezeko au kupungua kwa matukio hayo.
Jamila alieleza hayo huko ofisini kwake
Mpendae Mjini Zanzibar, wakati alipozungumza na mwandishi wa habari hizi,
ambapo alisema mfumo huo unasaidia kuweka kumbukumbuku za matukio hayo.
Mkurugenzi alisema mfumo huo unarahisisha
upatikanaji wa taarifa sahihi za matukio ya vitendo vya udhalilishaji kuanzaia
hatua za ufuatiliaji wa kesi mpaka kufikia mahakamani kwa mashirikano na
mashirika ya serikali na taasisi mbalimbali.
Jamila alisema tangu kuzinduliwa kwa mfumo
huo mwaka 2021 na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Hussein Ali Mwinyi, mfumo huo umekuwa msaada mkubwa wa kujua taarifa kwa
taasisi zilizomstari wa mbele kwenye mapambano dhidi ya vitendo vya
udhalilishaji.
“Mfumo huu ni muhimu na una faida kwa jamii
katika kupata taarifa sahihi dhidi ya kesi za matukio ya vitendo vya udhalilishaji
ambapo kesi hizo huripotiwa na taasisi zilizomo katika mfumo huo kama vile kituo cha huduma za sheria,
wasaidizi wa sheria, Polisi na Mahakama, kwani kila mmoja kwa nafasi yake ana
nafasi ya kushiriki katika uwekaji wa taarifa za matukio ya vitendo vya
udhalilishaji”, alisema.
Akizungumzia takwimu za vitendo hivyo kupitia
mfumo huo alisema kwa upande wa ZAFELA
peke yake wastani kila mwezi matukio 40 ya kesi tofauti zikiwemo kesi za udhalilishaji,madai ya
mahari,talaka na ukaazi wa mtoto huorosheshwa
kwa kuingizwa kwenye mfumo huo ingawa alisema changamoto iliyopo
kwa sasa, ni kwa taasisi nyengine
kutoingiza taarifa za takwimu zao hali ambayo inarudisha nyuma lengo
walilojipangia la kuwa na mfumo wa pamoja wa ukusanyaji wa taarifa.
Alielezea sababu zinazopelekea
taasisi hizo kutoweka taarifa za vitendo hivyo katika mfumo
huo ni kutokana na hofu ya usalama kutokana na unyeti wa taarifa
hizo kwa kuhofia nani anazipokea? na wapi zinakwenda? Sambamba na uhaba wa fedha kwa baadhi ya taasisi
kushindwa kuingiza taarifa zao kwasababu mfumo huo unatumia gharama za
kimtandao.
Fatma Khamis Ame ambae ni msaidizi wa
sheria kutoka Jumuiya ya Wasaidizi wa sheria Zanzibar (ZAPAO), alisema mfumo
huo unasaidia kurahisisha shughuli zao
za kisheria kwa kutambua wajipange vipi kulingana na kesi tofauti
za vitendo vya udhalilishaji
zinazoendelea kutokezea.
Kutokana na
changamoto ya mfumo huo iliyopo hivi sasa, Alitoa ushauri kwa ZAFELA
kuitisha kikao cha pamoja cha wadau
wote wanaopinga vitendo hivyo ili kuja na Suluhisho la changamoto
zinazojitokeza kupitia mfumo huo ikiwemo
changamoto ya mfumo kudai kitambulisho hali ambayo imekua ikiwarudisha nyuma.
Comments
Post a Comment