NA
HAJI NASSOR, PEMBA:::
UONGOZI
wa kampuni ya ulinzi ya Active Security with
Integrity ‘ASI’ umeziomba tasisiza serikali na zile za watu binafsi, kuwatumia
katika ulinzi wa maeneo yao mbali mbali, kwani vijana wao, wanayo mafunzo ya
kutosha ya kazi hiyo.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo
Salim Khamis Juma, wakati akizungumza hospitali ya Coteji Vitongoji wilaya ya
Chake chake, mara baada ya kumalizika kazi ya usafi, iliyofanywa na watendaji
wa kampuni hiyo.
Alisema, baada ya kusajiliwa rasmi serikalini na kwenye
taasisi zake nyingine, sasa ni wajibu wa tasisi mbali mbali kuwatumia wao
katika ulinzi.
Alieleza kuwa, tayari zipo tasisi chache wameshaanza
kuwatumia, lakini kwa idadi ya vijana walionao, ni vyema na tasisi nyingine
kuona umuhimu huo.
Mkrugenzi huyo alieleza kuwa, ili kufikia azma ya
serikali ya ajira 300,000 zilizotangaazwa na rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali
Mwinyi, basi ni kuwapatia ajira vijana wa kampuni yao ya ‘ASI’.
‘’Kama tasisi za serikali na zile za watu binafsi
watatumia sisi katika ulinzi, ni sehemu ya kuisaidia serikali kuu, katika kuwapatia
vijana ajira, kwani za serikali haiwezi kutupata ajira sote,’’alieleza.
Akizungumza suala la zoezi la usafi walilolifanya
hospitalini hapo, alisema ni sehemu ya malengo ya kampuni, kushrikiana na
serikali kuu katika kuimarisha usafi.
‘’Kampuni ya ‘ASI’ kufanya usafi huu ni sehemu ya kuunga
mkono juhudi na mawazo ya rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, ambae ni
muumini wa usafi wa mazingira,’’alifafanua.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema, zoei kama hilo litakuwa endelevu
katika maeneo mbali mbali, kwani pamoja na kazi za ulinzi, lakini suala la
usafi ni kipaumbele chengine.
Katibu wa Hospitali hiyo Dk. Nassir Suleiman Hamad,
alisema wazo la kampuni hiyo ya ‘ASI’ kufanya usafi katika eneo la wagonjwa, ni
jambo jema mno, maana ni njia moja wapo ya kukimbiza maradhi.
‘’Kampuni hii pamoja na kwamba ni ya ulinzi, lakini
kumbe inaashiria kuwa, inapenda kulinda kwenye eneo safi, na mmekuwa mabalozi
wetu katika kuyakimbia magonjwa mbali mbali,’’alieleza.
Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mdhamini wa wizara ya
Afya Pemba, Daktari dhamana wa hospitali hiyo, Fahad Ali Khamis, aliiomba
kampuni hiyo, kuendelea na kazi za usafi kila baada ya muda.
‘’Kampuni hii ni ya ulinzi, lakini kufanya kwenu usafi
sisi hili limetuvutia, na ikitokezea bahati ya kutaka watendaji wa kudumu wa kazi
hii, itakuwa rahisi kuwasiliana,’’alieleza.
Mapema mkuu Mafunzo na nidhamu wa wa kampuni hiyo ya
ulinzi ya Active Security with Integrity ‘ASI’ Khamis Salim Khamis, alisema
kampuni kwa sasa inafanyaka kazi zake kisheria.
Hata hivyo alieleza kuwa, pamoja na kazi hiyo ya ulinzi,
imejiegemeza katika kutoa huduma bure kwa jamii, ikiwemo ya usafi, ili kuwa na
taifa lenye afya bora.
Nae mlezi wa kampuni hiyo Mussa Salim Nassor, aliwapongeza
vijana hao kwa kushiriki katika kazi hiyo ya kujitolea na kuwataka wasisite
kila wanapoitwa.
‘’Moja ya jambo ambalo vijana wengi wamelikosa katika
miaka ya hivi karibuni ni jambo la uzalendo wa kujitolea, lakini hawa kwa
kampuni ya ‘ASI’ naona muko vizuri, hongereni sana,’’alieleza.
Baadhi ya vijana walioshiriki kwenye zoezi hilo la
usafi, walipongeza hatua ya uongozi wao, kubuni jambo hilo, ambalo ni
kuwasaidia wagonjwa kuishi kwa utulivu.
Kampuni ya ulinzi ya Active Security with Integrity ‘ASI’
ambayo imeanzishwa mwaka 2020, moja ya malengo yake ni kutoa huduma ya ulinzi,
na tayari imeshaajiri vijana 12.
Mwisho
Comments
Post a Comment